Nav bar

Jumatatu, 19 Aprili 2021

KAMPUNI YA ISRAEL YAANZA MAZUNGUMZO YA AWALI YA UWEKEZAJI KATIKA SEKTA YA MIFUGO NCHINI

Na. Edward Kondela.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amekutana na kufanya mazungumzo ya awali na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Smart Holding ya nchini Israel Bw. Avi Postelnik yenye lengo la kuwekeza hapa nchini kupitia sekta mbalimbali zikiwemo za mifugo na uvuvi.


Akizungumza jana (16.04.2021) mara baada ya kuhitimisha mazungumzo yao ya awali katika ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo jijini Dar es Salaam, Prof. Gabriel amesema katika mazungumzo yao wameainisha fursa kubwa zilizopo hapa nchini ikiwemo ya unenepeshaji mifugo na uongezaji thamani wa bidhaa zitokanazo na mazao ya mifugo.


Amesema nchi ya Israel ina ng’ombe ambao wana uwezo wa kutoa lita 40 hadi 50 za maziwa kwa siku moja na kwamba Bw. Postelnik amewaona ng’ombe wa aina hiyo hapa nchini katika Mkoa wa Kagera.


“Kwa bahati nzuri tayari kosaafu hiyo ya ng’ombe ameiona hapa Tanzania katika Mkoa wa Kagera na tuna dume la ng’ombe kutoka nchini Israel, ambalo lipo katika Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC) kilichopo Mkoani Arusha.” Amefafanua Prof. Gabriel


Aidha, ameongeza kuwa mkakati mzuri ukiwekwa baina ya Tanzania na Israel katika kukuza sekta ya mifugo hapa nchini, wafugaji wanaweza kupata faida kubwa hasa baada ya Israel kuwa na teknolojia ya kutengeneza malisho ya mifugo kwa kutumia mabaki ya mazao ya mifugo.


Katika mazungumzo hayo wamegusia umuhimu wa masoko ya bidhaa za mifugo na uvuvi, ambapo wamekubaliana kuwa na masoko ya bidhaa za mifugo na uvuvi katika nchi mbalimbali kutatoa hamasa zaidi kwa wafugaji na wavuvi kuzalisha zaidi bidhaa zao.


Katika mazungumzo hayo ya awali ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Smart Holding ya nchini Israel Bw. Avi Postelnik wamesema eneo ambalo wanalipa kipaumbele kwa sasa katika sekta ya mifugo ni ufugaji wa ng’ombe na uzalishaji wa mazao yatokanayo na ng’ombe ukifuatiwa na ufugaji wa kuku.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel akiagana na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Smart Holding ya nchini Israel Bw. Avi Postelnik mara baada ya Bw. Postelnik kufika katika ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya mazungumzo ya awali na katibu mkuu huyo juu ya nia ya kampuni yake kuwekeza katika sekta za mifugo na uvuvi. (16.04.2021)


Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Smart Holding ya nchini Israel Bw. Avi Postelnik (wa kwanza kulia) akifafanua jambo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel na Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka katika wizara hiyo Prof. Hezron Nonga, mara baada ya Bw. Postelnik kufika katika ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya mazungumzo ya awali na katibu mkuu huyo juu ya nia ya kampuni yake kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini zikiwemo za mifugo na uvuvi. (16.04.2021)


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel akimsindikiza Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Smart Holding ya nchini Israel Bw. Avi Postelnik mara baada ya kumaliza mazungumzo yao ya awali katika ofisi ndogo za wizara hiyo zilizopo jijini Dar es Salaam yenye lengo la kampuni hiyo kutaka kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini ikiwemo ya mifugo kwa kuanzia na ufugaji wa ng’ombe na uongezaji thamani wa mazao yatokanayo na mifugo hiyo. (16.04.2021)

Picha ya pamoja ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati), Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Smart Holding ya nchini Israel Bw. Avi Postelnik na Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka katika wizara hiyo Prof. Hezron Nonga, mara baada ya Bw. Postelnik kufika katika ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya mazungumzo ya awali na katibu mkuu huyo juu ya nia ya kampuni yake kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini zikiwemo za mifugo na uvuvi. (16.04.2021)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni