Nav bar

Alhamisi, 4 Februari 2021

WAFUGAJI, WAFANYABIASHARA ‘WAILILIA’ SERIKALI VIFO VYA NGURUWE

Na Mbaraka Kambona, Kahama.

 

Wafugaji na wafanyabiashara wa nguruwe na mazao yake wanaofanya shughuli zao Wilayani Kahama, Mkoani Shinyanga wameiomba Serikali kuendelea kuchukua hatua za haraka kuudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa Homa ya Nguruwe ulioikumba wilaya hiyo na kuathiri kwa kiasi kikubwa shughuli zao za kiuchumi.

 

Wafugaji na wafanyabiashara hao walitoa ombi hilo Januari 26, 2021 wakati walipokuwa wakiongea na Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Hezron Nonga alipokwenda Wilayani Kahama kwa ajili ya kuongeza nguvu kwa timu iliyoundwa na Serikali ya kudhibiti ugonjwa huo.

 

Wakiongea kwa nyakati tofauti, wafugaji na Wafanyabiashara hao walisema kuwa tangu ugonjwa huo uingie katika wilaya ya Kahama umesababisha hasara kubwa kwa wafugaji na wafanyabiashara kwa sababu nguruwe wengi wamekufa huku biashara ya mazao ya nguruwe hususan uuzaji wa nyama ukizorota kwa kiasi kikubwa.

 

Wilson Sawa, Mmiliki wa Baa na Muuza nyama ya nguruwe wilayani Kahama alisema kuwa biashara ya nyama ya nguruwe imekuwa ikisaidia biashara nyingine lakini tangu kusitishwa kwa biashara hiyo baa nyingi ambazo zinauza nyama ya nguruwe hazifanyi vizuri.

 

“Kusitishwa kwa biashara hii kumeathiri uchumi wetu kwa sehemu kubwa, tunaiomba serikali iharakishe kuudhibiti ugonjwa huu na iendelee kufanya tathimini ya maendeleo ya ugonjwa ili kama unapungua waturuhusu tuendelee kufanya biashara,” alisema Sawa.

 

Naye, Pendo Emmanuel, mmliki wa bucha ya nyama ya nguruwe katika wilaya hiyo alisema kabla ya ugonjwa huo kwa siku alikuwa anauza hadi kilo 80 kwa bei ya jumla na rejareja lakini kwa sasa baada ya ugonjwa hakuna biashara anayoifanya.

“Kwa kweli ugonjwa huu umeathiri kwa kiwango kikubwa katika kuendesha Maisha yangu, siwezi kupeleka watoto shuleni, tunaiomba Serikali ione itakavyoweza kutusaidia ili tuweze kuendesha maisha yetu,” alisema Emmanuel.

 

Frank Kimaro, Mfugaji wa Nguruwe, Wilayani Kahama alisema kuwa kutokuwepo na sehemu rasmi ya kuchinjia Nguruwe kumechangia kwa namna moja au nyingine katika kusambaza ugonjwa huo kwa sababu wakati wote wamekuwa wakichinja nguruwe wao katika maeneo yalipo mabanda yao.

 

“Ombi langu kwa Serikali ituwekee sehemu itakayokuwa maalum kwa ajili ya kuchinja nguruwe wetu hii itasaidia kudhibiti milipuko ya magonjwa lakini Serikali nayo itapata mapato yake,”alisema Kimaro

 

Akizungumza kuhusu hali halisi ya kuenea kwa ugonjwa huo wa homa ya nguruwe, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji, Kahama, Anderson Msumba alisema kuwa Serikali ipo kazini kuhakikisha ugonjwa huo unadhibitiwa haraka ili shughuli za ufugaji na biashara ya nguruwe na mazao yake ziweze kuendelea kama kawaida.

 

Aliongeza kwa kusema kuwa tangu Serikali ilipoingilia kati sakata la ugonjwa huo kwa kupeleka timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuungana na wataalam wa Halmashauri idadi ya vifo imeanza kupungua na anaamini kwa juhudu zinazoendelea ugonjwa huo sio muda mrefu utakoma.

 

“Nitoe wito kwa wafugaji kuendelea kutoa ushirikiano kwa timu ya wataalam ambayo imewekwa na Serikali kwa ajili ya kusaidia kutokomeza ugonjwa huo ikiwemo kuhakikisha mifugo yao haitoki nje ya mabanda yao, na wasiwe na tamaa, waache kuchinja nguruwe wagonjwa kwa sababu atakayebainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” alisisitiza Msumba.

 

Aidha, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Hezron Nonga pamoja na kutoa elimu ya kina kuhusu hatua za kuchukua katika kudhibiti ugonjwa huo usisambae, pia aliwataka wafugaji na wale wote wanaojihusisha na biashara ya nguruwe kuzingatia masharti ya karantini iliyowekwa na Serikali na atakayekaidi agizo hilo la Serikali sheria itachukua mkondo wake.

Alisema kuwa Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Na. 17 ya Mwaka 2003 inazuia shughuli za uchinjaji na usambazaji wa mifugo na mazao yake katika maeneo yenye mlipuko wa magonjwa, na yeyote atakayekwenda kinyume na Sheria hiyo akibainika atapewa adhabu ya papo kwa papo ya faini ya shilingi milioni tano (5) au akipelekwa Mahakamani na kupatikana na hatia atahukumiwa adhabu yake ni kulipa faini ya shilingi milioni kumi (10) au kifungo cha mwaka mmoja jela au vyote kwa pamoja.

Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mifugo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Hezron Nonga (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Timu ya Wataalam iliyoundwa na Serikali ya kudhibiti mlipuko wa homa ya Nguruwe pamoja na Wafugaji na Wafanyabiashara wa Nguruwe na mazao yake muda mfupi baada ya kufanya kikao cha kuwaelimisha wafugaji na wafanyabiashara hao hatua za kuchukua ili kudhibiti ugonjwa huo usisambae zaidi. Kikao hicho kilifanyika Wilayani Kahama Januari 26, 2021.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji, Kahama, Anderson Msumba (kulia) akiongea na Sehemu ya Timu ya Wataalam iliyoundwa na Serikali kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa ajili ya kwenda kuungana na Wataalam wa Halmashauri kudhibiti mlipuko wa homa ya Nguruwe ulioikumba Wilaya ya Kahama Januari 26, 2021.

Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mifugo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Hezron Nonga akimfanyia uchunguzi wa Afya Nguruwe katika moja ya Mabanda yaliyopo Wilayani Kahama, Mkoani Shinyanga Januari 25, 2021. Prof. Nonga alikwenda Wilayani  humo kwa ajili ya kuongeza nguvu kwa Timu iliyoundwa na Serikali kwa  ajili ya kudhibiti Mlipuko wa Ugonjwa wa homa ya Nguruwe uliyoikumba Wilaya ya Kahama.

Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Hezron Nonga (kulia) akionesha damu iliyovilia katika sikio la Nguruwe ikiwa ni moja ya kiashiria kuwa Nguruwe huyo ana homa kali alipotembelea banda mojawapo la Mfugaji lililopo Wilayani Kahama, Mkoani Shinyanga Januari 25, 2021. Kushoto ni Muhudumu wa Banda hilo Philipo Joseph.

Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Hezron Nonga (kulia) akichukua namba ya simu ya Mfugaji wa Nguruwe Wilayani Kahama, Mkoa wa Shinyanga, Stella Ngowi kwa ajili ya kufanya ufuatiliaji wa hali ya Mifugo yake alipomtembelea nyumbani kwake Januari 25, 2021.

Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Hezron Nonga akiwakagua Nguruwe wadogo waliosongamana sehemu mmoja wakiwa wanahisi baridi kali baada ya kupata homa kali katika banda la mmoja wa wafugaji lililopo Wilayani Kahama, Mkoani Shinyanga Januari 25, 2021.







Hakuna maoni:

Chapisha Maoni