Nav bar

Ijumaa, 5 Februari 2021

TAASISI ZA FEDHA ZAIPONGEZA SERIKALI KUFUFUA TAFICO, ZAAHIDI KUTOA MTAJI

Na Mbaraka Kambona,

 

Taasisi za fedha nchini zimeipongeza Serikali kwa maamuzi ya kulifufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) na kulipa tena nafasi ya kuweza kusimamia mnyororo wa thamani wa zao la Samaki huku wakiahidi kutoa mtaji ili kuliimarisha shirika hilo.

 

hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mtendaji, Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), Japhet Justine alipokuwa akiongea na Waandishi wa Habari muda mfupi baada ya kumaliza kikao kazi cha kujadili maeneo ya uwekezaji ya Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) kilichofanyika jijini Dodoma Februari 2, 2021.

 

Akiongea kwa niaba ya Viongozi wengine wa taasisi za fedha waliohudhuria kikao hicho, Justine alisema kuwa TAFICO ni shirika kubwa linaloshikilia mnyororo mzima wa thamani wa samaki hivyo kufufuliwa kwa shirika hilo kutawasaidia wavuvi kuwa na masoko ya uhakika.

 

“Tunaipongeza Serikali kwa maamuzi haya makubwa ya kulifufua shirika hili, na sisi tumewahakikishia kushirikiana nao katika kutoa mitaji ambayo itaanzia kwa TAFICO yenyewe na wale wote wanaojihusisha katika mnyororo huu wa thamani ikiwemo wavuvi, wasafirishaji na watengeneza barafu,” alisema Justine

 

Alisema kwa sasa kuna wananchi zaidi ya laki mbili (200,000) wanaojihusisha na uvuvi na kuongeza kuwa hao wote wataenda kuwafungamanisha katika mnyororo huo wa thamani.

 

Aliongeza kuwa kufufuliwa kwa shirika hilo kutaongeza fedha za kigeni, uhakika wa kupata masoko makubwa ya kimataifa ambayo yataleta mikataba ya kibiashara itakayowarahisishia wadau walioko katika sekta ya uvuvi kukopeshwa mitaji.

 

“Tunaamini mabenki ambayo yalikuwa yanapata shida kupata mikataba ya kuweza kuwapatia wafanyabiashara wadogowadogo mitaji, sasa kwa kupitia mikataba ya TAFICO italeta ahueni kubwa na kupunguza madhila yaliyokuwa yanazuia mabenki kutoa mitaji,” alifafanua Justine

 

“Sisi kama taasisi za fedha ikiwemo mabenki, Kituo cha Uwekezaji na Mifuko ya Pensheni tumekubaliana tutaweka nguvu kwa pamoja kuhakikisha miradi yote kumi (10) iliyobuniwa na TAFICO inayoangazia kutengeneza mazingira thabiti ya uvuvi inasimama kwa awamu nyingine tena ili tija ya shirika hilo iweze kuonekana,” alisisitiza Justine

 

Naye, Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah alisema kuwa uendeshaji wa shirika hilo kwa awamu hii utakuwa ni wa ubia kati ya Serikali na sekta binafsi.

 

Aliongeza kuwa kwa miaka mingi tangu uhuru haukuwepo uwekezaji katika bahari kuu huku akisema kuwa ni mategemeo yao kuwa uwekezaji ukianza katika uvuvi wa bahari kuu samaki wataongezeka mara tatu zaidi ya wanaopatikana sasa.

 

Dkt. Tamatamah alisema kuwa shirika hilo likianza kufanya kazi sekta ya uvuvi itaimarika na pia litasaidia kuzuia uvuvi haramu na kulinda rasilimali za uvuvi katika bahari kuu.

 

Taasisi zilizoshiriki kikao hicho ni Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), Benki ya CRDB, Benki ya NMB, na Benki ya Posta (TPB).

 

Nyengine ni Kituo cha Uwekezaji, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (katikati) akiongea na Washiriki wa kikao kazi cha kujadili maeneo ya uwekezaji ya Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) kilichofanyika jijini Dodoma  Februari 2, 2021.


Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi (WMUV), Magese Bulayi akifafanua jambo katika kikao kazi cha kujadili maeneo ya uwekezaji ya Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) kilichofanyika jijini Dodoma Februari 2, 2021.

Sehemu ya Washiriki wa Kikao kazi cha kujadili maeneo ya uwekezaji ya Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) wakipitia nyaraka mbalimbali katika kikao hicho kilichofanyika jijini Dodoma Februari 2, 2021.

Mkurugenzi Mtendaji, Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), Japhet Justine akiongea na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao kazi cha kujadili maeneo ya uwekezaji ya Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) kilichofanyika jijini Dodoma Februari 2, 2021.

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (wa sita kutoka kulia-mstari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Taasisi za fedha na  baadhi ya Wakurugenzi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao cha kujadili maeneo ya uwekezaji ya Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) kilichofanyika jijini Dodoma Februari 2, 2021.





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni