Nav bar

Alhamisi, 18 Februari 2021

MAWAKALA WA KUKU WASIOTAMBULIKA KUKAMATWA

Na. Edward Kondela

 

Chama cha Wafugaji wa Kuku wa Nyama  nchini (TABROFA) kimetakiwa kuwa na ushirikiano ili kutokomeza changamoto wanazozipata wafanyabiashara wa kuku hasa mawakala wasiotambulika wanaouza vifaranga vya kuku wa nyama pamoja na vyakula vya kuku kwa bei ya juu katika maeneo mbalimbali nchini.

 

Akizungumza katika mkutano wa wafanyabiashara na wazalishaji wa vifaranga vya kuku wa nyama jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amesema mawakala wanaotumiwa na wenye viwanda vya kutotolesha vifaranga kama hawajasajiliwa wakamatwe.

 

“Kuanzia sasa mawakala wa wauzaji wa vifaranga vya kuku pamoja na chakula cha kuku nataka wafuatiliwe na waeleze wapi walisajiliwa”. Amesema Mhe.Ndaki.

 

Aidha, Mhe. Ndaki amewataka wafugaji wote wanaouza kuku wa nyama  kujisajili  Bodi ya Nyama nchini (TMB) kwa ajili ya biashara kwani hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa atakayekaidi.

 

Pia, waziri huyo amewataka wafugaji wa kuku wa nyama kuanza kuuza kuku kwa uzito badala ya kukadiria ili waweze kuendana na gharama halisi za ufugaji na kupata faida ili ufugaji uwe na tija kwao na kutaka TABROFA kusimamia hilo na kuwachukulia hatua wafugaji watakaoenda kinyume na hilo.

 

Ameongeza kuwa sekta ya ufugaji ni muhimu kwa pato la nchi na kuwataka wataalamu wa mifugo kufanya tafiti za mifugo kwa kuwalenga wafugaji wenyewe kwa kubaini changamoto zao sio kuwatumia wasomi.

 

“Tuache kufanya tafiti kwa kuwatumia bwana shamba na bibi shamba ambao hawafikishi ujumbe kwa wafugaji  kuhusu elimu dhidi ya tafiti zilizofanyika,” ameeleza.

 

Naye Kaimu Msajili wa Bodi ya Nyama Bw. Imani Sichwale amewataka wafugaji hao kuacha kufuga kuku kwa mazoea bali wafuge kitaalamu kwa kuweka bajeti ya ufugaji kwa lengo la kukuza tasnia yao.

 

Hata hivyo Bw. Sichwale amesema kuwa nyama inasoko nje ya nchi kuliko kuku kwa sababu haijapata vigezo vya uuzaji nje ya nchi.

 

Amesema asilimia 80 ya wafugaji wa kuku wa nyama ni wanawake hivyo amewataka kushikilia tasnia hiyo kwa lengo la kuondoa umaskini kuanzia ngazi ya familia hadi taifa kwa ujumla.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji wa Kuku wa Nyama nchini (TABROFA) Bw. Costa Mrema amesema katika tafiti walizozifanya zimebaini kuwa ulaji wa kuku wa nyama Tanzania ni kati ya kuku laki 9 hadi milioni 1.2 kwa wiki.

 

“Idadi hiyo 70% ya walaji wa kuku wa nyama ni katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani ikifuatiwa na mikoa ya Arusha, Mwanza, Kilimanjaro na Dodoma”. Amesema Bw. Mrema.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza katika mkutano wa wafanyabiashara na wazalishaji wa vifaranga vya kuku wa nyama jijini Dar es Salaam, ambapo ameagiza kuchukuliwa hatua kwa mawakala wa kuku wasiotambulika pamoja na kuagiza Chama cha Wafugaji wa Kuku wa Nyama nchini (TABROFA) kuwataka wanachama wake kuuza kuku kwa uzito badala ya kukadiria. (17.02.2021)

Kaimu Msajili wa Bodi ya Nyama nchini (TMB) Bw. Imani Sichalwe akiwataka wafugaji wa kuku kujisajili katika bodi hiyo ili kufanya shughuli ya ufugaji kuwa rasmi kwao na kuweza kupata fursa mbalimbali zinazojitokeza pamoja na kusaidiwa kutatua changamoto zinazowakabili. (17.02.2021)


Mkurugenzi Msaidizi Ukaguzi wa Nyama na Mazao Yake kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Gibonce Kayuni, akiwataka wafugaji wa kuku wa nyama (hawapo pichani) kuweka kumbukumbu sahihi za ufugaji, kushirikisha wataalamu na kuishirikisha wizara katika msaada wa kisheria mara wanapopata hasara kutokana na kuuziwa vifaranga visivyo na sifa.  Dkt. Kayuni amebainisha hayo katika mkutano wa wafanyabiashara na wazalishaji wa vifaranga vya kuku wa nyama jijini Dar es Salaam. (17.02.2021)

Mtendaji Mkuu Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) Dkt. Pius Mwambene akizungumza katika mkutano wa wafanyabiashara na wazalishaji wa vifaranga vya kuku wa nyama jijini Dar es Salaam na kuwataka wafugaji kujiunga LITA ili wapatiwe elimu bora ya ufugaji. (17.02.2021)

Baadhi ya wafugaji wa kuku wa nyama jijini Dar es Salaam, wakionesha mzani unaoweza kupima kuku kwa mara moja kuanzia Kilogramu mbili hadi 300 na kuiomba serikali kusimamia azma yao ya kuuza kuku kwa uzito badala ya bei ya kukadiria ambayo imekuwa ikiwapa hasara kubwa na kushindwa kuendelea na ufugaji. (17.02.2021)

Baadhi ya washiriki wa mkutano wa wafanyabiashara na wazalishaji wa vifaranga vya kuku wa nyama jijini Dar es Salaam, wakisikiliza hoja mbalimbali ambazo zilikuwa zikiwasilishwa ambapo mgeni rasmi katika mkutano huo alikuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki. (17.02.2021)





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni