Nav bar

Ijumaa, 8 Januari 2021

HALMASHAURI ZASHAURIWA KUTUMIA BMU KUKUSANYA MAPATO YA UVUVI

Na Mbaraka Kambona,

 

Mratibu wa Mradi wa Usimamizi wa Rasilimali za Bahari Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish), Dkt. Nichrous Mlalila ameziomba Halmashauri kuvitambua Vikundi vya Ulinzi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) na kuzipa uwezo wa kukusanya mapato yatokanayo na shughuli za uvuvi ili ziweze kusaidia vikundi hivyo kujiendesha na kuendeleza sekta ya uvuvi nchini.

 

Dkt. Mlalila alitoa rai hiyo katika ziara ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi ya BMU inayojengwa na Mradi wa SWIOFish katika Kata ya Dunda, Wilayani Bagamoyo Januari 7, 2021.

 

Kwa mujibu wa Dkt. Mlalila sehemu kubwa ya mapato yanayokusanywa kwa sasa na Halmashauri hayarudishwi kwa Jamii ya wavuvi kwa ajili ya kuendeleza shughuli za sekta na uchumi wa jamii husika.

 

Dkt. Mlalila alisema anatambua kuwa kuna changamoto ya kisheria ambayo baadhi ya Halmashauri zimetumia kuzizuia BMU kukusanya mapato yanayotokana na rasilimali za uvuvi.

 

“Tunahamasisha Halmashauri kuwapa uwezo BMU kukusanya mapato ili kuziwezesha kupata kipato cha uhakika cha kuendesha shughuli zao za kulinda rasilimali za Uvuvi lakini pia mapato hayo yatawezesha kuendeleza sekta ya uvuvi tofauti na ilivyo sasa,” alisema Dkt. Mlalila

 

Katika baadhi ya Halmashauri ambazo wamewapa kazi BMU ya kukusanya mapato kama vile Halmashauri ya Wilaya ya Pangani, Mkoani Tanga, Mapato yanayotokana na uvuvi yameongezeka kutoka shilingi milioni 9 kwa robo mwaka hadi milioni 51 na kutoka shilingi milioni 36 hadi milioni 256 kwa mwaka.

 

“Nazishauri Halmashauri nyingine zichukue mfano wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani kwa sababu sisi tumezipa mafunzo ya kina hizi BMU katika kusimamia fedha na ukusanyaji wa mapato, hivyo tunaamini hilo ni suala la mchakato na tumewasilisha andiko TAMISEMI ili kuangalia namna ya kuzifanya BMU kuendelea na shughuli zake hata pale ambapo mradi wa SWIOFish utakapokwisha muda wake,” aliongeza Dkt. Mlalila

 

Akizungumzia suala hilo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul alisema kuwa BMU ya kata ya Dunda na zingine zikajifunze Pangani kuona wao wanafanyaje na sisi kama Wizara tutaangalia kama kuna chanzo ambacho wataalam wa Halmashauri wanakusanya na hakifanyi vizuri na kuna BMU mahali inakusanya vizuri basi tutaibua hiyo hoja tuone tutafanyaje.

 

“Ukweli ni kwamba kwenye vyanzo hivi vya leseni na ushuru wa rasilimali za uvuvi katika halmashauri zetu nyingi hazifanyi vizuri na hivyo kuna haja ya kuviangalia vizuri hasa wataalam wetu wanaotumika kukusanya hayo mapato kwa sababu kuna baadhi yao wamefanya hapo ndio maeneo yao ya kupatia pesa zao,” alisema Gekul

 

Alisema Wakurugenzi wanaweza kuwa na nia njema kabisa lakini wale wanaotumwa kukusanya hayo mapato wanarudisha maduhuli hayo kama walivyotumwa? Kama kuna watu wanauwezo wa kukusanya zaidi ya wataalam wa Halmashauri sidhani kama kuna haja ya kuwa na kigugumizi cha kuwatoa hao watu ili kazi hiyo apewe anayeweza kukusanya vizuri.

 

“Kwa sababu mwisho wa siku sisi wananchi tunachotaka ni maendeleo hivyo nisingependa niseme moja kwa moja hapa kuwa BMU wapewe kazi hiyo isipokuwa Halmashauri ziangalie kama sheria inawaruhusu kuwatumia BMU kukusanya mapato,” aliongeza Gekul

 

Gekul alisema kuwa wao kama Wizara watawasiliana na TAMISEMI kuona maelekezo yakoje kwa sababu anasema kuna vyanzo Halmashauri zenyewe zinakusanya na vingine vinaruhusiwa kukusanywa na wakala na pale ambapo BMU itaonekana inafaa ipewe uwezo wa kukusanya.

 

Mradi wa SWIOFish unafadhiliwa na Benki ya Dunia kuhamasisha ulinzi na usimamizi wa rasilimali za bahari na ndio umeimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi wa rasilimali za bahari (BMU) kwa ajili ya kulinda na kuhamasisha uvunaji endelevu wa rasilimali za bahari katika Wilaya za Mkinga, Pangani, Bagamoyo, Lindi Vijijini na Tanga Jiji.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (kushoto) akitoa maelekezo kwa Mratibu wa Mradi wa Usimamizi wa Rasilimali za Bahari Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish), Dkt. Nichrous Mlalila (kulia) alipotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi ya Kikundi Cha Ulinzi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) katika kata ya Dunda, Wilayani Bagamoyo Januari 7, 2021.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Ulinzi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU), Kata ya Dunda, Wilayani Bagamoyo, Isihaka Hudi (kulia) akimueleza jambo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (kushoto) alipotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa Ofisi ya BMU hiyo Januari 7, 2021.

Mratibu wa Mradi wa Usimamizi wa Rasilimali za Bahari Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish), Dkt. Nichrous Mlalila akimueleza jambo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (kushoto) alipotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi ya Kikundi cha Ulinzi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) inayojengwa katika Kata ya Dunda, Wilayani Bagamoyo Januari 7, 2021.





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni