Nav bar

Ijumaa, 22 Mei 2020

UKIFUGA KISASA HUWEZI KULALA NJAA. - MRUTTU





Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Hassan Mruttu amesema wafugaji wakifuga kisasa kwa kunenepesha na kuvuna mifugo yao ni rahisi kupata masoko ndani na nje ya nchi kwani watu wengi wanategemea bidhaa za ng'ombe.



Ameyasema hayo wakati akiongea na  wafugaji kwenye kijiji cha Nkerenge Wilaya ya  Misenyi Mkoani Kagera, (12/05/2020) Dkt. Mruttu amesema faida kuu za kufuga kwa mkakati ni pamoja na kupata masoko ya uhakika kutokana na  ng'ombe atakuwa akijiuza na sio kutafuta mnunuzi kwani  muonekano wake tuu utamvutia mnunuzi.



" Biashara ya mifugo ni nzuri na inafaida sana kwani mfugaji hawezi kulala njaa hata siku moja, inamuwezesha mfugaji kuvuna, kuuza na kufanya mambo ya maendeleo." Amesema Dkt. Mruttu



Aidha Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti Tanzania (TALIRI) Bi. Neema Urassa amehimiza wafugaji kuendelea kuwekeza kwenye lishe bora ya ng'ombe na kufuga kwa kufuata kanuni bora za ufugaji ili kupata faida zaidi na kuwataka wafugaji wanaofuga kwa kutumia mfumo huria kufuga ng'ombe katika eneo kwa kuzingatia uwiano wa idadi ya ng'ombe na malisho.



" Hii itachochea uwezo wa ng'ombe kuzalisha mazao bora ya Nyama, maziwa, ngozi na bidhaa zitokanazo na usindikaji wa mazao hayo  kupata soko la uhakika" Amesema Bi Neema



Hata hivyo Bi. Neema ameongeza kuwa ng'ombe ni kama kiwanda kwani ana uwezo wa kula na kutunza chakula (nyasi na vyakula vingine) na kuvibadilisha kuwa nyama, maziwa, ngozi na mbolea kwa ajili ya matumizi ya binadamu.



" Kinyesi cha ng'ombe ni chanzo cha nishati ya bayogesi kwa matumizi mbalimbali ya nyumbani na kuwa faida hizi zote zinampatia mfugaji uwezo wa kuongeza pato la kaya na kuchangia katika ukuaji wa uchumi.



Naye Mtafiti kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Atupele Mohammed amewapongeza wafugaji kwa kukubali na kutumia fursa ya uhimilishaji kwani kwa kufanya hivyo kasi ya uzalishaji wa mifugo yenye ubora itaongezeka.



"Wafugaji mmeonyesha mfano mzuri kwa mamna mnavyozingatia kanuni za afya kwa kuwa, karibu kila kaya imeweka maji na sabuni kwa ajili ya kusafisha mikoni kwa kila mtu anayeingia na kutoka katika maboma yenu." Amesema Bi. Atupele



Pia Bi Atupele  amewaeleza kwamba Wizara ya Mifugo na Uvuvi inajali afya na suala zima la kujikinga na maambukizi ya virusi vya korona hivyo imetoa vitakasa mikono kwa kila kaya iliyoshiriki katika mafunzo.



Aidha Mfugaji wa  kijiji cha Nkerenge Wilaya ya Misenyi Mkoani Kagera ambaye pia amepata fursa ya kuhimilisha ng'ombe zaidi ya sitini  ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi na  Serikali kwa kuona umuhimu wa kupeleka huduma hiyo kijijini kwao na  kuiomba Wizara hiyo kuwasaidia kupata madawa na chanjo kwa wakati, kupatiwa elimu, wataalam wa malisho, na kuanzisha utaratibu wa kopa ng'ombe lipa  ng'ombe ambao utamsaidia Mfugaji kupata maziwa, kuuza na kuweza kuendesha maisha yake.

Mfugaji wa kijiji cha Nkerenge kata ya Mtukula Wilaya ya Misenyi Mkoani Kagera Bw. Majid Kayondo ambae pia alipata fursa ya kuhimilisha mifugo yake ameishukuru Wizara ya mifugo na Uvuvi na Serikali kwa ujumla kwa kuweza kuwafikia na kuwahamashisha juu ya ufugaji bora na wenye tija. Aidha ameiyomba serikali kuwajengea Barabara ya kuingia mnadani, kupatiwa madawa kwa wakati, kupatiwa elimu ya malisho na kurudisha utaratibu wa kopa ng'ombe lipa ng'ombe. (12/05/2020) 

Zoezi la Uhamasishaji na uelimishaji wa wafugaji ukiendelea kwenye boma la Bw. Majid Kayondo Kata ya Mtukula  kutoka kwa watafiti wa wizara ya mifugo na Uvuvi leo Mkoani Kagera. (12/05/2020) 




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni