Nav bar

Jumatano, 23 Oktoba 2019

WAFUGAJI KUNUFAIKA NA UWEKEZAJI MRADI WA KIWANDA CHA MBOLEA



Wafugaji nchini mbioni kunufaika baada ya wawekezaji kuja na nia ya kuwekeza kwenye mradi utakaohitaji malighafi kutoka kwenye mifugo zikiwemo kwato,pembe,kinyesi na manyoya ambazo zitakuwa zikinunuliwa kama malighafi nyingine ili kutumika kwenye kiwanda cha kutengenezea mbolea.

Lengo la serikali ni kuendelea kufungua milango kwa wawekezaji wote wenye nia ya kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo sekta ya mifugo nchini.Miradi kama hii itasaidia kuhamasisha wananchi kuendelea kufuga kwa wingi na kwa tija baada ya kuona fursa za uwekezaji zikiongezeka.

Hayo yamesemwa leo (24/9/2019), na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Profesa Elisante Ole Gabriel wakati akiwakaribisha wawekezaji wa kampuni ya ROKOSAN inayojihusisha na utengenezaji wa mbolea kwa kutumia malighafi zitokanazo na mifugo kutoka Jamhuri ya watu wa Slovakia kwenye makao makuu ya Wizara hiyo eneo la mtumba jijini Dodoma.

Alisema wawekezaji walio tayari kuwekeza wanakaribishwa na wizara inawaahidi ushirikiano wa hali ya juu kwenye sekta ya mifugo kwa ajili ya kuinua hali za wafugaji wetu hapa nchini, kuongeza ajira, pia kuongeza ukusanyaji wa kodi kupitia bidhaa mbalimbali zikiwemo zile zitokazo viwandani.

Katibu Mkuu alisema viongozi wa serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani Dkt.John Pombe Joseph Magufuli wanahitaji uwekezaji wenye matokeo ya haraka na yenye tija kwa taifa ndio maana wizara yake iko tayari kutoa ushirikiano pale mwekezaji anapoonyesha nia ya kuwekeza kwenye sekta ya mifugo nchini.

Aidha Katibu Mkuu aliwahakikishia kuwa Tanzania ni mahali salama na sahihi kwa uwekezaji huo kutokana na rasilimali kubwa ya mifugo iliyopo nchini ambapo idadi ya ng,ombe ni takribani milioni.32.2 mbuzi mil.20,kondoo 5.5, kuku mil.79.1 na punda zaidi ya laki 6.

Prof.Gabiel aliongeza kuwa uwekezaji huo nchini Tanzania utakuwa na manufaa sio kwa watanzania tu bali hata kwa wawekezaji wenyewe kwa kuwa soko la bidhaa la ndani ya nchi ni kubwa, Afrika ya Mashariki pia lipo,bila kusahau nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Akizungumzia mradi huo wa kiwanda cha kutengeneza mbolea kwa kutumia malighafi zitokanazo na mifugo zikiwemo kwato, pembe, manyoya na kinyesi,Prof.Gabiel alisema itakuwa ni faraja kwa wadau wa sekta kuona hakuna kinachotupwa kutoka kwenye mifugo bali kinaongezewa thamani na kuwa bidhaa.

Profesa Gabriel aliongeza kuwa hata kwenye Mpango Kabambe wa Kuendeleza Sekta ya Mifugo nchini (TLMP) umeelekeza jinsi mnyororo wa kuongeza thamani malighafi zitokanazo na mifugo zitakavyoleta tija kuelekea uchumi wa viwanda nchini.

Kwa upande.wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya ROKOSAN Dkt. Stefan Szoke alisema anashukuru kwa mwitikio wa serikali wa kuonyesha ushirikiano katika hatua za awali za uwekezaji wa mradi huo.

Dkt. Szoke alisema baada ya kufuatilia masuala ya uwekezaji waligundua kuwa Tanzania ni nchi yenye fursa kubwa za uwekezaji kutokana na rasilimali na mazingira mazuri yaliyopo katika sekta ya mifugo na kusisitiza kuwa nia yao ni kuanzisha miradi yenye manufaa kwa haraka mara baada ya kukamilisha taratibu husika.

Akitolea mfano nchi za Ulaya ambako pia wamewekeza miradi ya aina hiyo, Dkt.Szoke alisema licha ya wafugaji kunufaika kwa kuuza malighafi hizo zitokanazo na mifugo, wakulima nao wamekuwa wakinufaika kwa kupata mbolea yenye ubora na kwa gharama nafuu.

Akifafanua faida nyingine ya mradi huo alisema kuwa gharama za uzalishaji zikipungua hata bei ya mazao sokoni hupungua hivyo kumfanya mwananchi kumudu bei za bidhaa mbalimbali ziwemo za vyakula ambayo ni muhimu kwa afya zao.





Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akiwakaribisha na kuwaahidi ushirikiano wawekezaji wa kampuni ya ROKOSAN kutoka Jamhuri ya Watu wa Slovakia, waliofika wizarani kwa lengo la kuwasilisha mada ya uwekezaji wa mradi wa kiwanda cha kutengeneza mbolea kwa kutumia malighafi zitokanazo na mifugo  katika ukumbi wa Wizara Mtumba jijini Dodoma leo. (24/9/2019)


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ( Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel( wa kwanza kulia) akijadili jambo na wageni kutoka nchini slovakia mara baada ya kuwasilisha mada kuhusu nia yao ya kuwekeza kwenye mradi wa kutengeneza mbolea nchini Tanzania katika ukumbi wa Wizara Mtumba jijini Dodoma.(24/9/2019)


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa kwenye picha ya pamoja na wageni kutoka Jamhuri ya watu wa Slovakia, wawakilishi wa mradi huo nchini Tanzania pamoja na wawakikishi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mara baada ya kikao kifupi katika ukumbi wa Wizara Mtumba jijini Dodoma leo (24/9/2019).


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni