Nav bar

Jumanne, 2 Julai 2019

KATIBU MKUU UVUVI AFUNGA MAFUNZO YA UFUATILIAJI UBORA NA UNADHIFU WA MAJI




Katibu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah amewataka washiriki wa mafunzo ya siku sita ya uelewa wa ufuatiliaji wa ubora na unadhifu wa maji na mazingira kuzingatia mafunzo hayo ili yawe na tija katika ukanda wa Bahari ya Hindi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam (30.06.2019) wakati wa kufunga mafunzo hayo yaliyokuwa yakifanyika katika Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi nchini (TAFIRI) Dkt. Tamatamah amesema mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na Serikali ya Watu wa China kupitia Sino-Africa Joint Research Centre (SAJOREC) na East African Great Lakes Urban Ecology (EAGLU) kwa kushirikiana na TAFIRI yanalenga kuboresha sekta ya uvuvi nchini pamoja na nchi zinazonufaika na Bahari ya Hindi pamoja na maziwa yaliyopo nchini.

Kuhusu mafunzo hayo katibu mkuu huyo Dkt. Tamatamah amesema washiriki walipata mafunzo kupitia mihadhara iliyotolewa na wakufunzi wabobezi kutoka China na Tanzania pamoja na kukusanya takwimu kutoka mito iliyopo Mkoani Dar es Salaam na kuchakata takwimu hizo katika maabara ya TAFIRI.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu TAFIRI Dkt. Semvua Mzighani amesema kupitia mafunzo hayo Serikali ya Watu wa China, SAJOREC na EAGLU wametoa vifaa vya utafiti vyenye thamani ya Tshs Milioni 70 ambavyo vitatumika kwa tafiti za kuangalia ubora na unadhifu wa maji na mazingira kwa ujumla.

Aidha Dkt. Mzighani amesema mafunzo hayo yalishirikisha washiriki kutoka nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Ethiopia pia walikuwepo waendesha mafunzo hayo kutoka China.



Vifaa vyenye thamani ya Tshs Milioni 70 vilivyotolewa katika Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi nchini (TAFIRI) na Serikali ya Watu wa China kwa kushirikiana na Sino-Africa Joint Research Cente (SAJOREC) na East African Great Lakes Urban Ecology (EAGLU) wakati wa mafunzo ya ufuatiliaji ubora na unadhifu wa maji pamoja na mazingira yaliyofanyika TAFIRI kwa siku sita.




Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah wakati akifunga mafunzo ya siku sita ya ufuatiliaji ubora na unadhifu wa maji pamoja na mazingira yaliyofanyika katika Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi nchini (TAFIRI) ambapo pia aliwakabidhi pia washiriki vyeti vya ushiriki wa mafunzo hayo.






x

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni