Nav bar

Jumatano, 3 Aprili 2019

WAZIRI MPINA AZINDUA RASIMU YA SHERIA YA UVUVI NA YA UKUZAJI VIUMBE MAJI.SERIKALI imeamua kuifumua Sheria ya Uvuvi Namba 22 ya mwaka 2003 na Kanuni zake za mwaka 2009 ili kuondoa vikwazo vya kibiashara na uwekezaji katika sekta ya uvuvi ili kwenda na kasi ya mabadiliko ya Serikali ya awamu ya tano inayolenga kujenga Tanzania ya viwanda na kuwatetea, kuwalinda wanyonge.

Akizungumza katika uzinduzi zoezi la ukusanyaji maoni ya wadau kuhusu rasimu ya Sheria ya Uvuvi na Sheria ya Ukuzaji viumbe kwenye maji katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam jana Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ametaja sababu nyingine zilizosababisha kuwepo mabadiliko hayo.

Ni pamoja na kutoa ulinzi madhubuti wa rasilimali za uvuvi, kuongeza uzalishaji na kuwa na masoko ya uhakika sambamba na kudhibiti utoroshwaji na uingizaji holela wa mazao ya uvuvi nchini.

Aidha Waziri Mpina alisema sheria hiyo mpya inatakiwa iendane pia na mabadiliko na matumizi ya sayansi na teknolojia katika uvuvi na ukuzaji viumbe kwenye maji ili kwenda sambamba na mahitaji pamoja na kuwepo mwamko mkubwa wa ufugaji wa samaki kwenye maji uliojitokeza miongoni mwa wananchi.

Alisema pamoja na rasimu ya sheria hizo mbili pia Serikali iko kwenye hatua za mwisho za kufazifanyia marekebisho Sheria ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Namba 29 ya mwaka 1994 na Kanuni zake za mwaka 2009 na Sheria ya Bahari Kuu Cap 388 na Kanuni zake za mwaka 2007 na 2016.

Hivyo Waziri Mpina aliwasihi wananchi kutoa maoni yasiyofungamana na upande wowote na kuacha tabia ya kila mmoja kuvutia upande wake ili kuwezesha kutunga sheria madhubuti.

Aidha Waziri Mpina alieleza utajiri wa kipekee wa rasilimali za uvuvi hapa nchini ikiwemo kuwa na eneo kubwa la maji lenye kilomita za mraba 346,337 sawa na asilimia 36.7 ya eneo lote la nchi yetu, fukwe ndefu na za kuvutia, kuwepo kwa samaki na viumbe vingine ambavyo vimetoweka na vingine vikiwa kwenye tishio la kutoweka duniani.

Pia kuwepo kwa mito, mabwawa na maziwa yenye sifa za kipekee ikiwemo Ziwa Victoria ambalo ni la pili kwa ukubwa duniani na Ziwa Tanganyika ambalo ni la pili kwa kina duniani na la kwanza kwa ujazo wa maji duniani.

Hivyo alisisitiza kuwa wakati nchi inakwenda kutunga sheria hiyo mpya ya uvuvi ni muhimu kama Taifa kujiuliza maswali kadhaa ikiwemo matumizi sahihi ya rasilimali hizo.

“lazima tujiulize tunapata wapi uhalali wa kuagiza samaki kutoka nje ya nchi?, tujulieze kwa nini tumeshindwa kulihudumia soko la ndani na la nchi jirani, Afrika na dunia?, kwa nini tuzidiwe uzalishaji na mauzo na nchi ambazo tunazizidi kwa mbali kwa rasilimali?”alihoji Mpina, 

“Vilevile Kwanini tuwe na wavuvi masikini tena ambao hawana zana bora za uvuvi, kwanini biashara, uwekezaji na ujenzi wa viwanda ni wa kusuasua ? haya ndio maswali tunayopaswa kujiuza kama Taifa”alihoji Mpina.

Hivyo Waziri Mpina alisema kutokana na ugumu wa maswali hayo ndio maana wizara yake ikaamua ni bora kuifumua Sheria ya Uvuvi Namba 22 ya mwaka 2003 na Kanuni zake za mwaka 2009 ili kusaidia kupata majawabu ya namna gani kama taifa litatoka kwenye mkwamo huo.

Wakichangia rasimu hiyo iliyowahusisha wavuvi, wachakataji wa samaki, wauza zana za uvuvi, wafugaji wa samaki kwenye maji, wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halamshauri, wawakilishi wa vyuo vikuu na viongozi wa dini.

Wakizungumzia mapungufu ya sheria hiyo baadhi ya wadau wa wavuvi walisema sheria imekataza matumizi ya taa za sola, jenereta pamoja na utitiri wa leseni hali iliyochangia wavuvi wengi kushindwa kutekeleza kikamilifu majukumu yao.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mahmoud Mgimwa aliipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kubuni wazo hilo na kusisitiza kuwa wao kama Bunge wako tayari kushirikiana na Serikali katika kubadilisha sheria zote zinazokwamisha juhudi za kujenga Tanzania ya viwanda huku akisitiza wadau kutumia vizuri fursa hiyo na kwamba wasijitoe katika uandaaji wa sheria hizo mpya.

Katibu Mkuu Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Rashid Tamatama alisema atasimamia kikamilifu uratibu wa zoezi zima la ukusanyaji maoni ya wadau na kwamba timu ya wataalamu wa wizara hiyo itaenda kila mahali walipo wadau.

Aidha Dk Tamatamata alisema zoezi hilo kwa ukanda wa Ziwa Victoria lilizinduliwa na Waziri Mpina Januari 28 mwaka huu ambapo wadau walijitokeza kutoa maoni yao na kwamba zoezi hilo litaendelea hadi Februari 28 mwaka huu huku akisisitiza maoni yanakaribishwa kwa maandishi kupitia barua pepe ya maoni@uvuvi.go.tz 
Add caption

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni