Nav bar

Jumatano, 3 Aprili 2019

MPINA AZINDUA MKAKATI KUENDELEZA SEKTA YA MIFUGO.




WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, amezindua Mpango Kambambe wa Kuendeleza Sekta ya Mifugo nchini (Tanzania Livestock Master Plan-TLMP) huku akimtaka Katibu Mkuu Mifugo kuandaa mpango wa utekelezaji wa mkakati huo ndani ya siku 30 ili utekelezaji uanze mara moja. 

Akizindua mpango huo jijini Dar es Salaam, Waziri Mpina alisema, ni lazima mpango mkakati wa utekelezaji uwasilishwe ofisini kwake ndani ya kipindi hicho ili kuondoa dhana iliyojengeka ya mipango mingi kuandaliwa kwa muda mrefu na gharama kubwa, lakini usimamizi na utekelezaji wake kuwa dhaifu na kushindwa kuleta matokeo yaliyotarajiwa.

Alisema Tanzania ina mifugo mingi, ikiwa na asilimia 1.4 ya ng'ombe duniani na asilimia 11 ya ng'ombe Bara la Afrika wako Tanzania huku ikiwa ya pili barani Afrika baada ya Ethiopia.

Waziri Mpina alisema fursa na changamoto zimefanikisha kuandaliwa kwa mpango huo ili kuondoa vikwazo na kuweka mazingira wezeshi ya ufugaji, biashara na uwekezaji.

Alizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na ukosefu wa malisho na maji, wafugaji kufukuzwa kila mahali, ukosefu wa dawa na chanjo za mifugo, ongezeko la bidhaa za mazao ya mifugo kutoka nje ya nchi, uwekezaji wa kusuasua, ukosefu wa bei nzuri, soko la uhakika na mitaji na ukosefu wa mifugo iliyoboreshwa na huduma za utafiti.

Aliwataka wadau wa maendeleo waliofadhili mpango huo Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mifugo (ILRI) na Taasisi ya Bill & Melinda Gate Foundation, kutoishia kufadhili uandaaji wa mpango huo badala yake washiriki moja kwa moja kwenye utekelezaji wake.

Pia aliwataka watendaji wote wa Serikali Kuu, Serikali za Mitaa kujipanga na kushiriki katika utekelezaji wa mpango huo ili kuleta matokeo ya haraka.

Waziri Mpina pia aliitaka sekta binafsi, wafugaji, jumuiya za wafugaji, wafanyabiashara, wawekezaji, taasisi za fedha kila mmoja kwa nafasi yake ashiriki kutekeleza mpango huo.

Kufuatia mpango huo, serikali italazimika kufanya marekebisho ya sera na sheria pamoja na kuanzisha mikakati na miongozo mipya ili kufanikisha utekelezaji wa mpango huo kwa ufanisi mkubwa.

Naye Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alisema kuzinduliwa kwa mpango huo kumeiwezesha wizara yake kupanga matumizi bora ya ardhi ili kufanikisha utekelezaji wa mpango huo.

"Ardhi yangu haina maana kama haitumiki vizuri, mimi nafurahi sasa mmejipanga na mmetengeneza mpango mzuri ambao utasaidia hata kunipa kazi ya kupanga matumizi ya kufanikisha mpango wenu, nataka nikuhakikishie mheshimiwa Mpina tuko pamoja najua mahitaji yenu,” alisema Lukuvi.

Katibu Mkuu Mifugo, Profesa Elisante Ole Gabriel, alisema mpango huo ulianza kuandaliwa miaka mingi iliyopita, lakini sasa umekamilika na kuzinduliwa huku akimhakikishia Waziri Mpina kuwa atasimamia kikamilifu utekelezaji wake ili kuleta matokeo ya haraka yanayotakiwa na Watanzania.

Kwa upande wao mawaziri wastaafu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Titus Kamani na Dk. Charles Tizeba, walimpongeza Waziri Mpina kwa kufanikisha mpango na kukiri kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi sasa imejizatiti kusimamia sheria, hatua itakayoiwesha kupiga hatua kubwa ya maendeleo.

Wenyeviti wa CCM, mikoa ya Dar es Salaam na Pwani wamepongeza mpango huo na kusisitiza kuwa CCM kinathamini na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na waziri Mpina katika kuleta mageuzi ya kweli katika sekta ya mifugo nchini. 

Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania, George Bajuta alimshukuru Rais Dk. John Magufuli kwa jitihada anazofanya za kuwasaidia wafugaji nchini huku akimpongeza waziri Mpina kwa kuendelea kuwa kielelezo cha mageuzi katika sekta ya mifugo nchini.

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, akizindua Mpango Kambambe wa Kuendeleza Sekta ya Mifugo nchini (Tanzania Livestock Master Plan-TLMP)








Hakuna maoni:

Chapisha Maoni