Nav bar

Alhamisi, 4 Aprili 2019

WANANCHI WAONYWA KUTOTUMIA VIBAYA MATAMKO YA RAIS WA NCHI, KUKWEPA KODI



Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka wananchi hususan wafugaji kutotumia matamko ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli vibaya kwa kutafuta mianya ya kutolipa kodi.

Prof. Gabriel amebainisha hayo akiwa katika mnada wa upili wa Meserani uliopo wilaya ya Monduli Mkoani Arusha mara baada ya kufanya ziara ya kukagua utendaji kazi wa watumishi waliopo katika mnada huo na kusikiliza kero za wafugaji.

Akizungumza na wananchi mara baada ya kufanya ziara hiyo Prof. Gabriel amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kipindi cha mwezi mmoja itashirikiana na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli kutoa tafsiri sahihi ya mfanyabiashara mdogo anayestahili kukatiwa kitambulisho cha biashara ndogo ndogo (machinga) cha Shilingi Elfu Ishirini kwa mwaka, kilichotolewa na Rais Magufuli kutokana baadhi ya wafugaji kutaka kufahamu endapo wanastahili kupatiwa vitambulisho.

“Mheshimiwa rais alikuwa amelenga hasa wale wafanyabiashara wadogo wadogo na tunachoamini tutaendelea kulifanyia kazi lakini suala la machinga kwamba naye mfanyabiashara wa ng’ombe kuhusishwa katika sifa za mfanyabiashara ndogondogo bado ni gumu kulitolea majibu, lakini ushauri tusitumie matamko ya rais vibaya tusitafute kichaka cha kujificha kwamba nawe ni machinga, wewe mwenyewe fikiria na jitafakari tulipe kodi na tujenge nchi yetu.” Alisema Prof. Gabriel

Akizungumza na wafugaji hao Prof. Gabriel amepokea kilio cha wafugaji kuwa wamekuwa wakiuza ng’ombe kwa makadirio au matakwa ya mnunuzi kutokana na kutokuwepo kwa mizani ili waweze kuuza ng’ombe kwa kilo badala ya bei ya kukadiria kati ya mfugaji na mnunuzi wa ng’ombe, kitendo ambacho wafugaji hao wamesema kimekuwa kikiwafanya wasiuze mifugo yao kwa bei yenye tija kwao.

“Lengo letu ni kuhakikisha minada yote hasa ya upili na ile ya mipakani inatumia mizani, mnada wa Kimesera mzani wake uko tayari unatakiwa kufanyiwa marekebisho ili kuondokana na bei ya kukisia katika kipindi cha mwezi mmoja.” Alisema Prof. Gabriel

Aidha katibu mkuu huyo, amewataka wafugaji kufuga kisasa kwa kuhakikisha wanawapatia ng’ombe malisho bora ili wapate mazao bora ya mifugo yao huku Wizara ya Mifugo na Uvuvi ikihakikisha inaendelea kuimarisha matibabu ili mifugo iwe na afya bora.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema pia licha ya uwepo wa masoko ya mifugo hususan ng’ombe hapa nchini, wizara inajikita katika kutafuta masoko ya mifugo nje ya nchi.

“Tunachoangalia hivi sasa ni kuangalia na masoko ya nje ya nchi lakini hauwezi kuuza ng’ombe nje ya nchi ambaye hana afya bora na tunaamini tukiendelea hivi hata mchango wetu wa wizara kwenye uchumi wa viwanda utakuwa ni mzuri.” Alisema Prof. Gabriel

Naye Bw. Kandidi Mlinyi ambaye ni msimamizi wa mnada wa Meserani amesema kuwa wamekuwa wakikumbwa na changamoto ya upatikanaji wa maji katika ukanda wa Wilaya ya Monduli hivyo kuwa na mazingira magumu ya upatikanaji wa huduma hiyo mnadani.

Kauli hiyo imeungwa mkono na baadhi ya wafugaji ambao wamesema ng’ombe wanaposafirishwa kutoka maeneo mbalimbali kuja katika mnada huo, kwa wastani wanakunywa maji lita 20 hadi 60 lakini kutokana na ukosefu wa maji ng’ombe wanakuwa katika mazingira magumu hali inayosababisha ng’ombe hao kuchoka kwa kuwa wanapoteza maji mengi mwilini.

Katika ziara hiyo ya Katibu Mkuu Prof. Gabriel wafugaji wamepongeza utendaji kazi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuwa viongozi na watendaji wa wizara wamekuwa wakifika mara kwa mara kwa wananchi wakiwemo wafugaji ili kutatua kero zao.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika uongozi wa mnada wa Meserani kwa siku zaidi ya ng’ombe 500 huuzwa na kusafirishwa kwenda katika mikoa mbalimbali wakati wa msimu ambao unakuwa na ng’ombe wengi kuanzia mwezi Machi hadi Julai kila mwaka.



Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gariel akikagua ubora wa baadhi ya ng'ombe waliofikishwa katika mnada wa Meserani


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni