Nav bar

Jumanne, 5 Desemba 2017


WAZIRI MPINA AAGIZA MIKATABA YA VITALU VYA RANCHI YA TAIFA VYENYE JUMLA YA HEKTA Waziri MPINA 68238 KUVUNJWA MARA MOJA.
Waziri wa  Mifugo na Uvuvi Mh. Luhaga Mpina ameagiza Mtendaji Mkuu wa Ranchi za  Mifugo za Taifa, Profesa Philemoni Wambura kuvunja  mikataba ya wawekezaji wa vitalu vyenye jumla ya hekta 68,238 kwenye ranchi ya Mkata na Dakawa ndani ya mwezi  mmoja baada kushindwa kuviendeleza vitalu  vya ranchi na kushindwa kulipia kwa muda mrefu.

Mpina ameyasema hayo jana wakati alipotembelea katika ranchi ya Mkata na Dakawa kwa lengo la kukagua shughuli mbalimbali zinazofanyika  katika ranchi hizo.

Amezitaja kampuni za wawekezaji  ambazo zilizomilikishwa  vitalu zinatakiwa kuvunja mkataba kwa kushindwa kuendeleza upande wa ranchi ya Mkata katika Wilaya ya Kilosa kuwa ni pamoja na Kadolo Farm Company Ltd  kitalu namba 418 yenye hekta 4005,Bagamoyo Farm kitalu namba 419 yenye hekta 3672.96, A to Z Animal Feeds Company Ltd kitalu namba 420 yenye hekta 3692.97 na Ereto Livestock Keepers kitalu namba 422 yenye hekta 4020.54.

Katika Wilaya ya Mvomero kampuni zilizoshindwa  kuendeleza vitalu ni pamoja na kampuni ya  Overland kitalu namba 415 yenye hekta19446.28, Katenda yenye hekta 2500, Mollel yenye  hekta 2500 na Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa (Mtibwa Sugar) chenye hekta 20000 walizomilikishwa toka mwaka 1999 na kushindwa  kukiendeleza na kukilipia kwa miaka 18.

Mpina amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kilosa kumaliza  mara moja migogoro inayoendelea baina ya wakulima na wafugaji. Aidha Waziri Mpina amemtaka Diwani wa kata yaTwatwatwa, Katibu Tawala  wa Halimashauri ya Wilaya ya Kilosa pamoja na jamii ya wafugaji kumaliza migogoro inayowasumbua kwa muda mrefu kwa njia ya mazungumzo kabla ya kukimbilia muhimili wa mahakama bila sababu yoyote.

Mpina amesema kama  vyombo  vya Serikali vingetumika vizuri kuanzia ngazi ya kijiji kungepunguza  migogoro ya wakulima na wafugaji  katika wilaya  hiyo. Wilaya ya Kilosa ni miongoni mwa Wilaya zinaongoza kwa  kuwa na migogoro mingi baina ya wakulima na wafugaji hapa nchini.

Kwa upande  mwingine, Waziri Mpina amezitaka Halimashauri zote nchini kutotunga sheria kandamizi  dhidi ya wafugaji. Akitolea mfano, wa sheria ndogo ya Halimashauri ya Mvomero ya kutoza faini ya shilingi 25, 000/=kwa kila mfugo kuingia  katika Wilaya hiyo bila kufuata taratibu  badala ya shilingi elfu kumi iliyoelekezwa katika Sheria ya Magonjwa ya  Wanyama namba 17 ya Mwaka 2003.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT)  Magembe Makoye amesema upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya wafugaji kutasaidia kuondoa migogoro  baina ya pande hizo na kuendelezwa kwa ranchi hizo za taifa  kutawasaidia wafugaji kupata shamba darasa litakalo wasaidia kufuga kwa kisasa  na kupata mbegu bora  za mifugo.

Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mh. Luhaga Mpina (aliyejishika kiuno)  akiangalia kundi la Mbuzi wapatao 100 walioletwa katika ranchi ya Mkata.

Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mh. Luhaga Mpina akiwa kwenye picha pamoja  na Viongozi wa Wilaya ya Mvomero na Viongozi wa Chama cha Wafugaji Tanzania  alipotembelea ranchi ya Dakawa.

Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mh. Luhaga Mpina (mwenye Kofia) akimsikiliza Mkuu wa Wilaya  ya Mvomero, Muhamed Utaly  kulia  akitoa maelezo ya kuhusu eneo la hekta 20000 zilizoshindwa kuendelezwa na mwekezaji Mtibwa Sugar kwa lengo  la ufugaji. Kushoto ni Meneja Mkuu  wa Kampuni hiyo bwana Stan Rau



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni