Nav bar

Alhamisi, 7 Desemba 2017


MPINA ABARIKI NARCO KUVUNJA MKATABA WA MWEKEZAJI MZEMBE KATIKA RANCHI YA KAGOMA

Na John Mapepele

Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi  Luhaga Mpina  ameridhia  maamuzi ya Kampuni ya Ranchi za NARCO kuvunja mkataba baina ya mwekezaji Agri Vision Global Ltd katika  Ranchi ya Kagoma  mkoani Kagera na kuamuru aondoka mara moja baada ya mwekezaji huyo kushindwa kutekeleza mkataba huo katika kipindi cha miaka mitano.

Waziri Mpina ametoa maelekezo  hayo jana  alipotembelea Ranchi ya Kagoma kuangalia shughuli mbalimbali  katika Ranchi hiyo ambapo ametoa siku saba kwa mwekezaji huyo kuondoka katika eneo hilo na badala yake Serikali kupitia NARCO kuendelea kusimamia shughuli za mifugo katika Ranchi hiyo.

“Ninakuagiza  Mkuu wa Wilaya  kuanzia sasa  hakikisha unaimarisha ulinzi katika ranchi hii katika kipindi cha kukabidhi Ranchi baina ya Serikali na Mwekezaji  ili kusitokee hujuma zozote” alisisitiza Mpina

Alitaja baadhi ya mambo ambayo hayakutekelezwa na mwekezaji huyo kuwa ni pamoja na  kujenga  machinjio ya nyama,  kujenga kiwanda, kutoa gawio la shilingi bilioni tatu kila mwaka katika kipindi cha miaka mitano, kutoa shilingi 2672 kwa hekta moja kama tozo la ardhi na kushindwa kuendeleza miundombinu ya NARCO waliyoikuta wakati  wanaingia mikataba hiyo miaka mitano iliyopita.

Waziri Mpina  amemuagiza Meneja Mkuu wa NARCO, Profesa  Philemoni Wambura  kuhakikisha kwamba ndani ya siku saba anamleta Meneja katika Ranchi hiyo kwa ajili ya usimamizi wa shughuli za ranchi hiyo na kuhakikisha kuwa inafanya kazi zake kisasa.

Aidha Mpina ametoa siku saba  kwa   Uongozi wa NARCO kuhakikisha kuwa imefanya tathmini  ya hasara zilizosababishwa na mwekezaji huyo ili taratibu za kisheria zichukuliwe dhidi yake  ili aweze kuilipa Serikali ikiwa ni pamoja na shilingi bilioni kumi na tano kama  gawio la miaka mitano iliyokaa ambalo amesema halijawahi kulipwa hata shilingi moja.

“Sasa tumeamua kuchukua hatua na tutaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wawekezaji wasiowaaminifu wanaotaka kuihujumu serikali katika sekta hizi za mifugo na Uvuvi” alihoji Mpina

Alionya wawekezaji kuacha tabia ya kuidanganya serikali kwamba wanauwezo wa kuwekeza katika vitalu  ili wapewe lakini wanabadili matumizi baada ya kupewa. Aliongeza kwamba  Serikali imegundua  baadhi ya wawekezaji wanaopewa vitalu wanawakodisha wafugaji kutoka nchi jirani  na kujipatia faida wakati  Serikali haipati chochote.

Awali,  akipewa ripoti ya maendeleo ya mifugo na uvuvi na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kagera Deodatus Kinawiro mbaye ni Mkuu wa Wilaya ya Bukoba . alisema kutokana na oparesheni za uvuvi haramu zinazoendelea wilaya ya ngara imekamata tani 6 za samaki zilizokuwa zikipelekwa katika nchi ya burundi .
Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina  akipima urefu wa bwawa la maji ya kunyeshea mifugo katika Ranchi ya Kagoma Mkoani Bukoba ambapo aliamuru mwekezaji  Agri Vision Global Ltd katika  Ranchi ya Kagoma  Mkoani Kagera kuondoka mara moja baada ya mwekezaji huyo kushindwa kutekeleza mkataba huo katika kipindi cha miaka mitano.

Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi  Mhe. Luhaga Mpina (mwenye Kofia )akitoa maelezo  ya kwa mkuu wa Wilaya ya Richard Lugango kuboresha ulinzi katika Ranchi ya Kagoma baada ya kumuamuru mwekezaji  katika Ranchi hiyo kuondoka mara moja baada ya kushindwa kutekeleza mkataba baina yake ya Serikali.

Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi  Luhaga Mpina  akiwa na viongozi wa Mkoa wa Kagera wa Serikali mara baada ya kuwasili jana kukagua shughuli za mifugo katika Ranchi za Mifugo zilizopo Mkoani.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni