Nav bar

Ijumaa, 8 Septemba 2017

HOTUBA YA NANENANE ILIYOWASILISHWA NA MHE. WAZIRI WA KILIMO MIFUGO NA UVUVI DKT. CHARLES TIZEBA ILIYOFANYIKA LINDI 2017


Mhe. Dkt. Charles Tizeba

HOTUBA YA WAZIRI WA KILIMO MIFUGO NA UVUVI MHE, MHANDISI, DKT. CHARLES JOHN TIZEBA (MB) WAKATI WA KUMKARIBISHA MGENI RASMI KATIKA KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKUKUU YA WAKULIMA, NANE NANE KITAIFA, VIWANJA VYA NGONGO KATIKA MANISPAA YA LINDI TAREHE 8/8/2017



Mheshimiwa, Mgeni Rasmi, Makamu wa  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan

Waheshimiwa Mawaziri wa Tanzania Bara na Visiwani,

Makatibu Wakuu wa Tanzania Bara na Visiwani,

Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa ya Tanzania Bara,

Makatibu Tawala wa Mikoa,

Mhe. Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo Mifugo na Maji

Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,

Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya,

Waheshimiwa Mameya na Wenyeviti wa Halmashauri mliopo,

Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya, Miji na Majiji,

Wataalamu wa Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Ushirika,

Wanahabari wa Vyombo mbalimbali,

Wageni Waalikwa,

Mabibi na Mabwana,



Kwanza kabisa, naomba kuchukua fursa hii kukushukuru, Mhe. Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukubali kufika na kushirikiana na Wakulima, Wafugaji na Wavuvi katika kilele cha Maadhimisho ya Sherehe za Wakulima, Nane Nane, yanayohitimishwa leo, hapa katika Viwanja vya Ngongo katika Manispaa ya Lindi na kwenye Kanda nyengine.

Kufika kwako, kwa mara ya pili mfululizo kwenye maadhimisho yetu kunadhihirisha jinsi unavyotilia maanani umuhimu wa Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, hususan katika maendeleo ya ujenzi wa  uchumi wa viwanda. Napenda pia kwa niaba ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi, nikushukuru sana kwa jinsi ulivyotenga muda wako na kutembelea mabanda ili kuona hali halisi ya Maadhimisho pamoja na teknolojia za uzalishaji, na uongezaji thamani wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Kama ambavyo umeona na kusikiliza, waoneshaji na waandaji wa Maadhimisho haya, Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa muda mrefu zitaendelea kuwa muhimili na kichocheo katika kujenga uchumi wa viwanda ambao ndio kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Tano unayoiongoza. Naomba, nikuhakikishie kuwa, Mimi na Watumishi katika Wizara yangu, tumejipanga kuhakikisha kuwa, Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi inaendelea kukua sawa sawa na mahitaji ya Wananchi. Hilo linawezekana na tutaweza kuzalisha malighafi za kutosha za kuwezesha viwanda kuzalisha bidhaa mbalimbali, ambazo zitauzwa ndani na nje ya nchi kwa bei nzuri na ya ushindani. Hivyo ndivyo tutaweza kuongeza mchango wa Sekta hizi katika uchumi wa Taifa na pia katika kuondoa umaskini kwa Watanzania wengi.

Mheshimiwa Mgeni rasmi,

Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo, mabadiliko ya tabianchi, ambayo kwa kiasi kikubwa yanachangia kupungua kwa uzalishaji na tija ya mazao, uhaba wa malisho ya mifugo na rasilimali maji.  Tumejipanga kuendelea, kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, ikiwa ni pamoja na kuzalisha mbegu bora zinazovumilia ukame, magonjwa na kutoa mavuno mengi.

Napenda pia kutoa taarifa kuwa, Serikali yako kwa kushirikiana na Wabia wa Maendeleo, tumekamilisha Mpango wa Kilimo Kinachohimili Mabaliliko ya Tabianchi na Miongozi ya uzalishaji mazao, ufugaji na uvuvi. Muongozo wa kilimo umetolewa kulingana na Kanda za Kilimo za Kiteknolojia. Miongozo hiyo, imezinduliwa na kuanza kusambazwa kwa Maafisa Ugani wa Kilimo Mifugo na Uvuvi na kwa wananchi, kuanzia Mwezi, Mei na Juni, 2017.

Mikakati mingine, tunayoendelea nayo ni pamoja na kuhakikisha kuwa mbolea bora, inapatikana kwa wingi na kwa bei nafuu zaidi, sawasawa na agizo lako la kuwasaidia Wakulima, Wafugaji na Wavuvi kupunguza gharama za uzalishaji ili waweze kufaidika na matunda ya juhudi zao.  

Sambamba na hilo, tumepanga na tutahakikisha kuwa tunaendelea kuwaelimisha na kuwasaidia Wafugaji wa Tanzania, kufuga kitaalam zaidi ili kuepuka hali ya kuhamahama kwa ajili ya kutafuta malisho na maji.

Hilo, litatuwezesha kufuga kwa tija na pia kupunguza migogoro ya Wakulima na Wafugaji.

Napenda pia kukuhakikishia kuwa, tumedhamiria kuboresha zaidi Sekta ya Uvuvi ili kuongeza uzalishaji na tija, ikiwa ni pamoja na kuongeza mchango wake katika pato la Taifa. Hapa tutahamasisha watu wengi kufuga samaki katika mabwawa na vizimba ili tuweze kuzalisha samaki wengi zaidi sambamba na kuboresha zaidi uvuvi wenye tija na ambao ni endelevu. Niishukuru sana Ofisi yako Mhe. Makamu wa Rais kwa hatua inazozichukua kulinda mazingira ya nchi yetu, ikiwa ni pamoja na kurahisisha upatikanaji wa cheti ya kukidhi matakwa ya utunzaji mazingira.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Mipango tuliyojiwekea, tutaitekeleza kwa ufanisi zaidi kwa kuhimiza ushiriki wa Sekta Binafsi, kuwekeza zaidi katika Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa kuzingatia mnyororo wa thamani ili kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwa nchi yenye uchumi wa kati ifikapo au kabla ya mwaka 2025.  Hili linaendana na Kaulimbiu ya mwaka huu, inayosema;

Zalisha kwa Tija Mazao na Bidhaa za Kilimo Mifugo na Uvuvi ili kufikia uchumi wa kati

Kupitia Kaulimbiu hii tunahimiza, matumizi ya nyenzo sahihi kama matrekta, na mashine nyingine za uzalishaji na usindikaji, kuongeza uwekezaji katika viwanda vodogo,  vya kati na vikubwa,  sambamba na kuweka mazingira bora yanayovutia Sekta Binafsi kuwekeza katika Kilimo, Mifugo na Uvuvi kupitia mnyororo wa thamani. Katika Maadhimisho haya, Wakulima, Wafugaji, Wavuvi, Wanaushirika na Wadau wengine wamepata nafasi ya kujifunza na kubadilishana uzoefu ili hatmae Sekta hii iweze kuongeza uzalishaji na tija zaidi. 

Kwa kuongeza uzalishaji, tutajihakikishia ziada kubwa ya chakula na malighafi za kutosha katika viwanda vilivyopo na vinavyotarajia kuanzishwa. Kama ambavyo, tunafahamu kuwa upatikanaji wa masoko ya uhakika, utachochea zaidi uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, uhakika wa bei kwa mazao na bidhaa zinazozalishwa na Mkulima, Mfugaji na Mvuvi atakayewekeza zaidi katika uzalishaji.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Mwisho, napenda pia, kukupongeza, Mhe. Rais kwa jitihada unazozichukuwa, pamoja na Serikali unayoiongoza katika kudhibiti matumizi, kuongeza makusanyo, kuhamasisha ujenzi wa viwanda, kulinda maliasili zetu, hususan madini na rasilimali zingine ili Taifa letu, liweze kufaidika, kupitia rasilimali hizo. Kwa niaba ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi.

Aidha, napenda kutoa shukrani kwako, na kwa Mhe. Dkt John Pombe Joseph Magufuli kwa kukubali kuondoa na kupunguza baadhi ya tozo, ushuru na kodi ambazo zilikuwa kero kwa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.  Naomba nikuahidi kuwa, Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi, itaendelea kusimamia maagizo unayotoa ili kuleta faraja kubwa kwa Wakulima, Wafugaji na Wavuvi na kuhamasisha Sekta Binafsi kuongeza uwekezaji katika Sekta hizo.  

Baada ya kusema hayo, naomba sasa, nikukaribishe ili uongee na Watanzania kupitia hadhara hii.

Mheshimia Rais, Karibu sana!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni