Nav bar

Ijumaa, 2 Januari 2026

DKT. BASHIRU APIGA MARUFUKU VIWANDA KUVUA, KULANGUA SAMAKI KWA WAVUVI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amepiga marufuku viwanda vya kuchakata samaki nchini kuingiza mitumbwi yao majini kwa ajili ya kuvua au kununua samaki kwa wavuvi waliopo ziwani ambapo amesema kuwa hatua hiyo inavuruga soko, kuwafilisi na kuwafukarisha wavuvi. 

Balozi Dkt. Bashiru amesema hayo mara baada ya kutembelea na kukagua kiwanda cha kuchakata samaki cha Nile Perch kilichopo Muleba mkoani Kagera Desemba 29,2025 ambapo ameongeza kuwa kitendo hicho kimekuwa kikifanywa na viwanda vyote vya kuchakata samaki nchini hatua ambayo ameeleza kuwa inawachochea wavuvi hao kufanya uvuvi usiofuata sheria kutokana na kukosa ushindani wa haki na kuwa na mapato madogo.

“Hawa watu mnasababisha wanavua kwa mikopo wakati wana watu wanatakiwa kuwalipa mishahara kama nyinyi, wapo kwenye biashara kama nyinyi, wanakopa kama nyie” Ameongeza Balozi Dkt. Bashiru.

Aidha Balozi Dkt. Bashiru amesisitiza kuwa kwa sasa ametengeneza mitandao mbalimbali inayompatia taarifa mbalimbali kutoka kwa wananchi ambao wamechoshwa na vitendo visivyofaa kwenye Uvuvi hivyo ni lazima afanyie kazi taarifa hizo ili kuwafanya wananchi hao kuendelea kushirikiana na Serikali kutokomoza vitendo hivyo.

Marufuku hiyo iliyotolewa na Balozi Dkt. Bashiru inatokana na Kanuni ya 13 ya Sheria ya Uvuvi nchini inayomkataza mtu yoyote kuvua, kukusanya, kumiliki au kusafirisha au kujihusisha na mazao ya Uvuvi kwa lengo la kibiashara kama hatokuwa na leseni inayomruhusu kufanya hivyo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa akikagua vifungashio vinavyotumiwa na kiwanda cha kuchakata samaki cha Nile Perch kilichopo Muleba mkoani kagera alipofika hapo Desemba 29,2025.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa akiangalia namna mnofu wa samaki unavyopimwa wakati wa ziara yake kwenye kiwanda cha kuchakata samaki cha Nile Perch kilichopo Muleba mkoani Kagera Desemba 29,2025.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (wa pili kutoka kulia) akitoa maelekezo kwa kiwanda kutopokea samaki wazazi wakati wa Ziara yake kwenye kiwanda cha Nile Perch kilichopo Muleba mkoani Kagera Desemba 29,2025.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni