Na. Hamisi Hussein, Dodoma
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally, ameiagiza timu ya wataalam wanaotekeleza Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabia ya Nchi kuzingatia maeneo sita muhimu yatakayowezesha utekelezaji wenye tija na kwa wakati mradi huo nchini.
Mhe. Balozi Dkt. Bashiru ametoa maelekezo hayo leo, Desemba 16, 2025, katika Ukumbi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mtumba jijini Dodoma, wakati wa kikao cha kupitia mwenendo wa utekelezaji wa mradi huo, ambapo alisisitiza umuhimu wa kuzingatia upatikanaji wa mbegu bora za ng’ombe wa maziwa, upatikanaji wa maji katika maeneo yanayotekelezwa mradi, utambuzi sahihi wa wanufaika, upatikanaji wa malisho kwa wafugaji, pamoja na usimamizi na uratibu unaojumuisha wadau wote wa sekta ya mifugo.
" Mfanye uratibu kwa makini kupata mbegu za bora za ng'ombe wa maziwa, malisho na maji ili hii tasnia ilete tija" Alisema Mhe. Balozi Dkt. Bashiru.
Aliongeza kuwa wataalam wanaosimamia mradi huo kuzingatia matumizi sahihi ya teknolojia ya kisasa ili kuendana na kasi ya dunia katika kuongeza tija na thamani ya tasnia ya maziwa nchini.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng’wasi Kamani, alisema kuwa utekelezaji wa mradi huo unapaswa pia kuzingatia kuwahusisha wataalam ili kutathmini fursa za ufugaji wa mbuzi wa maziwa kwa wanawake na vijana, hatua itakayopanua wigo wa ajira na kuongeza mchango wa makundi hayo katika tasnia ya maziwa.
Awali, akitoa taarifa ya mradi huo, Mratibu wa Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabia ya Nchi, Dkt. Lazaro Kapella, alisema mradi unagharimu dola za Marekani milioni 229.982 na utatekelezwa kwa kipindi cha miaka kumi na kueleza kuwa takribani wananchi 700,000 wanatarajiwa kunufaika na mradi huo unaotekelezwa katika mikoa nane ya Tanzania Bara na mikoa mitano ya Zanzibar.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Stephen Michael, alibainisha kuwa ucheleweshaji wa utoaji wa fedha kutoka kwa baadhi ya wafadhili umeathiri utekelezaji wa baadhi ya shughuli za mradi kwa wakati uliopangwa.
Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabia ya Nchi unafadhiliwa na wadau mbalimbali wakiwemo IFAD, OPEC Fund, GCF, AFD, TADB, HI, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na wanufaika wa mradi.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni