Na. Stanley Brayton, MWUV
◾ Vifaranga 1,500 vya pandikizwa Viwanja vya Maonesho Nanenane Dodoma.
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeendelea kutoa Mafunzo ya Upandikizaji Vifaranga vya Samaki ili kuwafanya wadau wa Sekta hiyo kuwa na Ujuzi wa kutosha katika kufuga Samaki pamoja na kuwasaidia kuwapa mbinu bora na ya kisasa ya ufugaji Samaki ili kuweza kujipatia kipato na lishe.
Akizungumza katika zoezi hilo la Upandikizaji wa Vifaranga vya Samaki katika Viwanja vya Maonesho ya Nanenane ya Dkt. John Samwel Malecela, leo Oktoba 28, 2025 jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Nazael Madalla amesema lengo kubwa la kupandikiza Samaki katika Vizimba na Mabwawa yaliopo katika Viwanja vya Maonesho ya nanenane ni kuwawezesha wadau wa Sekta kupata Mafunzo ya teknolojia mpya ya ufugaji wa Samaki kwa njia ya Vizimba pamoja na Mabwawa.
"Wizara inaendelea kuhamisha, kuendeleza pamoja na kusimamia shughuli za Ukuzaji Viumbe Maji kwa kutoa Mafunzo mbalimbali ya Ufugaji wa Samaki kwa vitendo kupitia Vizimba na Mabwawa yaliopo Maeneo ya Maonesho ya Nanenane, hivyo ni vyema wadau Kutembelea Maeneo hayo ili kujifunza mbinu bora ya Ufugaji wa Samaki kwa njia hiyo" alisema Dkt. Madalla
Aidha, Dkt. Madalla amesema kuwa hii yote ni kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuwa Huduma za Ugani na kutoa elimu juu ya Ukuzaji Viumbe Maji ziendelee kufanyika ata baada ya kuisha kwa Maonesho ya Nanenane.
Vilevile, Dkt. Madalla ameweka wazi kuwa utekelezaji wa agizo hilo unaendelea kwa ukamilifu na ndio mana siku ya leo wameanza kwa kupandikiza Vifaranga vya Samaki 1,500 katika Mabwawa matatu na kizimba kimoja, na matarijo ya Wizara ni kuwa wadau wengi wa Sekta watapata elimu ya kutosha ya Ukuzaji Viumbe Maji kwa vitendo.
Pia, Dkt. Madalla amewaweka wazi swala la Ufugaji Samaki ni moja ya shughuli muhimu ya Uchumi wa Buluu ambao unaweza wanufaisha wafugaji kwa kuboresha maisha yao na maendeleo ya Taifa kiujumla.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni