Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kichaa cha Mbwa Duniani wataalam wa afya za wanyama na mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo(SUA) wameanza zoezi la uelimishaji juu ya kichaa cha mbwa kwa wananchi zoezi lililoenda sambamba na utoaji wa huduma za afya kwa mbwa na paka.
Zoezi hilo lilianza leo Septemba 26, 2025 katika maeneo shule na kaya mbalimbali zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara lilihusisha utoaji elimu kwa umma pamoja na huduma ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa, kuwatoa kizazi mbwa na paka jike, kuwahasi mbwa na paka dume pamoja na kuwapa dawa za minyoo ambapo huduma zote zimeitolewa bure bila malipo.
Aidha, wafugaji wa mbwa na paka wamepatiwa elimu na ushauri wa kitaalamu kuhusu namna bora ya kuwahudumia wanyama wao ili kuhakikisha afya zao zinakuwa salama na kujikinga na maambukizi ya magonjwa hatarishi.
Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kichaa cha Mbwa Kitaifa kitafanyika Septemba 29, 2025 Wilayani Kiteto Mkoani Manyara na kuongozwa na Kaulimbiu isemayo " Chukua Hatua Sasa; Mimi, Wewe na Jamii".





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni