Na. Stanley Brayton, WMUV
Moshi, Kilimanjaro
Julai 4, 2025
⬛ Mifugo 3,405,500 inatarajiwa kuchanjwa na kutambuliwa Mkoani hapo.
⬛ Wafugaji wahimizwa kujitokeza kwa wingi kuchanja Mifugo yao.
Wafugaji Mkoani Kilimanjaro wameipokea Kampeni ya Chanjo ya Mifugo Kitaifa kwa mikono miwili na kujitokeza kwa wingi katika kuchanja Mifugo yao ikiwa ni ishara ya kuitikia wito wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya kuwataka wafugaji kuchanja Mifugo yao ili kutokomeza Magonjwa ya Mifugo ambayo yamekuwa yakisababisha athari kwa Mifugo na kupunguza soko la mazao yatokanayo na Mifugo ndani na nje ya nchi.
Akizungumza katika zoezi la Uhamasishaji na Utoaji Chanjo za Mifugo leo Julai 4, 2025 Wilayani Moshi Mkoani Kilimanjaro katika Kijiji Cha Mawala, Kata ya Kahe, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, ambaye ndiye Mgeni Rasmi wa zoezi la Uhamasishaji na Utoaji wa Chanjo za Mifugo Mkoani humo na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Mhe. Godfrey Mnzava, amesema hadi sasa Halmashauri zimeshapokea chanjo zote za ng'ombe, mbuzi, Kondoo na kuku ambazo leo zitaanza kutumika Rasmi katika uchanjaji wa Mifugo hiyo, na Mifugo 3,405,500 ndio inayotarajiwa kuchanjwa na kutambuliwa Mkoani hapo ambapo ng'ombe ni 492,700, mbuzi na kondoo 1,212,800, na kuku 1,700,000.
“hivyo nawahimiza wafugaji kujitokeza kwa wingi ili kufanikisha zoezi hili ambalo lina lengo la kuhakikisha Mifugo inalindwa dhidi ya Magonjwa kwani chanjo ni uwekezaji na si gharama.” amesema Mhe. Mnzava
Aidha, Mhe. Mnzava amesema kuwa wafugaji wa Mkoa wa Kilimanjaro wameipokea Kampeni ya Chanjo za Mifugo Kitaifa kwani lengo lake ni zuri na limelenga Kuimarisha Sekta ya Mifugo ili kuiwezesha kuwa na tija, kuchangia Uchumi wa viwanda, kuimarisha Biashara ya Mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na kuwanufaisha wafugaji na wananchi kwa ujumla.
Mhe. Mnzava amesema zoezi la Utoaji Chanjo za Mifugo litaenda sambamba na zoezi la Utambuzi wa Mifugo, ambalo litaongeza chachu ya kufuga kisasa na kuboresha maisha ya wafugaji kupitia Masoko ya Mifugo na mazao yake.
Vilevile, Mhe. Mnzava amemshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuridhia na kuwezesha Vifaa kama vishikwambi vya kuhifadhia Taarifa za Mifugo na Mfugaji pamoja na chanjo ili kufanikisha zoezi hili.
Pia, Mhe. Mnzava ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Timu za Wataalamu wake kwa kusaidia na kushiriki katika zoezi la uchanjaji Mifugo ili kufanikisha zoezi hili muhimu.
Halikadhalika, Mhe. Mnzava amewataka Wataalamu wa Mifugo kuhakikisha elimu ya kutosha ya Chanjo inatolewa kwa wafugaji hususani umuhimu wake, na amewataka Viongozi wa Halmashauri kutoa ushirikiano na uhamasishaji wa kutosha ili kufanikisha zoezi hili kwa Mafanikio makubwa.
Naye, Kaimu Msajili wa Baraza la Veterinari Tanzania (VCT), Dkt. Obed Nyasebwa, amesema Mifugo inachangia kwa kiasi kidogo sana kwenye pato la taifa, na hii inatokana na magonjwa yanayoikabili Mifugo.
Dkt. Nyasebwa amesema kuwa hii ndio sababu iliyompelekea Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuridhia Serikali kutenga Bajeti kubwa kwa ajili ya Chanjo za Mifugo ambapo ametoa Ruzuku ya asilimia 100% kwa kuku, yaani kuku wanachanjwa Bure, na asilimia 50% kwa ng'ombe na mbuzi/Kondoo, Yani tshs. 500/= kwa ng'ombe na tshs. 300/= kwa mbuzi/Kondoo.
Dkt. Nyasebwa alibainisha kuwa katika Kampeni hii chanjo zitatolewa dhidi ya Magonjwa Matano ambayo ni pamoja na Homa ya Mapafu ya ng'ombe, Sotoka ya Mbuzi/Kondoo, Mdondo wa kuku, mafua ya kuku na ndui ya kuku; kwa muda wa miaka mitano mfululizo kutoka 2025 hadi 2029.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni