Na Chiku Makwai - WMUV SIMIYU
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa wafugaji wameonyesha nia kuupokea ufugaji wa kisasa ili kuongeza tija kwenye sekta ya mifugo nchini.
Mhe. Dkt. Kijaji amesema hayo leo (Juni 15, 2025) wakati wa Kongamano la Wafugaji Tanzania lililofanyika katika Viwanja vya Nanenane Nyakabindi vilivyopo Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu.
“Tupo tayari kubadilika na kuanza kufuga kisasa kwa kutumia njia za kisasa ili kufikia mageuzi makubwa ya serikali kwenye Sekta ya Mifugo nchini” amesema Mhe. Dkt. Kijaji
Aidha, amesema wizara imefanya mikutano na wafugaji wote nchini kwa kukutana na wawakilishi wao ili kujadili changamoto za sekta hiyo na kuzigeuza kuwa fursa ili kuiboresha Sekta ya Mifugo.
Pia, amesema kwa kutambua mchango mkubwa unaotokaana na sekta hiyo serikali itaendelea kushirikiana na wadau wake wote waliopo katika mnyororo mzima wa Sekta ya Mifugo ili kuipa thamani sekta hiyo.
Ametoa rai kwa wakazi wa Mkoa wa Simiyu kujumuika katika Uzinduzi wa Kaampeni ya Chanjo Kitaifa na Utambuzi wa Mifugo utakaofanyika kesho (Juni 16, 2025) katika Viwanja vya Nanenane Nyakabindi mkoani hapo ambapo Mgeni Rasmi ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni