Nav bar

Ijumaa, 9 Mei 2025

AZMA YA DKT. SAMIA KWENYE SEKTA ZA UZALISHAJI IMETIMIA-DKT KIJAJI

Na. Omary Mtamike

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa miaka minne ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imetekeleza kwa vitendo dhana ya kuboresha maisha ya Watanzania kupitia sekta za Uzalishaji.

Mhe. Dkt. Kijaji amesema hayo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Hosteli ya wasichana na kumbi mbili za mihadhara kwenye Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) kampasi ya Mpwapwa Mei 08, 2025 mkoani Dodoma ambapo mbali na kuupongeza uongozi wa Wilaya ya chuo hicho kwa kukamilisha ujenzi wa majengo hayo kwa viwango stahiki amefurahishwa na namna wanafunzi wa chuo hicho walivyoandaliwa kuwa wataalam wazuri wa sekta ya Mifugo.

“Ni wazi kabisa yale ambayo nimejifunza kwa wanafunzi wetu kuanzia kwenye shamba lao la ng’ombe, kitotoleshi cha kuku na hatimaye kwenye kuku wenyewe yametosha kuonesha kazi aliyoamua kuifanya Daktari Samia Suluhu Hassan kwenye upande wa sekta za uzalishaji tangu alipoingia madarakani miaka minne iliyopita ambapo aliamini mbali na kuwawezesha vijana kujiajiri,  sekta hizi zitasaidia kuinua uchumi wa wananchi wote hasa wale wa kipato cha chini” Amesema Mhe. Dkt. Kijaji.

Mhe. Dkt. Kijaji ameeleza kuwa mbali na ujenzi wa majengo hayo na ukarabati wa kampasi mbalimbali za Wakala hiyo zilizogharimu bil.1.9, Serikali imeendelea kujenga na kukarabati miundombinu mingine ya Wakala hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa shilingi milioni 168 za ukarabati wa mabweni mawili ya kampasi ya Temeke.

“Aidha kufuatia kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu hii tumeongeza kiwango cha udahili kutoka 3574 mwaka 2021 hadi wanafunzi 4921 mwaka huu na tayari  tumepata shilingi bil. 2.05 kwa ajili ya ujenzi wa kumbi 10 za mihadhara katika kampasi za Mabuki, Mpwapwa, Morogoro na Tengeru” Ameongeza Mhe. Dkt. Kijaji.

Mbali na Ujenzi wa Majengo ya Wakala hiyo yaliyozinduliwa leo ambao umegharimu takribani kiasi cha shilingi bil. 1.6, Wakala hiyo imeanza ujenzi wa Kampasi nyingine mkoani Songwe itakayogharimu shilingi bil. 1.2 hadi kukamilika kwake.

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) Dkt. Pius Mwambene (katikati) akimuonesha Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (kushoto) Maeneo zinakohudumia Kampasi mbalimbali za Wakala hiyo muda mfupi kabla hajazindua Hosteli ya Wasichana na kumbi mbili za mihadhara za Wakala hiyo Mei 08, 2025 Mpwapwa, Dodoma.

Mwanafunzi wa chuo cha Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) kampasi ya Mpwapwa Bi. Kisawa Msaye akimpa maelezo mafupi kuhusu ufugaji wa kuku Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (katikati) wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa Hosteli ya wasichana na kumbi mbili za mihadhara za Kampasi hiyo Mei 08, 2025 Mpwapwa, Dodoma. Wengine pichani ni Mtendaji Mkuu wa Wakala hiyo Dkt. Pius Mwambene (kulia), Watendaji na viongozi mbalimbali wa Wizara hiyo na Wilaya ya Mpwapwa.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (wa tatu kutoka kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa Wizara hiyo, Wanafunzi na Watendaji wa Wilaya ya Mpwapwa ndani ya moja ya kumbi mbili za mihadhara alizozindua kwenye Wakala ya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) kampasi ya Mpwapwa Mei 08, 2025, Dodoma.

Pichani ni jengo la hosteli ya Wasichana la “Dkt. Ashatu Kijaji” lililopo kwenye Wakala ya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) kampasi ya Mpwapwa ambalo limezinduliwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji Mei 08, 2025 Mpwapwa, Dodoma.

Pichani ni jengo lenye kumbi mbili za mihadhara lililopo kwenye Wakala ya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) kampasi ya Mpwapwa ambalo limezinduliwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji Mei 08, 2025 Mpwapwa, Dodoma.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni