Nav bar

Jumapili, 13 Aprili 2025

NDEGE NYUKI YAANZA RASMI KUWASAKA WAVUVI HARAMU ZIWA VICTORIA

Na Edward Kondela - WMUV, Mwanza

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mara ya kwanza imenunua na kuzindua matumizi ya ndege nyuki (drone) itakayofanya kazi ya kuimarisha usimamizi wa shughuli za uvuvi katika Ziwa Victoria.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ndege nyuki hiyo jijini Mwanza Aprili 13, 2025 kwa niaba ya Mgeni Rasmi Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe. Alexander Mnyeti amesema serikali imeamua kuchukua hatua madhubuti za kisasa kuhakikisha inadhibiti uvuvi haramu kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

Mhe. Mnyeti ameongeza kuwa katika awamu hii wizara imetumia kiasi cha Shilingi Milioni 259, kwa ajili ya ununuzi wa ndege nyuki, kutoa mafunzo kwa waendeshaji, kufunga vituo vya kudhibiti, kufanya usajili na kuanzisha mfumo wa kuhifadhi na kuchambua taarifa zinazopatikana kutoka kwenye ndege hiyo.

“Ndege nyuki hii ni kwa ajili ya kuimarisha usimamizi wa shughuli za uvuvi katika Ziwa Victoria. Ndege nyuki hii ina uwezo wa kukimbia kwa mwendo kasi wa Kilometa 108 kwa saa na uwezo wa kuchukua picha za matukio kutoka umbali mita 350 na kuruka mita 120 kutoka usawa wa bahari na kusafiri umbali wa Kilometa 400 na kuweza kukaa angani kwa muda wa saa mbili.” amesema Mhe. Mnyeti

Aidha, amesema mpango wa matumizi ya ndege nyuki hautaishia Ziwa Victoria pekee, bali kupeleka matumizi hayo katika Ziwa Tanganyika na Nyasa, pamoja na maeneo ya Pwani ya Bahari ya Hindi ili kuhakikisha kila pembe ya nchi inaonja matunda ya teknolojia ya kisasa katika usimamizi wa rasilimali.

Pia, amesema ndege nyuki hiyo ina uwezo wa kutoa taarifa kulingana na muda halisia na kwamba itasaidia kupunguza vitendo vya uvuvi haramu na gharama za uendeshaji wa doria ziwani pamoja na kutumika katika masuala ya utafutaji na uokoaji.

Amefafanua kuwa ndege nyuki hiyo ni kifaa cha kisasa kinachoruka angani bila rubani kwa lengo la kusaidia kuimarisha doria na usimamizi wa rasilimali za uvuvi na kuwa kifaa hicho ni mali ya serikali, wizara itaendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na taasisi zingine za serikali kuimarisha ulinzi na usalama kwenye Ziwa Victoria.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Edwin Mhede akizungumza katika hafla hiyo amesema uwepo wa ndege nyuki unaenda sambamba na takwa la kidunia la matumizi ya teknolojia rafiki za kimazingira.

Ameongeza kuwa katika mapambano ya uvuvi haramu serikali ililazimika kutumia boti na magari yanayotumia mafuta ya diesel ambayo yanaleta hewa ya ukaa kwa kiasi kikubwa ila kwa matumizi ya ndege nyuki, itakuwa ikienda eneo mahsusi ambalo kuna viashiria vya uvuvi haramu hivyo kupunguza matumizi ya boti na magari kwa ajili ya kuwasaka wavuvi haramu.

Kufuatia maelekezo ya Naibu Waziri Mhe. Mnyeti, katika kudhibiti uvuvi haramu Dkt. Mhede amebainisha kuwa atahakikisha anasimamia maelekezo hayo yakiwemo ya baadhi ya maafisa uvuvi kutuhumiwa kushiriki katika matukio ya uvuvi haramu.

Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi amesema mkoa huo unategemea sana Sekta ya Uvuvi katika kukuza uchumi, hivyo kuzinduliwa kwa ndege nyuki kwa matumizi ya kudhibiti upotevu wa rasilimali za uvuvi kutasaidia kuwabaini wahalifu na kukomesha uvuvi haramu.

Amesema kama mkoa wamekuwa wakihakikisha doria zinafanyaika  mara kwa mara ili kuhakikisha maeneo yote ya Ziwa Victoria katika Mkoa wa Mwanza yanakuwa salama dhidi ya uvuvi haramu.

Baadhi wakazi wa jiji la Mwanza waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa ndege nyuki kwa ajili ya kudhibiti uvuvi haramu, wamepongeza jitihada za serikali na kusema ni jambo la kipekee kuwa na kifaa hicho ambacho wameshuhudia namna kinavyofanya kazi kwa mara ya kwanza baada ya uzinduzi.

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeweka wazi kuwa katika Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2025/2026 itatenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa ndege nyuki zaidi ili kuongeza wigo wa kudhibiti uvuvi haramu katika maeneo mbalimbali nchini.



Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti akikata utepe kuashiria kuzindua rasmi matumizi ya ndege nyuki (drone) kwa ajili ya kudhibiti uvuvi haramu katika Ziwa Victoria. (April 13, 2025)

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti akizungumza wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa matumizi ya ndege nyuki (drone) kwa ajili ya kudhibiti uvuvi haramu katika Ziwa Victoria, ambapo ametaka ndege hiyo itumike ipasavyo kukabiliana na vitendo hivyo. Hafla hiyo fupi imefanyika jijini Mwanza April 13,2025.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Edwin Mhede akifafanua baadhi ya taarifa kuhusu Sekta ya Uvuvi wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa matumizi ya ndege nyuki (drone) kwa ajili ya kudhibiti uvuvi haramu katika Ziwa Victoria. (April 13, 2025)

Baadhi ya wakazi wa jiji la Mwanza wakiiangalia ndege nyuki (drone) maalum kwa ajili ya kudhibiti uvuvi haramu, baada ya kuzinduliwa rasmi matumizi yake, ikiwa inaanza kuruka kuelekea angani kwa ajili ya kupiga picha katika Ziwa Victoria. (April 13, 2025)

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti (katikati) akipata maelezo kutoka kwa marubani wanaorusha ndege nyuki (drone) kwa ajili ya kudhibiti uvuvi haramu katika Ziwa Victoria, namna ndege hiyo inavyofanya kazi ikiwa angani na kuifuatilia nyendo zake kupitia televisheni. Kushoto kwa Naibu Waziri Mhe. Mnyeti ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Edwin Mhede na anayemfuatia ni Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mhe. Amina Makilagi. (April 13, 2025)

Ndege nyuki (drone) yenye namba za usajili 5H-25038 kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), ambayo ni maalum kwa ajili ya kudhibiti uvuvi haramu ikiwa angani kwa mara ya kwanza baada ya kuzinduliwa rasmi matumizi yake na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti, katika hafla fupi iliyofanyika jijini Mwanza, ambapo ndege nyuki hiyo imegharimu zaidi ya Shilingi Milioni 259. Ndege hiyo imenunuliwa na serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi. (April 13, 2025)

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti akibonyeza kifaa maalum cha kuongozea ndege nyuki (drone) na kuiruhusu ndege hiyo kuruka baada ya kuizindua rasmi kwa ajili ya matumizi ya kudhibiti uvuvi haramu katika Ziwa Victoria. (April 13, 2025)

Muonekano wa ndege nyuki (drone) yenye namba za usajili 5H-25038 kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), ikiwa ardhini kabla ya kuruka. Ndege hiyo imenunuliwa na serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi. (April 13, 2025)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni