Nav bar

Jumanne, 23 Januari 2024

RAS MWANZA AIPONGEZA WIZARA KWA KUWA NA MKAKATI WENYE TIJA KWA KUWAJENGEA VIJANA KUJIAJIRI


Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuweka mkakati wenye tija kwa vijana kwa kuwajengea kuweza kujiajiri kwa kutoa mikopo isiyo na riba ya pembejeo za vizimba, chakula cha samaki na vifaranga vya samaki kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo TADB.

Balandya ameyasema hayo ofisini kwake mara baada ya kupokea ugeni  kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi ukiongozwa na Afisa Uvuvi Mkuu Bi. Mkomanile Mahundi na kusema ufugaji kwenye vizimba utasaidia sana katika uzalishaji wa samaki.

Katika mazungumzo pia alitoa ushauri mpango huo wa ufugaji kwa njia ya vizimba ufanyike kwa awamu kutokana na wingi wa vikundi husika kutoka mikoa ya kanda ya ziwa.

"Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Samia imedhamiria kuwainua kundi la vijana kimaendeleo, mpango huu wa ufugaji wa kisasa wa samaki wataalamu kutoka wizarani ukiwawekea mazingira mazuri ya kazi utazidi kuwa na tija kwao kiuchumi", amefafanua Mtendaji huyo wa Mkoa wakati wa mazungumzo hayo.

Ameiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuweka ushirikiano na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili kuhakikisha miradi hiyo inafanyiwa ufuatiliaji na kuwa endelevu na mwishowe inafikisha ndoto ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kuona inawakomboa kiuchumi Wananchi hususani Vijana na wakinamama.

Kwa upande wake Afisa Uvuvi Mkuu Bi. Mkomanile Mahundi amesema lengo la kuja Mwanza ni kuainisha wanufaika wa mikopo ya pembejeo za ufugaji Samaki kwa Vizimba na kuwawezesha kukidhi vigezo vya mkopo wenye  masharti nafu na kushauri pale zitakapo bainika changamoto ili zoezi hilo liwe limekamilika kabla ya Januari 29 2024.

"Tutapita maeneo yote Mikoa ya Kanda ya Ziwa ambayo mradi huu wa ufugaji wa samaki kisasa kwa njia ya vizimba unafanyika ili tujiridhishe kwa kila hatua kabla ya kuwakabidhi wahusika wote waliokidhi vigezo vya mradi huu",amesisitiza Bi.Mahundi

Mkoa wa Mwanza una jumla ya vikundi 79 wakiwemo watu binafsi 11, kampuni 6, vijana 13 na vikundi 49.


Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana akiongea jambo na wataalamu wa Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi mara baada ya kifika ofisini kwake kwa lengo la kujitambulisha kwa ajili ya zoezi la kuainisha wanufaika wa Mikopo ya pembejeo za ufugaji samaki kwa Vizimba katika Mkoa wa huo, Januari 11.2024, Afisa Uvuvi mkuu Bi. Mkomanile Mahundi (kushoto) na Afisa uvuvi Mkuu Bw. Fredrick Mussa (kulia). Wakimsikiliza katibu huyo, Mkoani Mwanza.

Afisa Uvuvi Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi,  Bw. Fredrick Mussa akitoa elimu na kuelezea faida ya kuomba mikopo ya pembejeo za vizimba kwa wanufaika (hawapo pichani) wa mkopo wa vizimba na pembejeo zake kwa vyama vya Ushirika, Vikundi na watu binafsi kwenye  Halmashauri ya Wilaya ya Nyamagana Mkoani  Mwanza, Januari 11.2024.

Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Bw. Balandya Elikana (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na maafisa Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Mkoa wa Mwanza mara baada ya kikao kifupi kilichofanyika ofisini kwake,  lengo likiwa ni pamoja na kueleza nia ya Wizara hiyo kwa kushirikiana  na benki ya maendeleo ya kilimo (TADB) ya kutoa mkopo wenye masharti  nafuu isiyo na riba kwa vikundi, vyama vya ushirika na watu binafsi ikijumuisha  Pembejeo za  vizimba, Chakula cha Samaki  Mkoani Mwanza Januari 11.2024.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni