Nav bar

Jumanne, 23 Januari 2024

MAJONGOO BAHARI, MWANI, KAA NI BIASHARA KUBWA”


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amewahimiza wananchi wanaoishi Mtwara na maeneo mengine ya ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi kuchangamkia fursa ya ufugaji  wa Majongoo Bahari, Kaa, Kambakochi pamoja na kufanya kilimo cha Mwani kwa sababu mazao hayo yanahitajika sana katika nchi za Asia hususan China.

Waziri Ulega ametoa rai hiyo wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji cha Ruvula kinachojengwa Msimbati, mkoani Mtwara Januari 14, 2024.

“Mahitahi ya Majongoo Bahari, Kaa, Mwani, Kambakochi na Mwatiko ni makubwa katika nchi za Asia hasa china, hivyo ni lazima tucheze na fursa tulizonazo ili tuweze kufanikiwa na ndio maana serikali inatoa elimu kuwawezesha wananchi hususan vijana na kinamama kufanya shughuli hizo ili wauze nje ya nchi wajipatie kipato”, alisema Ulega

Halikadhalika, aliwahimiza wananchi kujipanga vyema ikiwemo kuunda vikundi ili serikali iweze kuwatambua na kuwapatia mikopo ya vifaa vya kisasa kwa ajili ya kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa ufanisi mkubwa.

Aidha, Waziri Ulega alionesha kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho cha ukuzaji viumbe maji cha Ruvula huku akiamini kuwa kitakamilika kwa wakati ili kianze kufanya kazi.

Awali, Mhandisi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. George Kwandu alimweleza Waziri Ulega kuwa ujenzi wa kituo hicho umefikia asilimia 90 na kwamba mpaka itakapofika Januari 30, 2024 mradi huo utakuwa tayari umekamilika.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (katikati)akikagua maendeleo ya ujenzi wa kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji kinachojengwa Msimbati, Ruvula, mkoani Mtwara alipofanya ziara ya kukagua kituo hicho Januari 14, 2024. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Ahmed Abbas. Kulia ni Mhandisi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. George Kwandu.

Pichani ni muonekano wa jengo la kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji linalojengwa Msimbati, Ruvula, mkoani Mtwara alipofanya ziara ya kukagua kituo hicho Januari 14, 2024.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni