Nav bar

Ijumaa, 21 Julai 2023

WADAU WA MAENDELEO WAUNGA MKONO BBT

Taasisi ya Kimataifa ya Heifer imeendelea kuunga mkono jitihada za Serikali ya  Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha vitendea kazi vijana wanaofanya shughuli za unenepeshaji wa mifugo katika kituo cha Mabuki kilichopo Wilayani Misungwi, Mkoani Mwanza Julai 18, 2023.


Akiongea na vijana katika hafla fupi ya kupokea vitendea kazi hivyo ikiwemo Lori moja na pikipiki Nne, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega aliwashukuru Wadau hao wa Heifer huku akisema kitendo hicho ni uungaji mkono jitihada za Mhe Rais Samia za kuwawezesha vijana na kina mama kujiajiri na kukuza kipato chao kupitia programu ya BBT Mifugo na Uvuvi.


Alisema kuwa Dkt. Samia anataka kuifanya programu hiyo ya BBT  kuwa ya kielelezo ambapo vijana wengi waweze kujikomboa kwa kujiajiri kupitia shughuli za Kilimo, Mifugo na Uvuvi.


Aliongeza kwa kusema kuwa ni wakati sasa kwa vijana hao kuanza kufanya ubunifu wa kufanya biashara yao hiyo kidigitali kupitia mifumo ya biashara mtandao ili kupunguza kutegemea kuuza mifugo yao kupitia masoko ya kawaida.


Aidha, aliwataka vijana hao wanaopata mafunzo ya unenepeshaji wa mifugo katika kituo hicho cha mabuki kuwa mstari wa mbele katika kufanya mapinduzi ya uchumi kupitia ufugaji wa kisasa ili vijana wenzao wengine waweze kuona na kuamini kwamba inawezekana.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkaazi, Heifer International Tanzania,  Mark Tsoxo alisema wataendelea kufanya kazi na Serikali hasusan katika programu zinazohusu vijana ili kuunga mkono uwezeshaji wa vijana na kina mama kupitia programu ya BBT.


"Hivi sasa tuna  mpango wa kufikia vijana laki moja kupitia programu ya kopa ng'ombe lipa ng'ombe ambayo tunaamini itawezesha vijana wengi kujiajiri", alisema tsoso


Aliongeza kwa kusema kuwa wametoa vitendea kazi hivyo kufuatia ombi la Waziri Ulega ambapo aliwaomba kuona namna ya kuunga mkono programu hiyo ya kielelezo ya Dkt. Samia Suluhu Hassan.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni