Nav bar

Jumatano, 7 Desemba 2022

WADAU WA MIFUGO WATAKIWA KUIWEZESHA SERIKALI KUPATA MAPATO

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. Tixon Nzunda amewataka wadau wa sekta hiyo kuwa makini wakati wanatoa mapendekezo ya kupunguza au kufuta kodi na tozo kwa kuzingatia kuwa ndio chanzo kikuu cha mapato ya serikali katika kuleta maendeleo ya wananchi.


Katibu Mkuu Nzunda ameyasema hayo Novemba 29 mwaka huu wakati akifungua kikao cha wadau cha maboresho ya kodi na tozo za mifugo katika ukumbi wa NBC jijini Dodoma.


Amesema umakini usipotumika serikali itapoteza mapato yake na taifa litakosa fedha ya kutoa huduma muhimu kwa wananchi wake hivyo ni muhimu pia kukawa na utamaduni wa kutoa mapendekezo ya namna serikali itakavyoweza kupata vyanzo vipya vya mapato kutoka kwenye sekta yetu ya mifugo.


"Mwaka jana tuliwasilisha maombi ya kupunguza au kufutiwa kodi na tozo 45 kati ya hizo maombi 42 yalikubaliwa (asilimia 93.3) kwa kupunguzwa au kufutwa kabisa ambapo maombi hayo yatawasilishwa hapa ili kutoa fursa kwa wadau kuona mabadiliko yaliyofanyika" amesema Bw. Nzunda.


Amefafanua kuwa msamaha huo ni ushahidi tosha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imelenga kuinua sekta ya mifugo kwa kufuta au kupunguza tozo na kodi tulizowasilisha.


Amesema lengo la kikao hicho ni  kuwa na uelewa wa pamoja kwa kupitia maombi ya tozo na kodi mbalimbali zilizoombwa mwaka huu wa fedha unaoendelea, pia kujadili maombi mapya ambayo mwisho wa kuwasilisha ni Novemba 31 mwaka 2022.


Aidha katibu mkuu amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan  kwa kupunguza kodi na tozo zilizoombwa mwaka jana na kupelekea kuongeza biashara ya ndani na nje ya nchi kwenye Sekta ya mifugo.


Naye mdau wa Sekta ya Mifugo Bw. Jitu Viajial Son ameishukuru Wizara hiyo kwa kufanya kikao na wadau wake na kuweza kusikiliza changamoto mbalimbali na kuweka umoja kati yao.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. Tixon Nzunda akiongea wakati wa kikao cha wadau cha maboresho ya kodi na tozo kilichofanyika kwenye ukumbi wa NBC Jijini Dodoma Novemba 29, 2022.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Tixon Nzunda (aliyekaa katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau wa Sekta hiyo mara baada ya kikao kifupi cha kujadili maboresho ya kodi na tozo kilichofanyika kwenye ukumbi wa NBC Jijini Dodoma Novemba 29,2022.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni