Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayesimamia Sekta ya Mifugo kusitisha mkataba wa ujenzi wa Mnada wa Malampaka unaojengwa na Kampuni ya Kumuli Engineering and Liveline Technology.
Waziri
Ndaki ametoa agizo hilo leo (01.10.2022) baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi
wa mnada huo uliopo katika Kata ya Malampaka Wilayani ya Maswa Mkoani Simiyu ambapo
hakuridhishwa na kazi iliyofanywa na mkandarasi huyo.
Mkandarasi
huyo alipewa kazi ya ujenzi wa mnada huo Januari 25, 2022 na alitakiwa kumaliza
ujenzi Mei 23, 2022. Kutokana na kushindwa kumaliza kazi kwa muda aliongezewa
muda mpaka Agosti 8, 2022. Lakini mpaka Waziri Ndaki alipofika kukagua kazi
iliyofanyika ilikuwa ni asilimia 9.2.
Kutokana
na hali hiyo, Waziri Ndaki amemuagiza Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Mifugo
kusitisha mkataba wa ujenzi wa mnada na Kampuni ya Kumuli Engineering and
Liveline Technology. Pili alimuagiza Kamanda wa Polisi Wilaya ya Maswa
kumtafuta mmiliki wa kampuni hiyo ili arudi kulipa madeni ya wafanyakazi wake
pamoja na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Aidha,
amemuagiza Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Mifugo kuhakikisha anamtafuta
mkandarasi mwingine haraka ili ujenzi wa mnada huo uweze kukamilishwa na kuanza
kutumika. Lakini pia alisema kuwa kama hatua za kumpata mkandarasi mwingine
zitachukua mud ani vema ujenzi huo ukafanyika kwa kutumia wataalam wa ndani ili
mnada uanze kufanya kazi.
Naye
Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Aswege Kaminyoge amesema kuwa mkandarasi huyu
ameshapewa muda wa kutosha lakini bado kazi halakamilisha, lakini pia ameondoka
bila kuwalipa wafanyakazi pamoja na watoa huduma hivyo ni vyema akawalipa
wafanyakazi wake.
Akizungumza
kwa niaba ya wafanyakazi, Wambura Richard amesema kuwa jumla ya deni wanalodai
ni shilingi 9,544,300 hivyo ameiomba serikali kuwasaidia ili waweze kulipwa
fedha hizo.
Ujenzi
wa Mradi huo wa Mnada wa Malampaka unagharimu shilingi milioni 261 na
mkandarasi alikuwa ameshalipwa shilingi milioni 44 ambayo kazi yake ilitakiwa
ifikie asilimia 17 lakini licha ya kuchelewa bado kazi ipo asilimia 9.2.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (katikati) akikagua kazi ya ujenzi iliyofanyika kwenye mradi wa ujenzi wa mnada wa Malampaka uliopo Wilayani Maswa Mkoani Simiyu. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Aswege Kaminyoge na kulia ni Mkurugenzi wa idara ya Uzalishaji na Masoko, Bw. Stephen Michael. (01.10.2022)
Mkurugenzi
wa idara ya Uzalishaji na Masoko, Bw. Stephen Michael (kulia) akifafanua jambo
kuhusu mradi wa ujenzi wa mnada wa Malampaka uliopo Wilayani Maswa Mkoani
Simiyu kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki mara baada ya Waziri
Ndaki kukagua mradi huo ambapo aliagiza kusitishwa kwa mkataba wa ujenzi
kutokana na kutoridhishwa na kazi iliyofanyika kulingana na mkataba.
(01.10.2022)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni