Serikali imetenge fedha shilingi bilioni 50 kwa ajili ya kuanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ambayo itajengwa Wilayani Kilwa mkoani Lindi.
Hayo yamesemwa leo
(09.11.2021) na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayesimamia Sekta ya Uvuvi,
Dkt. Rashid Tamatamah wakati wa makabidhiano ya eneo hilo la mradi kwa Mshauri
Elekezi wa kampuni ya Sering kutoka nchini Italia, kwa ajili ya kukamilisha
kandarasi ya upembuzi yakinifu utaopelekea kujulikana kwa gharama za mradi huo
na kutangaza zabuni ya ujenzi wa bandari hiyo.
Dkt. Tamatamah amesema kuwa
ujenzi wa bandari ya uvuvi ni moja ya mkakati wa serikali katika kuhakikisha
inaendelea kukuza sekta ya uvuvi hasa katika kuhamasisha uwekezaji na hivyo
kuongeza mchango wa sekta ya uvuvi
katika pato la taifa.
“Ujenzi huu wa bandari ya
uvuvi unakwenda sambamba na ununuzi wa meli mbili (2) kubwa za uvuvi ambazo zitafanya uvuvi katika bahari kuu lakini serikali pia inalifufua Shirika la
Uvuvi (TAFICO) ambalo ndilo litakalokuwa likisisimamia meli hizo,” alisema Dkt.
Tamatamah
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilwa,
Mhe. Zainabu Kawawa amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa wataalam
watakaofika kwa ajili ya kukamilisha mradi huo na kuhakikisha wanaanza
kujipanga kutumia fursa zitakazojitokeza kutokana na uwepo wa mradi huo.
Akizungumza kwa niaba ya
wananchi wa Kilwa, Kaimu Shekh Mkuu wa Kilwa, Muhidini Matata ameishukuru
serikali kwa kuamua kujenga bandari ya uvuvi wilayani Kilwa kwa kuwa itawaletea
manufaa mengi kiuchumi. Lakini pia ameiomba serikali kuendelea kupeleka miradi
mbalimbali itakayowasaidia wananchi kunyanyuka kiuchumi.
Kwa upande wa Mshauri Elekezi Bw. GABRIEL anayeiwakilisha Kampuni Sering Ingegneria kutoka Italia,anasema wanafuraha kubwa kwa kupata nafasi ya kushiriki katika mradi huu muhimu kwa wakazi wa Kilwa na Tanzania kwa ujumla.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mhe. Zainabu Kawawa wakikata utepe kama ishara ya kukabidhi mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi kwa mshauri elekezi Kampuni ya Sering Ingegneria kutoka Italia kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu. (09.11.2021)
Baadhi ya viongozi na wataalam kutoka Wizarani, Mkoa na Wilaya ya Kilwa wakitembelea eneo la mradi wa ujenzi wa bandari ya Uvuvi. (09.11.2021)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni