Nav bar

Alhamisi, 30 Septemba 2021

MKANDARASI ATAKIWA KUFUATA TARATIBU NA KANUNI UJENZI WA MAJENGO YA MIHADHARA.

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA) Dkt. Pius Mwambene ametaka ujenzi wa vyumba viwili vya mihadhara katika chuo hicho Tawi la Tengeru Mkoani Arusha kujengwa kwa kufuata taratibu na kanuni za ujenzi.

Dkt. Mwambene amebainisha hayo katika ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo katika jengo la NBC jijini Dodoma, wakati wa utiaji saini wa ujenzi wa vyumba hivyo.

Alisema anatarajia kazi ya ujenzi itatekelezwa kwa kuzingatia viwango vya ubora na kukamilika kwa wakati uliopangwa.

Aliongeza kuwa mkataba unaonyesha muda wa ujenzi  uliopangwa ni miezi sita, ambapo ujenzi utaanza mwishoni mwa mwezi huu wa Septemba na kukamilika  mwishoni mwa mwezi wa Machi mwaka 2022.

Aidha Mtendaji huyo alisema kuwa gharama za ujenzi wa vyumba viwili vya mihadhara ni Shilingi Milioni 800 hadi utakapokamilika.

Awali akiongea baada ya zoezi la utiaji saini kukamilika Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Ugani na Mafunzo Dkt. Angelo Mwilawa ameitaka kampuni ya LI JUN Devolopment Co Ltd ya Moshi inayotekeleza ujenzi huo, kufuata taratibu zote zilizoainishwa kwenye mkataba ili kupata matokeo bora yenye tija.

Naye meneja wa kampuni hiyo Bw. Xu Geng Sheng amewahakikishia viongozi na wataalam wa wizara waliokuwepo kwenye tukio hilo kuwa utekelezaji wa ujenzi huo utazingatia weledi na taratibu zote zilizopo ili kupata matokeo yenye tija na hatimaye kutangaza vyema jina la kampuni.

Kwa wakati mwingine Mtendaji wa Mkuu wa LITA Dkt. Mwambene alisema vyumba hivi vinajengwa ili kupanua wigo wa udahili wa wanafunzi kukidhi uhitaji wa elimu kwa sasa hususan katika Sekta ya Mifugo.


Mwanasheria wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Sekta ya Mifugo, Bi. Mariam Mgendwa akitia Saini sehemu ya Mwanasheria kwenye Mkataba wa Ujenzi wa Mihadhara 2 katika Chuo cha Tengeru Arusha akishuhudiwa na Mwanasheria, Bi. Irene Likindo aliyesimama wa kwanza kulia na Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Ugani na Mafunzo, Dkt. Angelo Mwilawa (wa kwanza kushoto aliyesimama), zoezi limefanyika katika ofisi ndogo ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo kwenye jengo la NBC Dodoma. (29.09.2021)

 


Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Vyuo vya Mfunzo ya Mifugo Tanzania, Dkt. Pius Mwambene (kulia) na Meneja wa Kampuni ya Ujenzi ya LI JUN Development (ltd) ya Moshi, Bw.Xu Geng Sheng (kushoto) wakisaini mkataba wa Ujenzi wa vyumba 2 vya Mihadhara (Lecture Theatre) vyenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 240 kila kimoja katika Kampasi ya Tengeru, ambapo ujenzi huo utakamilika ifikapo machi, 2022 na utagharimu shilingi Milioni 809,806,552.37. Hafla hii imefanyika katika Ofisi ndogo ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo kwenye jengo la NBC Dodoma (29.09.2021)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni