Nav bar

Jumamosi, 24 Julai 2021

NDAKI AAGIZA ULINZI KUWEKWA KWENYE SHAMBA LA UZALISHAJI MIFUGO - MABUKI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki ameagiza eneo la shamba la uzalishaji mifugo lililopo wilayani Misungwi mkoani Mwanza kulindwa na Suma JKT, Polisi pamoja na kujengewa fensi (uzio) ili kuimarisha ulinzi na usalama wa eneo hilo.

 

Hii ni baada ya Waziri huyo kufanya ziara jana ya kutembelea shamba la Mabuki pamoja na taasisi zilizomo ndani yake ambapo alielezwa kuwepo kwa uchungaji haramu na uchomaji moto pamoja na tishio la usalama kwa wanafunzi na watumishi katika shamaba hilo.

 

Ndaki amesema,eneo hilo ni kubwa na lipo wazi kwa hali hiyo  siyo salama kila mtu anaweza kuingia na kufanya jambo lolote hivyo waangalie uwezekano wa kuweka fensi ili mtu atakaye bomoa na kuingia itakuwa rahisi kumdhibiti.

 

Amesema,eneo hilo linapaswa kulindwa na Suma JKT,hivyo alimuagiza Mkurugenzi wa Utafiti ,Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya  Mifugo na Uvuvi Dkt.Angello Mwilawa pamoja na uongozi wa kituo hicho kukaa pamoja na kuangalia ni walinzi wa ngapi wanahitajika kwa ajili ya ulinzi wa shamba hilo.

 

Pia amesema katika suala la kuwalipa Suma JKT ni lazima taasisi hizo na wizara kukaa Pamoja kuangalia namna ambayo watakuwa wanawalipa ili kusiwe na sababu yoyote itayositisha ulinzi huo pindi utakapoanza.

 

Aidha, katika kuimarisha zaidi ulinzi wa eneo hilo amemuomba Mkuu wa Wilaya ya Misungwi awapatie Askari Polisi ambao watakuwa wanafanya kazi kwa kushirikiana na SUMA JKT lengo likiwa ni kuhakikisha eneo hilo linakuwa salama.

 

"Hatuwezi kuangalia wanafunzi na watumishi wapo hatarini,halfu sisi tunanyoosha mikono na kusema Mungu tusaidie na vitendo vya waangalizi wa ng'ombe,wanafunzi na watumishi kupigwa siyo sawa hivyo,tutafute pesa popote fensi ijengwe kama mwanzo,eneo hili lilindwe na Suma JKT na Polisi ili wavamizi wajue kuwa linalindwa," amesema Ndaki.

 

Awali Kaimu Meneja wa Wakala wa Mafunzo ya Mifugo (LITA) kampasi ya Mabuki Joel Ngogo,akisoma taarifa kwa Waziri huyo, amesema Juni 9,2020 wanafunzi wao wakiwa shambani  kukata fito za kujengea uzio wa ng'ombe walivamiwa,walipigwa na jaribio la kutaka kubakwa  mwanafunzi mmoja  wa kike ambaye aliokolewa na watu waliopita eneo hilo.

 

Ngogo amesema, Aprili 23, mwaka huu matukio ya wanafunzi kuvamiwa na kupigwa kwa kombeo wakiwa eneo la kantini (mgahawa) wakipata chakula yalirudiwa na wavamizi wanaodhaniwa kutumwa na wafugaji ambao mifugo yao ilikamatwa na uongozi wa shamba hilo.

 

Amesema katika kutatua changamoto hiyo alimuomba Waziri kusaidia kuoata ulinzi thabiti kwa kutumia makampuni ya ulinzi kwa kushirikiana na jeshi la Polisi.

 

Kwa upande wake Meneja wa shamba la uzalishaji mifugo Mabuki Lini Andey Mwalla,amesema wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya uchungaji haramu wa mifugo ya wananchi kutoka sehemu mbalimbali.

 

Hali hiyo imekuwa ikivuruga malengo yaliyokusudiwa na serikali na kusababisha athari ikiwemo kueneza magonjwa ya virusi na yaenezwayo na kupe hivyo kusababisha vifo vingi vya mifugo vitokanavyo na magonjwa kama ndigana kali na mengineyo.

 

Pia amesema,suala la uchomaji moto hususani kipindi cha kiangazi kinachofanywa na watu ambao bado hawajawabaini kutokana na mbinu wanazotumia wahusika limekuwa likisababisha uharibifu wa mazingira na hivyo mifugo kukosa malisho.



Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akiwa amemshika nyati maji wakati alipotembelea  shamba la L.M.U. Mabuki lililopo wilayani Misungwi mkoani Mwanza kwa lengo la kuona maendeleo yake. (14.07.2021)


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Mhe. Veronica Kessy (wa nne kutoka kushoto), Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Huduma za Ugani, Dkt. Angello Mwilawa (wa tatu kutoka kulia) na watumishi wa Shamba la L.M.U, LITA na TALIRI wote wa Mabuki wilayani Misungwi mkoa wa Mwanza wakati alipowatembelea kukagua maendeleo ya taasisi hizo ambapo amewataka kuwa na mipango ya kuweza kujiendesha wenyewe kwa faida badala ya kutegemea ruzuku kutoka serikali kuu, pia ameagiza kuwepo na ulinzi wa SUMA JKT. (14.07.2021)


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na wanafunzi wa LITA Mabuki wakati alipowatembelea kwa lengo la kuona maendeleo yao ya kielimu ambapo amewataka wasome kwa bidii ili waje wajiajiri na sio kutegemea ajira kutoka serikalini. (14.07.2021)


 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni