Nav bar

Alhamisi, 24 Juni 2021

WANAWAKE WANAOJIHUSISHA NA UVUVI WATAKIWA KUWA WABUNIFU


Wanawake wanaojihusisha na  shughuli za uvuvi wametakiwa kuwa wabunifu ikiwa ni pamoja na kujengeana uwezo Ili kukuza biashara zao huku wakikumbushwa   kujilinda dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi.

Ushauri huo umetolewa (24.06.2021)  na Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mara, Bi. Neema Ibamba katika warsha ya siku tatu ya wadau hao Mjini Musoma Mkoani Mara.

Ibamba amesema kuwa  biashara yoyote inahitaji ubunifu  na kwamba wadau hao kutoka Mikoa ya Kanda ya ziwa lazima waende na wakati.

Aliongeza kuwa ubunifu unaotakiwa ni pamoja na kuwa na vifungashio vizuri  vya kisasa kwa ajili ya bidhaa zao pamoja na kuangalia fursa nyingine za masoko zinazowagusa.

Aidha katika kukuza kipato cha familia, Ibamba amewataka wanawake kuendelea kushirikiana na waume zao badala ya kuwadharau kutokana na kipato wanachopata.

"Biashara ama kupata kipato kisiwe kigezo cha kufanya dharau kwa wanaume wenu kwa kuwa mna pesa, hakikisheni kile mnachokipata mnakiweka mezani ili kiwasaidie," alisema Ibamba.

Aidha Ibamba amewataka wanawake hao kujua mbinu mbalimbali za kuweza kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi hususani katika mialo ya kuuzia samaki na  dagaa na kuwaasa kuendelea kushikamana kwa umoja wao Ili waweze kupiga hatua kwenye biashara zao kwa sasa na siku zijazo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji  wa Shirika la  Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo   (EMEDO), Bi.Editrudith Lukanga amesema kuwa ushirikiano ndiyo njia pekee ya kuwafikisha wanawake katika mafanikio.

Lukanga amewataka wanawake hao  kuendelea kushirikiana na waume zao Ili kulinda ndoa zao badala ya kuwa chanzo cha migogoro katika ndoa hizo.

Ameongeza kuwa shirika lao limekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha Umoja wa Wanawake wanaojihusisha na Uvuvi (TAWFA) unazidi kuimarika na kuhusisha kundi kubwa.

Kwa upande wake, Afisa Uvuvi Mwandamizi ambaye pia ni mratibu wa dawati la jinsia la Uvuvi la Wizara kutoka Wizara ya Mifugo na Uvivi, Bi. Upendo Hamidu  amesema kuwa Wizara hiyo itahakikisha inaweka mipango imara Ili kuwasaidia wanawake katika shughuli zao.

Warsha hiyo ya siku tatu imeandaliwa na  Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Shirika la EMEDO na kufanyika  mjini Musoma mkoani Mara.


Mgeni Rasmi ambaye pia ni Afisa Maendeleo ya jamii Mkoa wa Mara, Bi. Neema Ibamba akiongea na washiriki wa warsha ya wanawake wanaojihusisha na Uvuvi (TAWFA) Kanda ya ziwa (hawapo pichani) kwenye warsha hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa John Ludini Mwembeni Complex Musoma. 24/06/2021.

Mteknolojia wa samaki Mwandamizi,  Bw. Masui Munda akiwasihi washiriki wa washra ya wanawake wanaojihusisha na Uvuvi (TAWFA) Kanda ya ziwa  kushirikiana kwa kushikana mikono Ili kuweza kupata maendeleo  zaidi Mkoani Mara. (24/06/2021)

Afisa Uvuvi Mwandamizi na Mratibu wa dawati la jinsia la Uvuvi la WMUV, Bi. Upendo Hamidu (picha ya juu), Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo (EMEDO), Bi. Editrudith Lukanga (kushoto) na Mwenyekiti wa NTT, Mr. Yahya Mgawe wakiongea na washiriki wa warsha ya wanawake wanaojihusisha na Uvuvi (TAWFA) hawapo pichani wakati wa warsha hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa John Ludini Mwembeni Complex Musoma. (24/06/2021)

Mgeni rasmi ambaye pia ni Afisa Maendeleo ya jamii Mkoa wa Mara, Bi. Neema Ibamba (katikati waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa warsha mara baada ya warsha ya wanawake wanaojihusisha na Uvuvi (TAWFA) Kanda ya ziwa iliyofanyika kwenye ukumbi wa John Ludini Mwembeni Complex Musoma (24/06/2021.)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni