Nav bar

Alhamisi, 17 Juni 2021

TAASISI ZA BIMA NA ZA FEDHA ZATAKIWA KUWA MKOMBOZI WA WAFUGAJI NA WAVUVI

Taasisi za bima na za kifedha zimetakiwa kuwa mkombozi kwa wafugaji na wavuvi kwa kuhakikisha wanakuwa na uwezo wa kuwa na bima ya mifugo na samaki itakayowasaidia kuwa na ulinzi wa uwekezaji wao na kuweza kukopesheka.

 

Haya yamesemwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega leo Juni 17, 2021 wakati akifungua kikao cha Wadau wa Dawati la Sekta Binafsi ambalo lipo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye ukumbi mdogo wa wizara uliopo kwenye ofisi za NBC jijini Dodoma.

 

Ulega amesema kuwa wafugaji na wavuvi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya kutokopesheka kirahisi na taasisi za kifedha na hivyo kuwafanya washindwe kuitumia fursa ya mikopo ambayo ipo ili kukuza mitaji yao na hatimaye kuongeza mitaji na kipato pia.

 

“Kutokana na changamoto hii, wizara imeona ni vema kuwakutanisha wadau wanaohusika ili wote kwa pamoja tujadili tatizo nini na nini kifanyike ili tutakapotoka hapa tuwe na suluhisho ambalo litajibu tatizo la wafugaji na wakulima kuhusu bima na mikopo,” alisema Ulega.

 

 

Ulega amesema kuwa mifugo na samaki ni uwekezaji na ni bishara kubwa hivyo taasisi hizi za bima na fedha lazima ziwe na mtazamo huo na kwamba kufanya kazi na wafugaji na wavuvi kutawaletea tija na wao wenyewe.

 

Lengo la wizara ni kuhakikisha uwekezaji na biashara kwenye sekta za mifugo na uvuvi zinakua na mchango wake katika kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla kinaongezeka. Vilevile amezishauri taasisi za fedha kuangalia uwezekano wa kupunguza riba kwenye mikopo ili wafugaji na wavuvi waweze kukopesheka kirahisi.

 

Vilevile amesisitiza kwa wataalam na wadau walioshiriki kikao hicho kuendelea kutoa elimu kwa wafugaji na wavuvi ili watambue kuwa mifugo na samaki walionao ni uwekezaji. Pia amesema biashara na uwekezaji ukishamiri na kukiwa na mazingira mazuri kila mtu atataka kuwekeza na kufanya biashara ya mifugo na samaki pamoja na mazao yake.

 

Naye Kaimu Katibu Mkuu anayeshughulikia sekta ya mifugo, Dkt. Bedan Masuruli amesema kuwa sekta za mifugo na uvuvi zinahitaji kuendelezwa na moja kitu kinachotakiwa ni mitaji hivyo kupitia kikao hicho anaamini kuwa tatizo la upatikikanaji mitaji litapatiwa majibu.

 

Mratibu wa Dawati la Sekta Binafsi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Stephen Michael amesema dawati lilifuatilia upatikanaji wa bima kwa wafugaji ili kuweza kuwasaidia wafugaji na wavuvi kupata mikopo. Shirika la Bima la Taifa (NIC), limetoa bima kwa vyama vya ushirika vya wafugaji vitatu na vyama vya ushirika vya wavuvi vitatu.

 

Kaimu Mkurugenzi wa Mipango, Utafiti, na Maendeleo ya Masoko ya Bima Tanzania, Bw. Muyengi Zakaria amesema kuwa wameshazielekeza kampuni zote za bima nchini waandae bidhaa ambazo zinakidhi mahitaji ya wafugaji na wavuvi. Lakini pia ni lazima kuwepo na muongozo ambao utawasaidia wafugaji na wavuvi kuhakikisha wanakata bima itakayowasaidia wakati wanapopatwa na majanga.

 

Kikao hicho cha wadau kilihudhuriwa na wawakilishi wa taasisi na kampuni za bima, taasisi za kifedha, wawakilishi wa vyama vya ushirika vya wafugaji na wavuvi pamoja na viongozi na wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akifungua kikao cha wadau wa bima kwa ajili ya mifugo na uvuvi (hawapo pichani) ambapo amezisisitiza kampuni za bima na taasisi za kifedha kuwasaidia wafugaji na wavuvi. Kikao hicho kimefanyika kwenye ukumbi mdogo wa wizara ulipo kwenye jengo la NBC jijini Dodoma. 17.06.2021)


Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Bedan Masuruli akizungumza wakati wa kikao cha wadau wa bima kwa ajili ya mifugo na uvuvi kilichofanyika kwenye ukumbi mdogo wa wizara ulipo kwenye jengo la NBC jijini Dodoma. Kushoto ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega. (17.06.2021)


Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Masiko na Mratibu wa Dawati la Sekta Binafsi, Bw. Stephen Michael akielezea kazi inayofanywa na dawati wakati wa kikao cha wadau wa bima kwa ajili ya mifugo na uvuvi kilichofanyika kwenye ukumbi mdogo wa wizara ulipo kwenye jengo la NBC jijini Dodoma. (17.06.2021)

Baadhi ya washiriki wa kikao cha wadau wa bima kwa ajili ya mifugo na uvuvi wakifatilia hotuba ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (hayupo pichani) kilichofanyika kwenye ukumbi mdogo wa wizara ulipo kwenye jengo la NBC jijini Dodoma. (17.06.2021)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni