Nav bar

Alhamisi, 15 Aprili 2021

WIZARA YA MIFUGO YATAKA KUWEPO NA ADHABU KWA WATAFITI WATAKAOSHINDWA KUFIKISHA MATOKEO YA TAFITI ZAO KWA WAFUGAJI

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imewataka watendaji wa wizara hiyo ambao wanahusika na utungaji wa miongozo ya utafiti wa mifugo kuangalia namna ya kuweka adhabu kwa watafiti watakaoenda kinyume kwa kutofikisha tafiti zao kwa wafugaji ambao ndio walengwa wa utafiti.

 

Agizo hilo lilitolewa Aprili 14, 2020  na Kaimu Katibu Mkuu wa  Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Bedan Masuruli wakati akizungumza na wadau wa sekta hiyo waliokutana jijini Dodoma kwa ajili ya kujadili miongozo ya tafiti za mifugo iliyotolewa na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI).

 

Alisema Wizara inatambua ugumu uliopo katika kuweka adhabu kwa watafiti watakaoshindwa kufikisha tafiti zao kwa ajili ya wafugaji lakini kitendo cha kutunga miongozo hiyo bila ya kuwa na sheria za kuwabana kutasababisha kuchelewa kufikia malengo waliyojiwekea.

 

"Nataka nisisitize kwamba miongozo hii tunayoijadili hapa mkaangalie namna ya kuweka na adhabu, japo naambiwa na wanasheria kwamba haiwezekani lakini hatuwezi kuacha hivi kwa sababu tutachukua hatua gani kama mtu hakufikisha matokeo ya utafiti kwa wafugaji au hata mtu akiamua kutoa majibu ya uongo, ni muhimu iwepo ili tufikie lengo letu la mwaka 2025" alisema Dkt Masuruli

 

 Aidha, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Dkt. Jonas Kizima alisema tayari sheria na kanuni za kuhakikisha tafiti zinazofanyika zinatoka kabatini na kuwafikia wafugaji na kwamba kinachofanyika sasa ni taasisi hiyo kufuatilia kila hatua ili watafiti wazifikishe tafiti hizo kwa walengwa waliokusudiwa.

 

Alisema pamoja na mambo mengine taasisi hiyo itahakikisha inashughulikia changamoto zote ikiwemo kuondoa vikwanzo mbalimbali na kuweka mifumo rafiki ili kusaidia kuharakisha tafiti zinazofanyika.

 

Naye mwakilishi kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Paulo Ochanga aliwataka wadau na watafiti kuendelea kutilia mkazo tafiti zinazofanyika ili kukuza sekta ya mifugo nchini ambayo inachangia pato la taifa kwa zaidi ya asilimia 7 kwa sababu ya mazao ya mifugo kuwa na thamani kubwa katika mnyororo wa thamani.

Kaimu Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Mifugo, Dkt. Bedan Masuruli (aliyekaa katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau wa Mifugo mara baada ya kikao cha kujadili miongozo ya utekelezaji wa kanuni za utafiti wa Mifugo kilichofanyika kwenye ukumbi wa Benjamin Mkapa Jijini Dodoma. (14.04.2021)
Kaimu Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Mifugo, Dkt. Bedan Masuruli akiongea na wadau wa Mifugo (hawapo pichani) wakati wa kikao cha kujadili miongozo ya utekelezaji wa kanuni za utafiti wa Mifugo kilichofanyika kwenye ukumbi wa Benjamin Mkapa Jijini Dodoma. (14.04.2021)

Kaimu Mkurugenzi Mkuu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Dkt. Jonas Kizima akifafanua jambo wakati wa kikao cha kujadili miongozo ya utekelezaji wa kanuni za utafiti wa Mifugo kilichofanyika kwenye ukumbi wa Benjamin Mkapa Jijini Dodoma. (14.04.2021)

Mwakilishi kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Paulo Ochanga akichangia hoja kwenye kikao cha wadau cha kujadili miongozo ya utekelezaji wa kanuni za utafiti wa Mifugo kwenye ukumbi wa Benjamin Mkapa Jijini Dodoma. (14.04.2021)


Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka WMUV, Dkt. Hassan Mruttu akifunga kikao kilichojadili miongozo ya utekelezaji wa kanuni za utafiti wa Mifugo kilichofanyika leo kwenye ukumbi wa Benjamin Mkapa Jijini Dodoma ambapo aliwashukuru wadau walioudhuria na kutoa maomi yao. (14.04.2021)





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni