Nav bar

Jumapili, 25 Aprili 2021

SERIKALI KUJA NA MKAKATI ENDELEVU KUDHIBITI UVUVI HARAMU

Na Mbaraka Kambona, Kigoma

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ipo katika mpango wa kuwa na mkakati endelevu wa kudhibiti uvuvi haramu na kuachana na utaratibu wa kuendesha oparesheni za muda mfupi.

 

Ndaki alisema hayo wakati akiongea na Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Mwalo wa Kibirizi ulipo katika Ziwa Tanganyika Mkoani Kigoma Aprili 24, 2021.

 

Akiongea na wavuvi hao Ndaki alisema kuwa lengo la Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni kuwa na udhibiti wa uvuvi haramu ambao utakuwa endelevu utakaoshirikisha wahusika wenyewe wanaofanya shughuli za uvuvi na viongozi wa eneo husika kuanzia ngazi ya Kijiji, Kata, Wilaya hadi Mkoa.

 

“Tunataka kuja na mkakati endelevu wa namna ya kudhibiti uvuvi haramu, tuusike sote, kuanzia Wataalamu, Viongozi wa ngazi zote na wananchi wanaohusika na uvuvi wenyewe,” alisema Ndaki huku akiongeza kuwa

 

“Uvuvi haramu unatishia rasilimali zetu za uvuvi, tusiulee, tuwashirikishe wahusika ili waone kuwa uvuvi haramu ni kitu kisichokubalika”.

 

Kwa Mujibu wa Ndaki anasema walichokigundua katika mkakati wa kutumia oparesheni za muda mfupi ni kwamba matokea yanakuwa ya muda mfupi na operesheni hizo zikiisha matukio ya uvuvi haramu yanaendelea tena kwa sababu operesheni hizo zinahusisha wataalamu kutoka Wizarani na sio wahusika wenyewe wa eneo husika.

 

‘‘Ulinzi wa rasilimali za uvuvi sio jukumu la watu wa makao makuu peke yake, ni jukumu letu sote, tuone umuhimu wa kutunza rasilimali zetu na wote tukubaliane kuwa uvuvi haramu haukubaliki na tukikukamata sheria itachukua mkondo wake,” alisisitiza Ndaki

 

Kuhusu baadhi ya viongozi wanaolalamikiwa kuhusika na vitendo vya uvuvi haramu alisema kuwa kiongozi au mtaalamu yeyote mwenye dhamana ya masuala ya uvuvi atakayepatikana kuhusika na vitendo vya uvuvi haramu na yeye atakuwa haramu na atashughulikiwa kama wahalifu wengine.

 

Aliongeza kuwa kiongozi yeyote aliyepewa dhamana ya kusimamia masuala ya uvuvi na eneo lake linafanya uvuvi haramu, wataanza kumchukulia hatua huyo kiongozi na wengine wote watakaokuwa wanahusika kwa namna moja au nyingine kwa kutokuwajibika kwao.

 

Ndaki alisema kuwa hatalegeza nati hasa linapokuja suala la uvuvi haramu na kuwataka wananchi na viongozi wa ngazi zote kushirikiana kwa pamoja kupiga vita uvuvi haramu huku akiwahimiza kuwafichua wale wote wanaohusika na vitendo vya uvuvi haramu katika maeneo yao.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki akiongea na Wavuvi wa Mwalo wa Kibirizi ambapo alisema kuwa Serikali ipo katika mipango ya kuandaa mkakati shirikishi na endelevu wa kupambana na uvuvi haramu nchini. Ndaki alifanya Mkutano na Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Mwalo wa Kibirizi uliopo Mkoani  Kigoma. (24.04.2021)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (kushoto) akijadiliana jambo na Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (kulia) Katika Mkutano wa Waziri huyo na Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Mwalo wa Kibirizi uliofanyika Mkoani Kigoma. (24.04.2021)


Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akisisitiza jambo wakati akitoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja zilizoibuliwa na Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Mwalo wa Kibirizi katika Mkutano wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi na Wavuvi hao uliofanyika Mkoani Kigoma. (24.04.2021)


Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi, Magese Bulayi akiongea na Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Mwalo wa Kibirizi wakati alipokuwa akijibu baadhi ya Maswali yaliyoulizwa na wavuvi hao katika Mkutano wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi na Wavuvi uliofanyika Mkoani Kigoma. (24.04.2021)


Mstahiki Meya, Manispaa ya Kigoma Mjini, Baraka Lupoli akiongea na Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Mwalo wa Kibirizi wakati wa Mkutano wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi na Wavuvi hao uliofanyika Mkoani Kigoma. (24.04.2021)


Sehemu ya Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Mwalo wa Kibirizi wakifuatilia matukio yanayoendelea  katika Mkutano wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki na Wavuvi hao uliofanyika Mkoani Kigoma. (24.04.2021)


Mbunge wa Kigoma Mjini, Kilumbe Ng'enda akiongea na Wavuvi wa Mwalo wa Kibirizi katika Mkutano wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki na Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Mwalo wa Kibirizi uliofanyika Mkoani Kigoma. (24.04.2021)


Baadhi ya Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Mwalo wa Kibirizi waliojitokeza kumsikiliza Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (hayupo pichani) katika Mkutano baina ya Waziri huyo na Wavuvi wa Mwalo wa Kibirizi uliofanyika leo Mkoani Kigoma. (24.04.2021)


Mchakataji Mazao ya Uvuvi, Prisca Steven akitoa kero zinazowashumbua Wachakataji wa Mazao ya Uvuvi kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (wa kwanza kushoto) katika mkutano wa waziri huyo na Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika mwalo wa Kibirizi uliofanyika Mkoani Kigoma. (24.04.2021)





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni