Nav bar

Jumapili, 7 Machi 2021

WANANCHI WAMETAKIWA KUSHIRIKIANA KATIKA SUALA LA KUDHIBITI UVUVI HARAMU

 Na Elibariki Mafole, MWANZA


WANANCHI wametakiwa kushirikiana katika suala la kudhibiti uvuvi haramu Ziwa Victoria ili kuendelea kunufaika na rasilimali za uvuvi.


Hayo yalisemwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki, katika kikao cha wadau wa Uvuvi kanda ya Ziwa kilichojadili kuhusu  ulinzi na usimamizi wa rasilimali za Uvuvi na kusema suala la udhibiti wa uvuvi haramu katika mwambao huo ni la kila mmoja.


Mashimba alisema suala la ulinzi wa rasilimali zilizopo ziwani ni jukumu la kila mmoja katika ngazi zote kuanzia kitongoji mpaka  wilaya hadi wizarani na si jukumu la askari kudhibiti uvuvi haramu.


“Ikiwa uvuvi haramu tutaukumbatia wenyewe mtajiangamiza wenyewe, ninyi mnaofaidika na ziwa mpo, na athari mnaiona kwanini waje maaskari kutoka Dodoma au sehemu nyingine kuja kufanya msako kwenu, ndugu zangu naomba tushirikiane wote, ngazi ya Kitongoji, Kijiji, Kata wote hili ni jukumu letu suala la uvuvi haramu halikubaliki,” alisema Ndaki.


Ndaki alisema ipo dhana inazungumzwa kuwa uvuvi haramu ni dhana tu inayojengwa na wataalamu na serikali na kuna dhana nyingine kuwa samaki wapo tu ziwani na kuongeza kuwa ikiwa uvuvi haramu tutaukumbatia tutajiangamiza wenyewe.


“Kuna dhana kuwa uvuvi haramu ni dhana tu inayojengwa nawataalam na serikali , kwamba uvuvi haramu hamna, na dhana hiyo inasema kuwa samaki wapo ziwa litaenda wapi, lakini ninyi wenyewe ni mashahidi, kuna wakati mmeanza kulia ninyi wenyewe kwamba samaki hawapo, mpaka sasa upungufu upo sasa kwanini isiwaume ninyi imuume zaidi waziri au Katibu Mkuu wa Uvuvi ambaye nyumbani kwao ni Mtwara bahari pana kuliko ziwa letu, kwanini lisituume sisi,” alisema Ndaki.


Mwenyekiti wa kikundi cha usimamizi shirikishi wa rasilimali za uvuvi (BMU) Wilaya ya Rorya Stephano Mchoye alisema halmashauri ishirikiane na vikundi hivyo ili kudhibiti uvuvi haramu kwa manufaa ya vizazi vilivyopo na vizazi vijavyo.


Ulinzi shirikishi katika ziwa letu haujaanza leo, ninaomba Wizara iangalie zana hizi zinazotumika tika uvuvi haramu zinatoka wapi dawa ya hiyo ikishapatikana naamini uvuvi haramu Tanzania hautapatikana.


Kwa upande wake Nadhil Sadick msambazaji wa mazao ya samaki nje ya nchi aliomba serikali kuangalia tozo mbalimbali wanazotozwa pasipokuangalia madhara yake kwa wanaotoza pamoja na wale wanaotozwa.


Mashimba amewaagiza halmashauri pamoja na mabaraza ya madiwani kuangalia upya tozo wanazotoza katika mialo na katika rasilimali mbalimbali za uvuvi ili kuwapunguzia mzigo wavuvi.


“Niombe halmashauri pamoja na mabaraza yenu ya madiwani hebu kaangalieni upya tozo mnazowatoza kwenye mialo na mazao mbalimbali ya uvuvi, mkaangalie upya tuone tutakapowapunguzia, tuwapunguzie mzigo kwenye hayo maeneo tunayotoka,” alisema Mhe. Ndaki.


“Mimi ni shahidi nimeenda kule Geita tozo za kwetu ngazi ya wizara kwa upande wa dagaa ni mbili tu royality na leseni, lakini zipo tozo 8 ambazo halmashauri inatoza, jumla tozo 10 anatozwa mtu mmoja halmashauri tuangalie pia ustawi wa watu wetu, anaondoka na nini kwenye hicho tunachotaka kumtoza vinginevyo mtapunguza mapato yeye ninyi wenyewe,” alisema Mhe. Ndaki.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na Viongozi wa Serikali wa Kanda ya Ziwa Victoria kuhusu ulinzi na usimamizi shirikishi wa rasilimali za uvuvi katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza. (05.03.2021)


Baadhi ya viongozi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi na viongozi wa serikali wa Kanda ya Ziwa Victoria wakifuatilia mada iliyokuwa ikiwasilishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi, Bw. Emmanuel Bulayi (aliyesimama) wakati wa mkutano kuhusu ulinzi na usimamizi shirikishi wa rasilimali za uvuvi uliofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. (05.03.2021)

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah (wa kwanza kulia) akiwa na timu ya wataalam wakati wa kuandaa maazimio ya mkutano wa viongozi wa serikali wa mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria kuhusu ulinzi na usimamizi shirikishi wa rasilimali za uvuvi uliofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. (05.03.2021)Picha ya pamoja ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (aliyekaa katikati), Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah (aliyekaa kulia kwake) na Makatibu Tawala wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa na Viongozi wengine baada ya kumaliza mkutano wa wadau wa sekta ya uvuvi uliofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza. (06.03.2021)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni