Nav bar

Jumatatu, 8 Februari 2021

WAFUGAJI NA WATENDAJI WATAKIWA KUZINGATIA MWONGOZO WA CHANJO ZA MIFUGO.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewataka wafugaji pamoja na wataalam wa sekta ya mifugo kuusimamia na kuutekeleza mwongozo wa chanjo za mifugo.

 

Waziri Ndaki ameyasema hayo jana (07.02.2021) baada ya kumalizika kwa semina kuhusu masuala ya chanjo za mifugo iliyoandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Kilimo, Mifugo na Maji iliyofanyika katika ukumbi wa Pius Msekwa Jijini Dodoma.

 

“Wizara ilishaandaa na kuzindua mwongozo utakao simamia masuala ya uchanjaji mifugo hivyo ni wajibu wetu sote kuhakikisha tunausimami na kuutekeleza badala ya kusubiri mpaka sheria zitumike,” alisema Mhe. Ndaki.

 

Akizungumza na wajumbe hao wa kamati, Waziri Ndaki amewaomba pindi watakapo rejea majimbo kwao kila mmoja akasaidie kuhakikisha anasimamia utekelezaji wa mwongozo huo kwani kwa kufanya hivyo nchi itakuwa na uhakika wa kuwa na mifugo iliyo na afya bora na ambayo ipo salama hivyo kuongeza thamani ya mazao yanayotokana na mifugo hiyo.

 

Pia alieleza kuwa wizara inaendelea kuboresha huduma za chanjo kwa kuendelea na mkakati wa kuhakikisha inakamilisha uzalishaji wa chanjo zote 13 za magonjwa ya kimkakati ili wafugaji wasiendelee kuteseka dhidi ya magonjwa hayo pindi chanjo zitakapokamilika. Hivyo amewaomba wajumbe wa kamati hiyo kwenda kusaidia kutoa elimu kwa wafugaji na wananchi kwa ujumla katika maeneo wanayotoka ili wote kwa pamoja waweze kufahamu umuhimu wa chanjo kwa mifugo.

 

Aidha, Waziri Ndaki amesema kuwa katika semina hiyo wamepokea michango mizuri sana kutoka kwa wajumbe wa kamati, kuhusu masuala ya chanjo, mwongozo wa chanjo na mambo mengine ya sekta ya mifugo. Pia amesema amewaomba wajumbe hao wa kamati kwenda kusimamia utekelezaji wa maelekezo yanayotolewa na serikali kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa katika maeneo wanayotoka ili malengo yaliyowekwa yaweze kufikiwa.

 

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mhe. Christine Ishengoma alisema upo umuhimu wa maafisa ugani kuhakikisha wanafanya ufuatiliaji kuhakikisha wafugaji wanachanja mifugo yao kwani kwa kutofanya hivyo magonjwa ya mifugo yataendelea kusambaa hasa pale mifugo iliyochanjwa ikichanganyika na isiyochanjwa.

 

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul, amewataka wakurugenzi wa halmashauri kuusoma vizuri mwongozo wa chanjo na kuangalia uwezekano wa kuwatumia wataalam wa mifugo waliomaliza vyuo wakishirikiana na madaktari wa mifugo wa halmashauri kutoa chanjo za mifugo.

 

Gekul amesema kuwa kwa kufanya hivyo halmashauri zitakuwa zinapata mapato ambayo yatasaidia pia katika kukarabati na kujenga miundombinu ya mifugo kama majosho, malambo na minada na hivyo kuleta manufaa kwa wafugaji pia.

 

Vilevile alisema kuwa wizara ilishatoa bei elekezi za chanjo hizo ambapo kila mmoja anatakiwa kuzifuata na endapo katika utekelezaji kutakuwa na changamoto yoyote ni vema wahusika wakafanya mawasiliano na wataalam wa wizara. Pia amesema wizara imejipanga kuhakikisha inaendelea kutoa elimu kuhusu chanjo kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI pamoja na Chama cha Wafugaji ambapo pia amewataka wataalam wa mifugo katika mikoa na halmashauri kuhakikisha wanatumia mikutano ya kisheria iliyopo katika ngazi mbalimbali kutoa elimu kuhusu masuala ya chanjo.

 

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof.Elisante Ole Gabriel alisema kuwa vipaumbele vikubwa vilivyopo katika sekta ya mifugo kwasasa ni kushughulikia afya ya mifugo kwa ujumla, kuboresha kosaafu za mifugo ili kupata mifugo iliyo bora na kujenga na kukarabati miundombinu ya mifugo kama vile majosho, malambo, masoko (minada) na uhamasishaji wa ujenzi wa viwanda kwa ajili ya kuchakata mazao yatokanayo na mifugo.

 

Kwa upande wa chanjo za mifugo, Prof. Gabriel alisema upo umuhimu kwa nchi kuzalisha chanjo zake yenyewe kwani kwa kutegemea chanjo kutoka nje ni rahisi kwa mtu mwenye nia mbaya kuweka kemikali ambazo zinaweza kuidhuru mifugo. Lakini pia alisema kwa nchi kuzalisha chanjo yenyewe kutasaidia kutoa ajira kwa wahitimu kutoka katika vyuo vya hapa nchini, kuongeza kipato katika nchi na kujihakikishia usalama wa chanjo zinazokwenda kutumika katika kuchanja mifugo ya hapa nchini na hata nje ya nchi.

 

Prof. Gabriel alisema kuwa asilimia 60 ya magonjwa wanayougua binadamu yanatokana na magonjwa yanayohama kutoka kwenye mifugo, hivyo mkazo, hivyo mkazo mkubwa ukiwekwa kwenye kudhibiti afya ya wanyama serikali itaokoa fedha takribani Sh. Bilioni 160 zinazotumika na Wizara ya Afya kutibu magonjwa hayo.

 

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Dkt. Stella Bitanyi amesema wakala hiyo ina majukumu mbalimbali ikiwemo utafiti na utambuzi wa magonjwa ya mifugo na kuhakiki ubora wa mifugo na kuzalisha chanjo za magonjwa ya mifugo.

 

Dkt. Bitanyi amesema TVLA imepata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kufikisha huduma zake katika mikoa, lakini pia wameweza kuzalisha chanjo 6 za magonjwa ya kimkakati kati ya magonjwa 13 na mwezi Machi mwaka huu wanatarajia kuzalisha chanjo ya saba.

 

Wakala hiyo ya Maabara ya Veterinari kwa sasa inahitaji kupata sh. Bilioni 2.6 ili kujiimarisha katika miundombinu, vifaa vya maabara na wataalam ambapo watakuwa na uwezo wa kuzalisha sh. Bilioni 10.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Kilimo, Mifugo na Maji, Mhe. Dkt.  Christine Ishengoma (wa pili kutoka kulia), Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (wa pili kutoka kushoto), Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Pauline Gekul (wa kwanza kushoto) na Katibu Mkuu anayesimamia sekta ya Mifugo, Prof. Elisante Ole Gabriel (wa kwanza kulia) wote kwa pamoja wakiandika hoja zilizokuwa zikiulizwa na wajumbe wa kamati hiyo (hawapo pichani) wakati wa semina iliyoandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhusu masuala ya chanjo za mifugo. Semina hiyo imefanyika katika ukumbi wa Pius Msekwa Jijini Dodoma. (07.02.2021)

Kaimu Mtendaji Mkuu – Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Dkt. Stella Bitanyi akiwasilisha mada kuhusu majukumu na mipango ya Wakala ya Maabara ya Veterinari kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Kilimo, Mifugo na Uvuvi wakati wa semina iliyoandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhusu masuala ya chanjo za mifugo. Semina hiyo imefanyika katika ukumbi wa Pius Msekwa Jijini Dodoma. (07.02.2021)

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mifugo, Dkt. Gibonce Kayuni (kulia aliyesimama) akiwasilisha mada kuhusu masuala ya chanjo za mifugo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Kilimo, Mifugo na Maji wakati wa semina iliyoandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhusu masuala ya chanjo za mifugo. Semina hiyo imefanyika katika ukumbi wa Pius Msekwa Jijini Dodoma. (07.02.2021)

Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Kilimo, Mifugo na Maji wakiwa pamoja na wataalam kutoka WMUV, wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa wakati wa semina iliyoandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhusu masuala ya chanjo za mifugo. Semina hiyo imefanyika katika ukumbi wa Pius Msekwa Jijini Dodoma. (07.02.2021)

Baadhi ya Viongozi na Wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakiandika hoja na maelekezo yaliyokuwa yanatolewa na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Kilimo, Mifugo na Maji wakati wa semina iliyoandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhusu masuala ya chanjo za mifugo. Semina hiyo imefanyika katika ukumbi wa Pius Msekwa Jijini Dodoma. (07.02.2021)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni