Nav bar

Jumamosi, 2 Januari 2021

TOZO ZISIZO RAFIKI KUKUZA SEKTA ZA MIFUGO NA UVUVI KUONDOLEWA

Na. Edward Kondela

 

Serikali imesema inatafuta namna ya kuwa na kituo kimoja cha kulipia tozo zote za mazao ya mifugo na uvuvi pamoja na kuondoa tozo ambazo zinakwamisha sekta hizo zisikue.

 

Akizungumza jana (30.12.2020) na baadhi ya wavuvi katika Kata ya Nyamikoma, iliyopo Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu, wakati wa ziara yake ya siku moja mkoani humo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amesema wizara itaangalia tozo ambazo zitakuwa rafiki kwa wawekezaji, wafanyabiashara pamoja na wafugaji na wavuvi wa hali ya chini ili kuhakikisha sekta za mifugo na uvuvi zinachangia kwa sehemu kubwa pato la taifa.

 

“Tutaenda kuangalia ni tozo zipi na baadhi tayari mmeshazitaja zikiwemo za kusafirisha mazao ya mifugo na uvuvi nje ya nchi halafu tunatafuta namna ya kuwa na kituo kimoja cha kulipia hizi tozo zote.” Amesema Mhe. Ndaki

 

Waziri Ndaki ambaye amefuatana na Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe. Pauline Gekul ameongeza kuwa uwepo wa tozo ambazo zitakuwa rafiki katika kukuza sekta za mifugo na uvuvi kutasababisha watu wengi kuwekeza katika sekta hizo na kuongeza pato la taifa kwa kuwa shughuli za kuchumi zitaongezeka.

 

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul ameendelea kusisitiza kuwa watu wanaondelea kujihusisha na uvuvi haramu kuacha mara moja vitendo hivyo kwa kuwa wizara haitafumbia macho ambao bado hawataki kuacha kuharibu mazao ya uvuvi kupitia vitendo hivyo.

 

Amesema ni wakati sasa jamii kushirikiana na serikali kuwabaini watu wanaojihusisha na uvuvi haramu kwa kuwa wanaishi katika maeneo wanayofahamika ili serikali ichukue hatua na kwamba Wizara ya Mifugo na Uvuvi itazidi kutoa elimu juu ya athari ya uvuvi haramu kwa jamii na taifa kwa ujumla.

 

Siku moja kabla ya kuanza ziara ya kikazi Mkoani Simiyu, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki wakati akihitimisha ziara ya siku mbili Mkoani Mwanza amefika katika Kijiji cha Kitongosima kilichopo Wilaya ya Magu mkoani humo na kuzungumza na jamii ya wavuvi na kuwasisitiza waanze kufuga samaki kupitia njia za vizimba na mabwawa ili kujiongezea kipato na kuongeza kuwa mahitaji ya soko la samaki kwa sasa ni makubwa.

 

Mhe. Ndaki amemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah kuhakikisha anaanzisha utaratibu wa kuwepo kwa kizimba cha mafunzo kwa ajili ya kufugia samaki na kuhakikisha wataalamu kutoka wizarani wanafika katika kijiji hicho kuwafundisha wananchi namna ya kufuga na kulisha samaki ili jamii ya hapo iweze kupata mapato kupitia mazao ya uvuvi.

 

Waziri Ndaki amebainisha hayo baada ya kutembelea vizimba vya kufugia samaki katika kijiji hicho vinavyomilikiwa na Shamba la Konga na kufurahishwa na namna mwekezaji anavyofuga samaki kwa wingi kwa njia ya vizimba ndani ya Ziwa Victoria kwa kuwa ni sera ya serikali kuhakikisha katika kipindi cha miaka mitano ajira zaidi ya elfu arobaini na tano zinapatikana kupitia ufugaji wa samaki.

 

Katika kuhakikisha wananchi wa Kijiji cha Kitongosima wananufaika kupitia ufugaji wa samaki Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Bw. Lutengano Mwalwiba amewataka wanakijiji hao kujiunga katika ushirika ili halmashauri hiyo iweze kuwakopesha fedha kwa ajili ya shughuli za uvuvi huku Mwenyekiti wa Chama cha Wafuga Samaki Ziwa Victoria Bw. Cyprian Matembo amemuomba Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki kuangalia namna wizara inavyoweza kuwasaidia kupata vyakula vya samaki kwa bei nafuu kwa kuwa kwa sasa vyakula vingi vimekuwa vikiagizwa kutoka nje ya nchi na kuongeza gharama za uzalishaji.

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki leo (31.12.2020) anahitimisha ziara ya kikazi katika mikoa mitatu ya Kanda ya Ziwa kwenye Mkoa wa Shinyanga, baada ya kufanya ziara kwenye mikoa ya Mwanza na Simiyu, akiambatana na Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe. Pauline Gekul.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa kwanza kushoto) akifuatiwa na Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe. Pauline Gekul wakipatiwa maelezo na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah, namna ya kufuga samaki kwa njia ya vizimba wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri Ndaki katika Kijiji cha Kitongosima kilichopo Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza, kujionea namna mwekezaji Shamba la Konga anavyofuga samaki kupitia vizimba ndani ya Ziwa Victoria. (31.12.2020)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na baadhi ya wavuvi katika Kata ya Nyamikoma, iliyopo Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu, wakati wa ziara yake ya siku moja mkoani humo, na kubainisha kuwa serikali inatafuta namna ya kuwa na kituo kimoja cha kulipia tozo zote za mazao ya mifugo na uvuvi pamoja na kuondoa tozo ambazo zinakwamisha sekta hizo zisikue na kuainisha tozo ambazo zitakuwa rafiki katika kuzifanya sekta hizo kuchangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa. (31.12.2020)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akishuhudia na kuhesabu idadi ya vizimba vya kufugia samaki vilivyopo ndani ya Ziwa Victoria katika Kijiji cha Kitongosima kilichopo Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza, ambavyo vinamilikiwa na Shamba la Konga na kuwataka wananchi wa kijiji hicho kuanza kufuga samaki ili wajiongeze kipato kwa kuwa mahitaji ya soko la samaki yanayongezeka na kutaka kuanzishwa kwa vizimba vya mafunzo katika kijiji hicho kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi. (31.12.2020)

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul akizungumza na baadhi ya wavuvi katika Kata ya Nyamikoma, iliyopo Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu akiwataka watu wanaondelea kujihusisha na uvuvi haramu kuacha mara moja vitendo hivyo na kubainisha ni wakati sasa jamii kushirikiana na serikali kuwabaini watu wanaojihusisha na uvuvi haramu kwa kuwa wanaishi katika maeneo wanayofahamika ili serikali ichukue hatua. (31.12.2020)




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni