Nav bar

Jumatano, 16 Desemba 2020

UFUGAJI WA SAMAKI KATIKA MABWAWA, VIZIMBA KUPUNGUZA UVUVI HARAMU

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amesema ufugaji wa Samaki katika Mabwawa na Vizimba ukihamasishwa na kupewa msukumo mkubwa utasaidia kuongeza wingi wa samaki na utasaidia kupunguza uvuvi harama katika maji ya asili.

 

Ndaki aliyasema hayo alipotembelea Shamba la Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda lilipo jijini Dodoma Disemba 9, 2020.

 

Alisema kuwa serikali imefanya kazi kubwa katika kuimarisha sekta ya uvuvi ikiwemo ufugaji wa samaki katika vizimba na mabwawa lakini alisisitiza kuwa kunahitajika kuongeza nguvu na jitihada zaidi kuwahamasisha wananchi kujiingiza katika ufugaji wa samaki ili kujiongezea kipato na kupunguza utegemezi wa mazao ya samaki kutoka katika maji ya asili.

 

“Ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba na mabwawa utatusaidia kupunguza purukushani kati ya serikali na wavuvi haramu kwa sababu kama samaki wengi watapatikana kupitia ufugaji, watu hawataona haja ya kuhangaika na uvuvi usio na tija,” alisema Ndaki huku akiongeza kuwa;

 

“Tunahitaji kufanya jitihada zaidi kutangaza na kuhamasisha ufugaji wa samaki hasa kwa kutumia mabwawa ya gharama nafuu kama malambo ili wafugaji na wananchi kwa ujumla waweze kuona ufugaji huo ni nafuu na wanaweza kupata kipato kupitia kazi hiyo,” alisema Ndaki

 

Aliongeza kwa kusema kuwa hamasa ya ufugaji wa samaki ikiwa kubwa na wanunuzi nao wataongezeka jambo ambalo litapelekea pia kuongezeka kwa wawekezaji katika vyakula na ukuzaji wa vifaranga na hivyo kutatua changamoto iliyopo sasa ya uchache wa vifaranga na vyakula vya samaki.


“Ndani ya Wizara tutaona namna ya kujipanga ili tuendelee kuiwezesha zaidi hii sekta ya uvuvi iweze kukua zaidi na kuongeza kipato cha watu wetu na kutoa mchango mkubwa katika pato la Taifa,” alisisitiza Ndaki

 

Awali wakati akimkaribisha Waziri huyo Mteule Shambani hapo, Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda alisema kuwa changamoto kubwa anayoipata shambani hapo ni kutopatikana kwa urahisi kwa vifaranga vya samaki pamoja na chakula cha uhakika.

 

“Hapa tunapata changamoto ya vifaranga vya samaki havipatikani kwa urahisi lakini pia hakuna mahala ambapo unaweza kusema hapa wanazalisha chakula cha uhakika,” alisema Pinda

 

Aliongeza kwa kusema kuwa pamoja na jitihada kubwa za serikali katika kuimarisha sekta ya uvuvi lakini angetamani kuona sekta hiyo inaendelea kupewa nafasi kubwa zaidi hasa katika ufugaji wa samaki wa kutumia mabwawa na vizimba kwani utasaidia wananchi kujipatia kipato na kukuza uchumi wao.

 

Naye, Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah alisema kuwa kwa sasa serikali inaendelea kukarabati vituo vya uzalishaji wa vifaranga ili kuongeza uwezo wa kuzalisha ikiwemo kuimarisha mashamba darasa ili kufundisha watu namna ya kutengeneza chakula cha samaki na ufugaji wa samaki.

 

Dkt. Tamatamah aliongeza kuwa serikali inaendelea kuhamasisha uwekezaji katika uzalishaji wa vifaranga na uzalishaji wa Chakula na kwa sasa wapo katika mazungumzo na serikali ya Misri ili Kampuni zao ziweze kuwekeza katika uzalishaji mkubwa wa vifaranga na vyakula vya samaki hapa nchini.

 

Ndaki alifanya ziara hiyo muda mfupi baada ya kuapishwa rasmi kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Disemba 9, 2020, na kazi yake ya kwanza ilikuwa kutembelea machinjio ya Dodoma na Shamba la Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki akiwapa chakula Samaki katika moja ya Mabwawa ya samaki yaliyopo katika shamba la Waziri Mkuu (Mst) wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda (wa kwanza kushoto) alipotembelea shamba hilo lililopo jijini Dodoma Disemba 9, 2020. Kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul.

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (kulia) akimueleza jambo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge (kushoto) walipotembelea Machinjio ya Dodoma yaliyopo jijini Dodoma Disemba 9, 2020. Katikati ni Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (wa pili kutoka kulia aliyeinama) akikagua mbuzi wanaosubiria kuchinjwa alipotembelea Machinjio ya Dodoma yaliyopo jijini Dodoma Disemba 9, 2020. Wa kwanza kulia aliyeshika mbuzi ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul. Wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel na wapili ni Meneja wa Machinjio ya Dodoma, Victor Mwita.

Waziri Mkuu (Mst.) wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda (kulia) akiongoza na Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (kushoto) alipokuwa akimkaribisha Waziri wa Mifugo na Uvuvi pamoja na Ujumbe wake uliotembelea shambani kwake jijini Dodoma Disemba 9, 2020. Nyuma yao, kushoto ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki na kulia ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul.

Sehemu ya Wafanyakazi wa Machinjio ya Dodoma yaliyopo jijiji Dodoma wakiwa katika hatua za kuwaandaa mbuzi waliochinjwa tayari kwa ajili ya kupelekwa sokoni.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki akikagua moja ya sehemu ya kuhifadhia wanyama waliochinjwa alipotembelea Machinjio ya Dodoma yaliyopo jijini Dodoma Disemba 9, 2020. Wa kwanza kulia ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul na wapili kutoka kulia ni Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel.









Hakuna maoni:

Chapisha Maoni