Nav bar

Ijumaa, 4 Desemba 2020

PINDA AWATAKA WATAAMU WA MIFUGO KUISHAURI SERIKALI KUBORESHA SEKTA YA MIFUGO

 Na Mbaraka Kambona, Dodoma

Wataalamu wa Uzalishaji na Uendelezaji wa Mifugo na Uvuvi nchini wametakiwa kutumia taaluma zao kuishauri Serikali namna bora ya kuboresha na kuendeleza Sekta ya mifugo na Uvuvi ili ziweze kutoa mchango wa kutosha katika kukuza uchumi wa nchi na kuongeza Pato la taifa na uchumi wa mtu mmoja mmoja.

Waziri Mkuu (Mst) wa   Awamu ya Nne wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Pinda aliyasema hayo kwa  Wataalamu wa Uzalishaji na Uendelezaji wa Mifugo na Uvuvi waliotembelea nyumbani kwake jijini Dodoma Jana jioni (Disemba 3, 2020) kwa lengo la kujifunza na kubadilishana utaalamu kuhusu masuala ya  ufugaji, uvuvi na kilimo.

Alisema kuwa takwimu zinaonesha kuwa nchini kuna Ng’ombe wengi zaidi ya milioni 30, Mbuzi zaidi ya milioni 20 na mifugo mingine mbalimbali vyote hivyo kama vikisimamiwa vizuri vinaweza kusaidia kukwamua wananchi kutoka katika lindi la umasikini hasa ikizingatiwa watu wengi wanaojishughulisha na ufugaji ni wafugaji wadogowadogo ambao vilevile ndio wakulima katika maeneo ya vijijini.

 “Kwa hili lazima niseme ukweli bado panahitajika kazi kubwa sana, lakini napata faraja kwa sababu Rais wetu John Pombe Magufuli katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2020/ 2025 unaona dhamira ipo kubwa ya namna ya kuleta mabadiliko makubwa kwenye sekta ya mifugo, uvuvi na kilimo hivyo nyie Wataamu nadhani ndio kipindi muafaka sasa kwa kusaidia  nchi kimawazo,” alisema Pinda

 “Pia nafarijika kwa kuamua kufanya mkutano wenu wa kujadili masuala ya kuinua viwango vya minyororo ya thamani ya mazao ya mifugo hapa Dodoma hivyo nina hakika kabisa baada ya mkutano wenu mtatoka na vitu vikubwa ambavyo baadae vitakuwa msaada kwa ushauri kwa upande wa Serikali,” aliongeza Pinda

Aidha, aliongeza kwa kusema kuwa anatamani sana Wataalamu hao wakaweka mifumo mizuri ya kuwavuta vijana wanaomaliza elimu zao kujiingiza katika sekta ya ufugaji, uvuvi na kilimo ili waweze kupata nafasi ya kutambua kwamba sekta hizi ni fursa kubwa inayoweza kuleta mabadiliko makubwa sana katika uchumi wa nchi na mwananchi mmoja mmoja.

Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Wataamu wa Mifugo Tanzania (TSAP), Dkt. Daniel Komwihangilo alisema wao kama wataalamu wa mifugo na uvuvi wamefaidika sana na ziara hiyo na wameweza kuona kwamba kumbe mambo yanawezekana kinachohitajika ni juhudi na uvumilivu katika kuanzisha jambo lolote.

“Kikubwa tulichojifunza hapa ni kwamba mifugo inaweza kufugwa kwa tija kama utazingatiwa ushauri, sayansi ya ufugaji na tekinolojia kama ambazo Mhe. Pinda anazitumia, hivyo kama kuna mtu anataka kufanya anavyofanya sio swala la kuanza leo na hapo hapo uone matokea hapana mambo haya yanahitaji muda na kuzingatia ushauri wa Wataalamu,” alisema Dkt. Komwihangilo

Wataalamu hao wa mifugo wamekutana jijini Dodoma katika Kongamano la siku 3 kuanzia Disema 2- 4, 2020 kwa lengo la kujadiliana namna bora ya Kuinua viwango vya minyororo ya thamani ya mifugo na uvuvi ili sekta hizo ziweze kuwa na tija kubwa kwa nchi. 



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni