Nav bar

Jumatatu, 7 Desemba 2020

SERIKALI YAONYA ‘WANAOCHAKACHUA’ MAZIWA

Na Mbaraka Kambona, Dar es Salaam

 

Serikali imewataka baadhi ya wafugaji wenye mtindo wa kuongeza unga katika Maziwa kuacha kufanya hivyo kwani sio tu inaharibu biashara ya maziwa katika soko la ndani ya nchi bali hata soko la nje.

 

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel alitoa onyo hilo alipotembelea Banda la Maonesho la Bodi ya Maziwa lililopo katika Viwanja vya Maonesho ya bidhaa za Viwanda yanayoendelea kufanyika katika Viwanja vya Maonesho vya Mwl. Nyerere jijini Dar es Salaam Disemba 6, 2020.

 

Prof. Gabriel alisema wanaofanya hivyo wanapaswa kutambua kuwa kitendo hicho ni kibaya, wanajidanganya wao wenyewe na wasipo jirekebisha wataishia pabaya.

 

“Bodi endeleeni kutafuna wale wote ambao wanachakachua maziwa kadri iwezekanavyo na sheria ichukue mkondo wake na hatutakuwa na huruma yeyote kwa sababu wanaharibu taswira nzima ya biashara ya maziwa ndani na nje ya nchi,” alisema Prof. Gabriel

 

Aliongeza kwa kusema kuwa Wafugaji wajue kwamba Serikali ina vipimo ambavyo vinaweza kutambua maziwa yaliyowekwa unga na hivyo aliwataka wale wote wanaojihusisha na uhalifu huo kuacha kufanya hivyo kwani watakaokutwa sheria itachukua mkondo wake.

 

Aidha, Prof. Gabriel aliitaka Bodi ya Maziwa kuhakikisha unywaji wa maziwa unaongezeka na wawahamasishe Watanzania kadri iwezekanavyo walau ndani ya miaka mitano ijayo wazidi walau lita zaidi ya 100 kwa mwaka kwani kwa sasa unywaji upo kwenye lita 54 jambo ambalo ni aibu kwa nchi yenye ng’ombe milioni 33. 4 na inazalisha lita za maziwa bilioni 3.01 huku kukiwa na viwanda vya kuchakata maziwa 99.

 

“Bodi fanyeni kazi ya ziada, msifanye kazi kwa mazoea, wekeni sayansi kwenye kazi yenu na pia pimeni elimu mliyoitoa imeeleweka kiasi gani ili wale wanaofanya vizuri muwapongeze na wale wanaokosea muwaadhibu kwa mujibu wa sheria na taratibu ili kuifanya tasnia iwe bora zaidi,” aliongeza Prof. Gabriel

 

Aliongeza kuwa anaamini tasnia hiyo ya maziwa itaendelea kusimamiwa vizuri sana na itachangia vizuri katika uchumi wa kati ambao Dkt. John Pombe Magufuli ameshafanya kazi ya ziada kuipeleka nchi katika uchumi wa kati miaka mitano kabla, hivyo anaamini nchi itaendelea kupanda kiuchumi na zao la maziwa ni muhimu likaendelea kuimarishwa ili litoe mchango unaohitajika katika kukuza pato la taifa.

 

“Bodi ya Maziwa hakikisheni ubora wa maziwa unakuwepo na yapatikane kwa wingi kwa ajili ya kujenga afya bora kwa watumiaji,” alifafanua Prof. Gabriel

 

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Godwin Gondwe alisema katika Wilaya ya Temeke na Mkoa wa Dar es Salaam watahakikisha wanaendelea kuhamasisha unywaji wa maziwa kupitia michezo mbalimbali na wamejipanga hivi karibuni wanatarajia kufanya tamasha kubwa ambalo litatumika kuchagiza pia unywaji wa maziwa nchini.

 

Kaimu Msajili wa Bodi ya Maziwa, Noely Byamungu alisema kuwa wamejipanga kuhakikisha wanajenga utamaduni kwa jamii kupenda kunywa maziwa na wameanza na kundi la wanamichezo lakini kuna mpango mkakati wa kitaifa wa kuwafikia Watoto mashuleni.

 

“Mpango wa kitaifa unalenga kukuza utamaduni wa unywaji wa maziwa kwa Watoto wadogo na kwa kufanya hivyo kutasaidia kujenga jamii inayopenda kunywa maziwa, hivyo tunawaomba Waandishi wa Habari mtusaidia kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa unywaji wa maziwa ili tuwe na jamii inayopenda kunywa maziwa kwa afya,” alisema Byamungu

 

Aliongeza kwa kusema kuwa katika kutekeleza mpango huo Bodi itashirikisha wadau tofautitofauti ikiwemo Wizara ya TAMISEMI, Wizara ya Afya na Wizara ya Elimu na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kuhakikisha unywaji wa maziwa unaongozeka lakini pia wafugaji wazalishe na waweze kupata masoko ya uhakika.

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (wanne kutoka kushoto) akiwa pamoja na washiriki wengine wakifurahia bonanza la Maziwa lililoandaliwa na Bodi ya Maziwa lililofanyika katika Viwanja vya Maonesho vya Mwl. Nyerere (Sabasaba) jijini Dar es Salaam Disemba 6, 2020.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (watatu kutoka kushoto) akiwapigia makofi kuwapongeza wacheza sarakasi wakati akiongoza vikundi mbalimbali vya mazoezi vilivyoshiriki mbio za taratibu (Jogging) katika bonanza la maziwa lililofanyika jijini Dar es Salaam Disemba 6, 2020. Washiriki hao walikimbia takriban kilomita 5 kutoka Uwanja wa Taifa mpaka kwenye Viwanja vya Maonesho ya Mwl. Nyerere (Sabasaba) kwa kupitia njia ya Police Changombe.

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati aliyevaa Miwani) akimsikiliza kwa makini mmoja wa Maafisa wa Kampuni ASAS alipotembelea banda la Kampuni hiyo lililopo katika Maonesho ya bidhaa za Viwanda yanayofanyika katika Viwanja vya Mwl. Nyerere (Sabasaba) jijini Dar es Salaam Disemba 6, 2020.

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akimkabidhi Kaimu Mkurugenzi, Masoko na Uzalishaji, Stephen Michael cheti cha ushiriki wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika Bonanza la Maziwa lililofanyika katika Viwanja vya Maonesho vya Mwl. Nyerere (Sabasaba) jijini Dar es Salaam Disemba 6, 2020.

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akimkahidhi Naibu Mkurugenzi, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Latifa Khamis cheti cha ushiriki katika bonanza la maziwa lililofanyika katika Viwanja vya Mwl. Nyerere jijiji Dodoma Disemba 6, 2020.


Mmoja wa washiriki wa Bonanza la Maziwa akifurahia moja ya bidhaa ya maziwa inayozalishwa na Kampuni ya Asas katika bonanza hilo lililofanyika katika Viwanja vya Maonesho vya Mwl. Nyerere (Sabasaba) jijini Dar es Salaam Disemba 6, 2020.


Kaimu Msajili wa Bodi ya Maziwa, Noely Byamungu (kulia) akiongea na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Godwin Gondwe muda mfupi baada ya kumalizika kwa Bonanza la Maziwa lililofanyika katika Viwanja vya Mwl. Nyerere (sabasaba) jijini Dar es Salaam Disemba 6, 2020.


Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akionesha kuvutiwa na moja ya bidhaa inayozalishwa na Wajasiriamali kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alipotembelea Banda la chuo hicho katika Maonesho ya Bidhaa za Viwanda yanayofanyika katika Viwanja Maonesho vya Mwl. Nyerere (Sabasaba) Dar es Salaam Disemba 6, 2020.


Kaimu Msajili wa Bodi ya Maziwa, Noely Byamungu (kulia) akimueleza jambo Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (wa kwanza kushoto) alipotembelea banda la Maonesho la Bodi hiyo katika Maonesho ya Bidhaa za Viwanda yanayofanyika katika Viwanja vya Mwl. Nyerere (sabasaba) jijiji Dar es Salaam Disemba 6, 2020.


Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akifurahia jambo na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Godwin Gondwe wakati wakiagana baada ya kumalizika kwa Bonanza la Maziwa lililofanyika katika Viwanja vya Mwl. Nyerere (Sabasaba) jijini Dar es Salaam Disemba 6, 2020.Hakuna maoni:

Chapisha Maoni