Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah amefanya ziara ya kikazi ya siku mbili katika mikoa ya Pwani na Tanga na kubainisha kuridhishwa na ujenzi wa majengo maalum kwa ajili ya ofisi za Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) kupitia Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFISH).
Akizungumza na viongozi wa
BMU na wananchi kwa nyakati tofauti mara baada ya kutembelea majengo hayo
kwenye kata ya Dunda, wilaya ya Bagamoyo na kata ya Saadani, wilaya ya Chalinze
katika mkoa wa Pwani, kata ya Kipumbwi, wilaya ya Pangani na kata ya Zingibari,
wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, Dkt. Tamatamah amesema ujenzi wa majengo hayo
unaendelea vizuri huku akiwataka makandarasi kuhakikisha majengo hayo
yanakamilika ifikapo mwezi Desemba Mwaka 2020 kama makubaliano yalivyo kwenye
mikataba.
“Nimeridhishwa na ujenzi wa
baadhi ya majengo hayo kupitia mradi wa SWIOFISH ila ninawaagiza makandarasi
kuhakikisha majengo haya yanakamilika kwa wakati ili kuanzia mwezi Januari mwaka
2021 yaanze kutumika na viongozi wa BMU kama ofisi katika shughuli mbalimbali
za kulinda rasilimali za uvuvi kwenye Ukanda wa Pwani, mkandarasi yeyote ambaye
hatakamilisha jengo kwa wakati tutamchukulia hatua,” Alisema Dkt. Tamatamah
Ameongeza kuwa mradi huo
ambao unahusisha majengo matano ya BMU likiwemo la kata ya Sudi, halmashauri ya
wilaya ya Mtama mkoani Lindi utakaogharimu zaidi milioni 700 ikiwa ni mkopo
kutoka Benki ya Dunia, kukamilika kwake kutasaidia kusimamia zaidi rasilimali
za uvuvi ikiwa ni pamoja na kutunza nyaraka muhimu.
“BMU zina matatizo ya ofisi
na mmekuwa mkishiriki kutokomeza uvuvi haramu, mkikamata nyavu haramu mnaziweka
wapi? Ndiyo maana tunawajengea ofisi kupitia mradi wa SWIOFISH. Nia ni ulinzi
shirikishi kwa kuwapatia zana, elimu na miundombinu mbalimbali.” Amebainisha
Dkt. Tamatamah.
Aidha, amesema mara baada
makandarasi kukabidhiwa ramani za majengo hayo Mwezi Julai Mwaka 2020 na
kutakiwa kuanza mara moja ujenzi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi inayosimamia mradi
wa SWIOFISH kwa upande wa Tanzania Bara inatarajia mara baada ya kukabidhiwa
majengo hayo Mwezi Desemba Mwaka 2020, mradi utanunua pia samani na vitendea
kazi vingine vya ofisi zikiwemo kompyuta.
Pia, amesema lengo la mradi
huo unaotekelezwa katika nchi tatu za Tanzania, Msumbiji na Comoro kwa Ukanda
wa Pwani ya Bahari ya Hindi ni kuwajengea uwezo wananchi hususan jamii ya
wavuvi kusimamia rasilimali za uvuvi kupitia vikundi, ambapo kwa Zanzibar
unasimamiwa na Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi hali kadhalika ikiwemo
taasisi ya muungano ya Mamlaka ya Usimamizi wa Uvuvi wa Bahari Kuu (DFSA).
Katika ziara hiyo ya kikazi
ya siku mbili kwenye mradi wa ujenzi wa majengo ya ofisi za Vikundi vya
Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) kupitia Mradi wa Usimamizi
Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi
(SWIOFISH), Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt.
Rashid Tamatamah amesema mradi huo wa miaka sita ulioanza mwezi Juni mwaka 2015
na kutarajiwa kukamilika mwezi Mei mwaka
2021, umekuwa ukiendeleza jitihada za serikali ambazo imekuwa ikifanya tangu
zamani kwenye maeneo yenye shughuli za uvuvi kote nchini katika kusimamia
rasilimali za uvuvi ili kutoa ajira na kuhakikisha mazao ya uvuvi yananufaisha
taifa na mwananchi mmoja mmoja.
“Tunatarajia mradi huu
kukamilika mwezi Mei mwaka 2021 ni mategemeo yetu Benki ya Dunia itaendelea
kutupatia mradi huu ambao umekuwa na matokeo chanya katika kulinda rasilimali
za uvuvi, pia maeneo ambayo mradi huu bado haujafika nchini, serikali imekuwa
ikitenga fedha kuhakikisha rasilimali za uvuvi zinalindwa kwa kukomesha uvuvi
haramu na kutoa elimu juu ya mchango wa seta ya uvuvi kwa jamii ya wavuvi
nchini”. Amesema Dkt. Tamatamah
Ili kuhakikisha serikali
inakusanya mapato mengi kupitia sekta ya uvuvi katibu mkuu huyo amewataka
viongozi wa halmashauri nchini kwenye maeneo zilipo shughuli za uvuvi kuvipatia
vikundi vya BMU mamlaka ya kukusanya mapato, akibainisha kuwa baadhi ya
halmashauri ambazo zimefanya hivyo zimekuwa zikipatiwa makusanyo mengi tofauti
na yale ambayo wamekuwa wakikusanya siku za nyuma.
Nao baadhi ya viongozi wa BMU
wa maeneo ambayo majengo hayo yanajengwa wamepongeza juhudi za serikali kupitia
Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kubainisha kuwa mara baada ya kukamilika kwa
majengo hayo na hatimaye kukabidhiwa kwa ajili ya ofisi watahakikisha
wanayatumia kwa madhumuni yaliyokusudiwa na kuyatunza ili yadumu kwa muda
mrefu.
Wamebainisha kitendo cha
kujengewa majengo maalum kwa ajili ya ofisi kuna dhihirisha namna serikali
inavyotambua mchango wa BMU katika kuhakikisha wanaisaidia kulinda rasilimali
za uvuvi.
Aidha Dkt. Tamatamah amepata
pia fursa ya kufika na kukagua nyumba za Taasisi ya Hifadhi ya Bahari na Maeneo
Tengefu (MPRU) kwenye Hifadhi ya Silikanti Tanga zilizopo Kata ya Kigombe
Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga, ambazo pia zimejengwa kupitia mradi wa SWIOFISH
kwa ajili ya watumishi wa hifadhi hiyo na kuridhishwa na nyumba hizo ambazo
tayari zimekabidhiwa wizarani tangu Mwezi Februari Mwaka 2020 na kutaka
watumishi watakaotumia nyumba hizo kuzitunza ili ziwe na tija kwao.
Katika ziara hiyo Katibu Mkuu
Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah
amezungumza na jamii ya wavuvi na kusikiliza baadhi ya changamoto
zinazowakabili na kuwaahidi kuzifanyia kazi na kwamba wizara imekuwa ikifanya
marekebisho ya kanuni na tozo mbalimbali za uvuvi pamoja na kuhakikisha wavuvi
wanapata masoko ya mazao yao.
Pia, amewasisitiza akinamama
kuendelea na kilimo cha mwani ambacho kimekuwa na tija kwao katika kuendesha
familia zao.
Mratibu wa Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFISH), Bw. Nichrous Mlalila (wa kwanza kulia) akimuelezea Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (wa pili kutoka kushoto), namna mkandarasi anayejenga jengo la BMU kata ya Saadani anavyochelewesha ujenzi huo, hali iliyomlazimu Dkt. Tamatamah kumtaka mkandarasi huyo SARO Builders Ltd kukamilisha ujenzi kwa mujibu wa mkataba. (17.11.2020)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (kushoto) akiangalia mchoro wa ramani wa majengo matano yanayojengwa kwa ajili ya ofisi za Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) katika mikoa ya Pwani, Tanga na Lindi, kupitia wizara hiyo chini ya Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFISH). (17.11.2020)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo
na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (kulia picha ya juu) akipata maelezo ya kukamilika
kwa mradi wa ujenzi wa nyumba za watumishi wa Hifadhi ya Silikanti Tanga
kupitia mradi wa SWIOFISH, kutoka kwa Kaimu Mhifadhi Mfawidhi wa hifadhi hiyo,
Bw. Humphrey Mahudi. (17.11.2020)
Ujenzi wa jengo la ofisi za
Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) katika kata ya
Kipumbwi Wilaya ya Pangani Mkoani Tanga, ambao Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na
Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah ameridhishwa na
maendeleo ya ujenzi huo. (17.11.2020)
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani Mkoani Tanga Bw. Oscar Mbenje akimuelezea Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah namna halmashauri hiyo ilivyofanikiwa kukusanya mapato mengi kupitia Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU).
Moja ya mikutano ambayo
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah amefanya
katika ziara yake ya kikazi ya siku mbili katika mikoa ya Pwani na Tanga,
ambapo pichani akizungumza na wakulima wa zao la mwani katika kata ya Zingibari,
wilaya ya Mkinga, mkoani Tanga. (17.11.2020)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo
na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (wa kwanza kulia) akizungumza na baadhi
ya wadau wa uvuvi katika Kata ya Kipumbwi, wilaya ya Pangani mkoani Tanga,
ambapo wamemuelezea katibu mkuu huyo changamoto za soko la dagaa. (17.11.2020)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni