Nav bar

Jumamosi, 28 Novemba 2020

BARAZA LA VETERINARI LAKIFUNGIA KITUO CHA AFYA SENDEU

Baraza la Veterinari Tanzania limekifungia kituo cha huduma ya afya ya wanyama cha Sendeu kilichopo Wilayani Longido, Mkoani Arusha kwa kubainika kutokuwa na wataalam waliosajiliwa na Baraza hilo.

 

Baraza limefikia hatua hiyo mkoani humo Novemba 22, 2020 kufuatia ukaguzi unaoendelea kufanywa katika mikoa mbalimbali nchini na wakaguzi wa baraza hilo ikiwa ni sehemu ya majukumu yao ya kila siku. 

 

Msajili wa Baraza Veterinari Tanzania, Dkt. Bedan Masuruli alieleza kuhusu uamuzi huo wa baraza ofisini kwake, jijini Dodoma Novemba 23, 2020.

 

Dkt. Masuruli alisema kuwa uamuzi huo wa baraza umefikiwa baada ya kujiridhisha kuwa kituo hicho cha afya ya wanyama kinaendesha shughuli zake kinyume cha taratibu.

 

Aliongeza kuwa wakaguzi wa baraza walipoenda kufanya ukaguzi katika kituo hicho walibaini mapungufu hayo ambayo kimsingi ni kinyume cha taratibu na ni hatari kwa afya ya wanyama.

 

 Aidha, Dkt. Masuruli aliwahimiza wamiliki wote wa vituo vya afya ya mifugo kuhakikisha kuwa vituo hivyo vinasimamiwa kikamilifu na huduma zinazotolewa na wataalam wa mifugo waliosajiliwa na baraza la veterinari Tanzania.

 

Dkt. Masuruli amevisisitiza vituo vingine vyote nchini kuzingatia taratibu zote za kutoa huduma, na baraza halitasita kuchukua hatua kwa vituo vyote vitakavyoshindwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utoaji huduma ya afya ya wanyama.

 

Awali msajili wa Baraza hilo alisema walifanya ukaguzi kwenye mikoa ya Tanga, Shinyanga, Simiyu na Ruvuma na kubaini changamoto za ukiukwaji wa maadili ya utoaji huduma ya afya ya wanyama na kupelekea kulipishwa   faini na wengine kufungiwa kutoa huduma ya afya ya wanyama.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni