Nav bar

Ijumaa, 23 Oktoba 2020

WATUMISHI WATAKIWA KUZIFAHAMU SHERIA NA TARATIBU ZA UTUMISHI WA UMMA.

 Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Zachariyya Kera amewataka watumishi wa umma kujijengea tabia ya kusoma katiba na sheria za kiutumishi ili kuzifahamu sheria na haki zao za msingi.

 

Akiongea wakati alipotembelea ofisi za Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI) (20.10.2020) zilizopo Mkoani Pwani, akiambatana na baadhi ya viongozi waandamizi wa wizara hiyo sekta ya mifugo, Bw. Kera ametoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwataka  wafanyakazi kujua haki zao za msingi na kufuatilia kwa wakati.

 

"Watumishi waelimishwe kuhusu haki zao na wapate stahiki zao kwa wakati na kujijengea tabia ya kusoma sheria na taratibu za kiutumishi ili wasipitwe na mambo mengi." alisema Bw. Kera.

 

Katika ziara hiyo ya baadhi ya viongozi waandamizi wa Wizara ya Mifugo na uvuvi sekta ya mifugo, walipata pia fursa ya kutembelea kituo cha uhimilishaji kanda ya mashariki (kibaha) kilichopo Mkoani humo na Shamba la Malisho Vikuge kujifunza shughuli mbalimbali zinazofanywa na kituo pamoja na shamba hilo.

 

Meneja wa Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI), Dkt. Stella Bitanyi amesema chanjo ni muhimu sana kwa mifugo kwani huboresha afya za mifugo na mfugo ukiwa na afya nzuri hata afya ya binadamu huimarika pale atumiapo, chanjo zinaongeza pato la taifa kwani huzalishwa na kuuzwa.

 

Aidha, Dkt. Bitanyi ametumia nafasi hiyo kuwaeleza watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi changamoto zinazowakabili ikiwa ni pamoja na upungufu wa vifaa vya kisasa vya kufanyia kazi kwani wanatumia teknolojia ya chini sana katika utendaji wao wa kazi.

 

Hata hivyo ameshauri kuwe na utaratibu wa kutoa elimu kwa wataalam ya namna ya kutumia Chanjo kwani wengi hukosea na kuchanja maeneo yasiyostahili.

 

"Elimu ya uchanjaji inahitajika kwa wingi kwa wataalam wetu kwani wanachanja shingoni badala ya kuchanja nyuma ya kwapa kwenye ngozi." Alisisitiza Dkt. Stella.

 

 Mkuu wa kituo cha uhimilishaji kanda ya Mashariki (Kibaha), Bw. Anzigary Kasanga Balaka ameeleza kazi wanazofanya ikiwa ni pamoja na kuzalisha mbegu bora za madume na kuuza, kutoa ushauri kwa wafugaji na kuboresha mifugo yao kwa uhimilishaji, kuratibu Mafunzo ya uhimilishaji na kuuza vitendea kazi vya uhimilishaji kama mitungi ya gesi.

 

Aidha, Viongozi wa TVI, Kituo cha Uhimilishaji na Shamba la Malisho Vikuge waliishukuru serikali ya awamu ya tano kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuendelea kuona umuhimu wa shughuli wanazofanya na kuwatembelea kujionea mazingira ya watumishi wao na changamoto wanazopitia katika maeneo yao ya kazi na kuzitafutia ufumbizi.

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu (WMUV), Bw. Zachariyya Kera (kulia) akitoa ufafanuzi wa hatua na namna mtumishi anavyopandishwa cheo kwa watumishi wa Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI) walipotembelea kituo hicho wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani. (20/10/2020)

Mkurugenzi wa Manunuzi na Ugavi (WMUV), Bw. Emanuel Mayage akipata ufafanuzi wa namna ya kutengeneza chanjo mbalimbali kutoka kwa Meneja wa Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI), Dkt. Stella Bitanyi walipotembelea Taasisi hiyo mkoani Pwani. (20.10.2020)

Meneja wa Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI), Dkt. Stella Bitanyi akitoa taarifa ya Taasisi hiyo kwa watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo) juu ya namna wanavyofanya kazi na mafanikio waliyopata hadi sasa walipotembelea Taasisi hiyo mkoani Pwani. (20.10.2020)





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni