Nav bar

Jumapili, 11 Oktoba 2020

IDARA YA UVUVI YAHAKIKISHA RASILIMALI ZA BAHARI ZINALINUFAISHA TAIFA KIUCHUMI

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imesema ukusanyaji wa takwimu za sekta ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi unalenga kutoa tathmini ya hali ya uvuvi katika ukanda huo na kuhakikisha rasilimali za bahari zinaendelea kuleta manufaa na kuchangia katika uchumi wa nchi.


Akizungumza jijini Dar es Salaam (09.10.2020) wakati wa kufunga mafunzo ya siku mbili ya ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa mazao ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani yanayohusisha maafisa uvuvi na viongozi kutoka Vikundi vya Kusimamia Rasilimali ya Uvuvi Mwaloni (BMU), kutoka Mikoa ya Dar es Salaam katika Wilaya za Kinondoni, Kigamboni na Ilala pamoja na Mkoa wa Pwani ukihusisha Wilaya za Bagamoyo na Chalinze, Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi Bw. Emmanuel Bulayi amesema maendeleo ya wananchi katika eneo hilo yanategemea sana shughuli za uvuvi.


“Kwa hiyo suala la kuchukua takwimu na kujua rasilimali ikoje kila wakati na kila muda ni suala la msingi sana ni ukweli uliowazi maendeleo ya wananchi katika hili eneo yanategemea sana shughuli za uvuvi, hivyo ni muhimu sana halmashauri na wananchi wanakuwa katika mstari wa mbele katika kuhakikisha tunaendelea na uchumi endelevu katika Ukanda wa Pwani kwa manufaa yetu na vizazi vijavyo.” Amebainisha Bw. Bulayi


Aidha, amesema taarifa zinazochukuliwa wakati wa kukusanya takwimu kwa njia ya mfumo wa kieletroniki ni pamoja na kufahamu kiwango cha samaki wanaovuliwa kwa kilo, kwa boti na kwa siku, ni suala la msingi ili baadae serikali iweze kufahamu kiasi gani cha samaki kinachovuliwa na kuweka mipango itakayosaidia mikakati mbalimbali ya maendeleo.


Pia, Bw. Bulayi amewataka wakusanya takwimu kuhakikisha wanakusanya takwimu halisia kwani bila kuzingatia hilo watalidanganya taifa, hivyo wanapaswa wafahamu jukumu kubwa walilonalo kwa ajili ya kuitumikia sekta ya uvuvi nchini.


“Takwimu ndiyo hasa tunasema ni msingi wa sekta ya uvuvi katika kuhakikisha wavuvi wanaendelea, lakini pia sekta inaendelea, lakini pia sekta tunanufaika nayo kwa hiyo bila takwimu hakuna la kuongea.” Amefafanua Bw. Bulayi


Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Emmanuel Bulayi, amewakumbusha pia washiriki wa mafunzo ya siku mbili ya ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa mazao ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani kuwa, ukusanyaji wa takwimu ya sekta ya uvuvi ni takwa la kidunia kupitia Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), lakini pia ni takwa la nchi hivyo washiriki wa mafunzo hayo wana jukumu kubwa katika ukusanyaji wa takwimu sahihi.


Amesema mafunzo ya namna hiyo yanatarajia pia kuendelea kwenye halmashauri 15 katika Ukanda wa Bahari ya Hindi, hivyo kutaka uwepo ushirikiano wa kutosha kati ya maafisa uvuvi na wadau wa sekta ya uvuvi ili kuhakikisha rasilimali za bahari zinalinufaisha taifa.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uratibu wa Sekta kutoka Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw. Yusuf Semuguruka, ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuandaa mafunzo hayo kwa kuwa serikali inaangalia uwepo wa Vikundi vya Kusimamia Rasilimali ya Uvuvi Mwaloni (BMU) katika kusaidia kutafuta taarifa sahihi kwa ajili ya maandalizi ya sera mbalimbali.


Bw. Semuguruka amesema TAMISEMI itafuatilia kuangalia mafunzo hayo namna yanavyowasaidia maafisa uvuvi na viongozi wa BMU katika kukusanya takwimu sahihi.


Kwa upande wao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo ambao wamekuwa wakituma taarifa za takwimu kwa kutumia mfumo maalum wa njia ya simu ya mkononi katika ofisi za makao makuu ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), wakizungumza kabla ya kuahirishwa kwa mafunzo hayo wakiwa kwenye mwalo wa samaki katika soko la Kunduchi jijini Dar es salaam wamesema wamenufaika na mafunzo hayo yakiwemo ya namna ya kupata takwimu kwa usahihi.


Mafunzo ya ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa mazao ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani yamefanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Tanga na baadaye yatafanyika katika Mkoa wa Mtwara kwa maafisa uvuvi na Vikundi vya Kusimamia Rasilimali ya Uvuvi Mwaloni (BMU), ambao wamekuwa wakikusanya takwimu hizo.


Mafunzo hayo yamehusisha ukusanyaji wa takwimu kwa kutumia sampuli za wingi wa samaki, idadi ya uchaguzi wa aina ya vyombo na zana za uvuvi, njia za ukusanyaji takwimu ikiwemo ya kutumia mfumo wa simu ya mkononi, namna ya kupata wastani wa uzito wa samaki pamoja na kufahamishwa umuhimu wa takwimu za uvuvi nchini.


Washiriki wa mafunzo hayo wamepatiwa vifaa mbalimbali vya kukusanyia takwimu katika maeneo ya kazi zikiwemo simu za mkononi, mizani, makoti ya mvua na mabuti.


Mafunzo ya ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa mazao ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani yameandaliwa kupitia mradi wa usimamizi wa samaki wanaopatikana katika tabaka la maji la juu na kati unaotekelezwa kwa ushirikiano na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO).

Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Emmanuel Bulayi akizungumza na washiriki wa mafunzo ya ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa mazao ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani yaliyofanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam na kusisitiza umuhimu wa kupata takwimu sahihi ili kulinda rasilimali za bahari na kuhakikisha zinakuza uchumi wa taifa. (09.10.2020)

Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Emmanuel Bulayi akionesha vifaa mbalimbali zikiwemo simu za mkononi, makoti ya mvua, mizani na mabuti ambavyo wamekabidhiwa washiriki (hawapo pichani) wa mafunzo ya ukusanyaji wa takwimu za sekta ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani baada ya kuhitimu mafunzo ya siku mbili jijini Dar es Salaam. (09.10.2020)

Mkurugenzi wa Uratibu wa Sekta kutoka Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw. Yusuf Semuguruka, akizungumza na washiriki (hawapo pichani) wa mafunzo ya ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa mazao ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani yaliyofanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam na kubainisha kuwa TAMISEMI itahakikisha inafuatilia ili kufahamu namna mafunzo hayo yanavyoleta tija kwa maafisa uvuvi na viongozi wa BMU’s. (09.10.2020)

Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Emmanuel Bulayi na Mkurugenzi wa Uratibu wa Sekta kutoka Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw. Yusuf Semuguruka wakikabidhi vifaa vya kukusanyia takwimu kwa washiriki zikiwemo simu za mkononi, mizani, makoti ya mvua na mabuti. (09.10.2020)

Afisa Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani Bi. Antonia Mpemba, akionesha na kuwaelezea washiriki wenzake (hawapo pichani) wa mafunzo ya ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa mazao ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani namna mfumo wa kukusanya taarifa kwa kutumia simu ya mkononi unavyofanya kazi. (09.10.2020)

Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa mazao ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani wakipima uzito wa samaki kama sehemu ya mafunzo waliyopata, wakati walipotembelea soko la samaki katika mwalo wa Kunduchi jijini Dar es Salaam. (09.10.2020)

Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa mazao ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani walipata fursa ya kufanya mahojiano na wavuvi waliokuwa wakitoka baharani kuvua samaki kama sehemu ya mafunzo waliyopata ya kufahamu mahali ambapo mvuvi amevua samaki na muda aliotumia kuwa baharini, wakati walipotembelea soko la samaki katika mwalo wa Kunduchi jijini Dar es Salaam. (09.10.2020)

Picha ya pamoja ya washiriki wa mafunzo ya ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa mazao ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani wakiwa na baadhi ya maafisa kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, mara baada ya kumaliza masomo ya vitendo katika mwalo wa Kunduchi jijini Dar es Salaam. (09.10.2020)










Hakuna maoni:

Chapisha Maoni