Nav bar

Jumanne, 15 Septemba 2020

WATUMISHI WA WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI WATEMBELEA OFISI ZA ZVC, TVLA MKOANI IRINGA.

Watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakiongozwa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu, Bw. Zachariyya Kera walifanya ziara ya kutembelea ofisi za Kituo cha Huduma za Mifugo cha Kanda (ZVC) na Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Mkoani Iringa kwa lengo la kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na ofisi hizo.

 

Akiongea wakati wa ziara hiyo kwenye ofisi za ZVC na TVLA zilizopo Mkoani Iringa, (14.09.2020), Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu Bw. Zachariyya Kera alitoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwataka wafanyakazi kujua haki zao za msingi na kufuatilia kwa wakati.

 

"Watumishi waelimishwe kuhusu haki zao na wapate stahiki zao kwa wakati," alisema Bw. Kera.

 

Katika ziara hiyo Watumishi hao walipata fursa pia ya kutembelea Kiwanda cha Maziwa cha ASAS kilichopo Mkoani humo na kujifunza shughuli mbalimbali zinazofanywa katika kiwanda hicho.

 

Aidha, watumishi hao wa ZVC na TAVLA walitumia nafasi hiyo kumueleza Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu changamoto zinazowakabili ikiwa ni pamoja na upungufu wa watumishi, uhaba wa Rasilimali fedha na vitendea kazi.

 

Changamoto nyingine walizozitaja ni upungufu wa vyumba vya ofisi, upungufu wa mafunzo rejea kwa Watumishi wa kituo na kukosekana kwa vituo vya kukagulia wanyama.

 

"Kujengwa kwa machinjio kubwa ya nguruwe katika mji wa Mbeya katikati ya kanda ya nyanda za juu kusini kutasaidia kudhibiti magonjwa ya nguruwe katika kanda zingine," alisisitiza Bw. Dkt. Jeremiah Choga

 

Pia, watumishi hao waliiomba Wizara kuwa na mpango maalum ya utoaji wa mafunzo rejea kwa watumishi kuendana na kasi ya ukuaji wa sayansi na teknolojia, kuanzisha vituo vya ukaguzi wa wanyama, mazao ya wanyama na vyakula vya wanyama.

 

Meneja wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Dkt. Qwari Tluway Bura alieleza mpango kazi wao ikiwa ni pamoja na kusambaza chanjo kwa wafugaji, kutoa mafunzo ya ufugaji bora wa kuku wa asili, kutanua mtandao wa huduma za Maabara, udhibiti wa minyoo na magonjwa ya kupe kwa mifugo.

 

"Tutahamasisha wataalam wa Mifugo wa vijijini, kata au Wilaya pamoja na wananchi kwa ujumla kuleta sampuli za kupima ugonjwa wa kichaa cha mbwa katika mikutano ya hadhara,” Alisisiza Dkt. Bura

 

Aidha, Viongozi wa ZVC na TVLA waliishukuru Serikali ya awamu ya tano kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuendelea kuwahudumia wafugaji kwa kuviwezesha vituo kufanya kazi wakati wote.

Mkurugenzi wa Kiwanda cha Maziwa cha ASAS Mkoani Iringa, Bw. Fuad Abri akitoa maelezo kwa Watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhusu mashine zinavyofanya kazi kwenye Kiwanda hicho. (14.09.2020)

Mkaguzi na Mdhibiti wa Ubora kutoka Kiwanda cha Maziwa cha ASAS Mkoani Iringa, Bw. Shadrack Luhwago (kushoto) akitoa maelezo ya namna wanavyopima ubora wa Maziwa kwenye Kiwanda hicho kwa Watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi walipotembelea Maabara ya Kiwanda hicho. (14.09.2020)

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Zachariyya Kera (kushoto) akitoa shukrani kwa Mkurugenzi wa shamba la mifugo la Kibebe, Bw. Richard Philip kwa kukubali kuwapokea na kuwatembeza kwenye shamba hilo na kuona ufugaji wa kisasa. (14.09.2020)

Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Kulwa Zephania (wa tatu kutoka kushoto) akielekeza jambo nje ya ofisi ya Meneja wa Wakala ya Maabari ya Veterinari Tanzania (TVLA) Mkoani Iringa walipotembelea kujifunza na kujionea shughuli zinazoendelea katika ofisi hizo. (14.09.2020)

Mkurugenzi wa shamba la Kibebe Mkoani Iringa, Bw. Richard Philip (wa kwanza kulia) akiwaonyesha watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi maeneo ya shamba hilo lenye ukubwa wa hekari 1,200 ambalo lina jumla ya Mifugo 600, wafanyakazi 30, josho, mashine za kukamulia Maziwa pamoja na sola zinazosaidia katika kuendesha shughuli zinazoitaji umeme katika shamba hilo. (14.09.2020)

Watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakimsikiliza kwa makini Mkurugenzi wa Kiwanda cha Maziwa cha ASAS Mkoani Iringa, Bw. Faud Abri walipotembelea Kiwanda hicho. (14.09.2020)

Watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Kiwanda cha Maziwa cha ASAS, Bw. Fuad Abri Mara baada ya kutembelea kiwanda hicho kilichopo Mkoani Iringa. (14.09.2020)

Mkurugenzi wa Manunuzi na Ugavi, Bw. Emanuel Mayage akiangalia pikipiki pekee ambayo inatumika kwa shughuli za usafiri, nyingine ikiwa imearibika kwenye ofisi za ZVC Mkoani Iringa. (14.09.2020)

Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Mifugo, Dkt. Stanford Ndibalema (wa pili kutoka kulia) kutoka Wizara ya Mifugo na uvuvi (Mifugo) akifafanua jambo kwenye ofisi za Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) walipotembelea Mkoani Iringa. (14.09.2020)










Hakuna maoni:

Chapisha Maoni