Nav bar

Alhamisi, 17 Septemba 2020

WATENDAJI WA SHAMBA LA LANGWILA WATAKIWA KUZINGATIA TARATIBU ZA UPANDAJI MALISHO.

Mkufunzi Mkuu wa Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Kejeri Gilla amesema ni vema kufanya kilimo cha malisho ya mifugo kwa mzunguko katika eneo moja kwa muda usiozidi miaka mitano ili kuzalisha kwa wingi na kupunguza kiwango cha magugu.

 

Dkt. Gilla alisema hayo wakati wa ziara ya watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye shamba la malisho la Langwila lililopo mkoani Mbeya walipotembelea kujionea shughuli zinazoendelea shambani hapo.

 

"Tusibuni namna ya kuotesha malisho bali twende kwa utaratibu unaotakiwa na hii itasaidia kupata muda wa kurutubisha ardhi na kupata malisho yaliyo bora," Alisema Dkt. Gilla

 

Hata hivyo Dkt. Gilla amesema ili kuweza kuwa na mbegu bora ni vyema kuvuna kwa wakati, kuchakata na kuhifadhiwa vizuri ili kuepuka kuoza kwa mbegu na kuwa na utaratibu wa kuhakikisha ubora wa mbegu za malisho.

 

Aidha, alishauri kupitia Idara ya Uendelezaji wa Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo isaidie kutengeneza duka la malisho pembezoni mwa Barabara kuu ili kujitangaza na kusaidia watu kupata huduma kwa ukaribu zaidi na kuweza kuongeza pato la shamba na taifa kwa ujumla.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Bw. Amos Zephania alisema ili uzalishaji uwe bora na wa tija ni vyema wafugaji wakapewa elimu ya upandaji na ulimaji wa malisho kwa vitendo ili kuongeza ufanisi zaidi.

 

"Tunahitaji kutumia miundombinu yetu vizuri ili kuweza kujipatia fedha za kuendesha shamba letu kwa kukodisha matrekta kwa wakulima," Alisema Bw. Zephania

 

Aliongeza kuwa mikataba ya kukodisha matrekta kwa wakulima iandaliwe kwa kuonyesha idadi za ekari zilizokodishwa na kwa kiasi kilichopendekezwa.

 

"Mashamba yasikodishwe kwa kufikiria tuu bali ni vyema kuwasiliana, kupata mwongozo na ni vyema pia Katibu Mkuu Mifugo alifahamu hili ili kuondokana na migogoro isiyo ya lazima," Alisisitiza Bw. Zephania

 

Naye Meneja wa shamba la Langwila, Bw. Datus Ngerera Alexander aliwashukuru watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kufanya ziara shambani kwao na kupokea yale yote waliyofundishwa na kuelekezwa na kuahidi kuyafanyia kazi kwa wakati.

Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Steven Michael akichangia hoja wakati wa ziara ya kutembelea shamba la malisho la Langwila mara baada ya kutembelea stoo iliyojazwa mbegu za malisho na kushauri kuangalia namna bora zaidi ya kuhifadhi mbegu hizo. (16.09/2020)

Mkurugenzi wa Manunuzi na Ugavi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Emmanuel Mayage akikagua faili la kumbukumbu ya manunuzi ya vifaa kwenye shamba la malisho ya mifugo Lagwila, mkoani Mbeya walipotembelea shambani hapo. (16.09.2020)

Afisa Utumishi Mwandamizi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Andrew Ponda (katikati) akiwakumbusha watumishi wa shamba la Langwila juu ya ujazaji wa fomu za opras na umuhimu wake walipotembelea shamba hilo mkoani Mbeya. (16.09.2020)

Mchumi Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Ephron Sanga (kushoto) akipata maelezo ya namna ya kukusanya malisho, kuyafunga kwenye marobota na kuhifadhi kwa ajili ya kuuza. (16.09.2020)

Kaimu Mkurugenzi wa kituo cha Utafiti wa Mifugo Uyole, Dkt. Edwin Chang'a (wa nne kutoka kulia) akiwatembeza watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika maeneo mbalimbali ya kituo hicho wakati wa ziara yao mkoani Mbeya. (16.09.2020)

Afisa Mifugo Mkuu kutoka Wizara ya Mifigo na Uvuvi, Bw. Israel Kilonzo akifungua kikao cha kujadili namna wanaweza kusaidia shamba la malisho Langwila kufanya vizuri zaidi ikiwa ni pamoja na ushirikiano baina yao, walipotembelea shamba hilo lililopo mkoani Mbeya na kuona shughuli zinazoendelea. (16.09/2020)

Watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakiangalia ndama katika eneo lililotengwa kwa ajili ya ndama mara baada ya kuzaliwa ambapo hupewa huduma na uangalizi wa karibu. (16.09.2020)

Meneja wa shamba la malisho ya mifugo Langwila, Bw. Datus Ngerera Alexander akieleza namna mashine ya kukatia nyasi inavyofanya kazi kwa watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi walipotembelea shamba hilo mkoani Mbeya. (16.09.2020)

Mtunza Kumbukumbu Msaidizi kutoka Wizara ya mifugo na Uvuvi, Bi. Nsia Kileo akichangia mada kwenye kikao kifupi kilichofanyika kwenye shamba la malisho Langwila mkoani Mbeya. (16.09.2020)

Watumishi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakiwa kwenye picha ya pamoja na wafanyakazi wa shamba la mbegu za malisho ya mifugo Lagwila walipotembelea kujifunza na kujionea mazingira na shughuli zinazofanywa katika shamba hilo. (16.09.2020)

Kaimu Mkurugenzi wa kituo cha Utafiti wa Mifugo Uyole, Dkt.  Edwin Peter Chang'a akiongea na watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (hawapo pichani) walipotembelea kituo hicho wakati wa ziara yao mkoani Mbeya. (16.09.2020)

Watumishi wa Wizara ya mifugo na Uvuvi wakielekea kuangalia jengo kwa ajili ya Kiwanda kidogo cha uchakataji wa Maziwa ambalo bado lipo kwenye ujenzi kwenye kituo cha Utafiti wa Mifugo Uyole (TALIRI) mkoani Mbeya. (16.09/2020)













Hakuna maoni:

Chapisha Maoni