Nav bar

Jumatatu, 7 Septemba 2020

UAGIZAJI HOLELA WA MAYAI KUTOKA NJE YA NCHI, WAZIDI KUDHIBITIWA.

Watanzania wametakiwa kupenda bidhaa zinazozalishwa hapa nchini yakiwemo mayai ya kuku ili kukuza sekta ya ufugaji ikiwemo ajira huku serikali ikisisitiza mayai ya kuku wa kienyeji na kisasa ubora wake unatokana na mchanganyiko wa vyakula anavyokula kuku.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema hayo katika Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro mara baada ya kutembelea shamba la ufugaji kuku wa mayai Afro Farm Limited lenye kuku elfu ishirini (20,000) wenye uwezo wa kuzalisha mayai zaidi ya makasha (trays) 500 kwa siku, na kubainisha kuwa serikali imedhibiti uagizaji holela wa mayai kutoka nje ya nchi na sasa mayai yapo mengi nchini.

“Udhibiti uingizaji holela wa mayai kutoka nje ya nchi soko sasa limepatikana na niseme udhibiti huo siyo nguvu ya soda ni kwamba ni suala endelevu na tutaendelea nalo na tunazidi kujipanga lakini sasa lazima tuhamasishe watanzania kwamba wapende vya kwetu, ni suala ambalo kama wizara tumejipanga mayai yanaleta afya bora na tunapoelekea uchumi wa viwanda tunahitaji watu wenye afya bora.” Amefafanua Prof. Gabriel.

Kuhusu wafanyabiashara wanaotozwa tozo ya shilingi elfu moja (1,000/=) kwa kila kasha moja la mayai (tray) kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar Prof. Gabriel amesema tayari kanuni zimeshabadilishwa na tozo imepungua hadi shilingi mia moja (100/=) kwa kasha moja na kusisitiza wadau wa sekta ya ufugaji kulipa kodi ili serikali iweze kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo.

“Nitoe angalizo kwamba siyo vizuri sana mnapokuwa mnafikiria kuwa ifike mahali kwamba msilipe gharama yoyote kwa serikali, hilo hapana ni lazima mlipe kwa sababu mchango mnaotoa ndiyo unaojenga hospitali, barabara, shule n.k.” Amesisitiza Prof. Gabriel.

Aidha Katibu Mkuu Prof. Gabriel, ametoa wito kwa vijana kujiajiri katika sekta ya kuku kwa kuwa ni sekta ambayo ni rahisi na yenye mahitaji makubwa kwa watu kwa ajili ya nyama, mayai na mbolea huku akiwataka pia wafugaji wote watambue kwamba lazima waangalie mnyororo wa mapato, gharama na faida ili kupata kupata mafanikio makubwa na kuongeza ajira.

Pia amefafanua kuwa ni vyema wadau wa ufugaji wa kuku wa mayai kufuata kanuni bora za lishe ili waweze kuzalisha mayai bora badala ya kuwa na mayai mengi yasiyo na ubora na kubainisha kuwa kwa sasa Tanzania ina kuku milioni 83 na mayai bilioni nne huku mahitaji ya mayai yakizidi kuongezeka ndani na nje ya nchi.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka pia wafugaji kutumia Dawati la Sekta Binafsi lililo chini ya wizara hiyo kutatua changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo ikiwemo ya mitaji na miongozo kwa kuwa dawati hilo ni kiungo kati ya serikali na wadau wa sekta binafsi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Afro Farm Limited Bw. Remen Kweka amewataka vijana kubadilisha fikra zao kwa kuhakikisha wanajifunza pindi miradi mbalimbali inavyoanzishwa maeneo mbalimbali nchini ili kujiwekea mazingira ya kupata ajira na kubuni mitambo mbalimbali ya uzalishaji.

Bw. Kweka pia amewaasa wadau wa ufugaji wa kuku katika miradi mikubwa kutumia Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) iliyo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupeleka sampuli za vyakula vya kuku ili kuhakikisha kuku wanakula vyakula bora ambavyo vitatoa matokeo chanya ya upatikanaji mayai yaliyo bora ambayo yanaweza kushindanishwa katika soko la kimataifa.

Bi. Amillen Kweka ambaye ni mke wa mkurugenzi wa shamba la Afro Farm amesema mradi huo umewawezesha kusomesha watoto shule pamoja na kuwasaidia akinamama kutokata tamaa na kuwafundisha juu ya ufugaji wa kuku wa mayai huku Bi. Emma Kweka ambaye ni mtoto wa familia hiyo akiwaasa vijana kuwa na shauku ya kujifunza ili kutafuta zaidi na kujiajiri kwa kuwa kujiajiri ni jambo zuri ambalo unaweza kupangilia jambo lako katika muda unaotaka na kusisitiza bidii na mipangilio ya kazi.

Shamba la ufugaji kuku wa mayai la Afro Farm Limited kwa sasa lina kuku elfu ishirini (20,000) na kuzalisha mayai makasha (trays) zaidi ya 500 kwa siku, huku likiwa na uwezo wa kuhifadhi kuku elfu arobaini (40,000) na linatumia mitambo ya kisasa katika kulishia kuku, kukusanya mayai pamoja na mbolea.


Kutoka Kushoto: Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel, Bi. Amillen Kweka msimamizi wa Afro Farm Ltd, Mkurugenzi wa Afro Farm Ltd Bw. Remen Kweka, Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Stephen Michael na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Gabriel Bura, wakipata maelezo kutoka kwa Bw. Kweka namna shamba hilo linavyotumia mashine kukusanya mbolea ya kuku, kusambaza chakula na kukusanya mayai. (04.09.2020) 

 


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel (mwenye koti jeupe) akizungumza na Mkurugenzi wa Afro Farm Ltd, Bw. Remen Kweka, mara baada ya katibu mkuu kufika katika shamba hilo lenye kuku elfu ishirini ambao wanazalisha mayai makasha (trays) zaidi ya 500 kwa siku. (04.09.2020) 


Baadhi ya kuku wanavyoonekana wakiwa katika banda kwenye shamba la kufugia kuku wa mayai Afro Farm ltd, lenye kuku elfu ishirini (20,000) ilhali likiwa na uwezo wa kuhifadhi kuku elfu arobaini (40,000). (04.09.2020) 

 


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akikanyaga dawa maalum kabla ya kuingia kwenye banda la kufugia kuku wa mayai kwenye shamba la Afro Farm Ltd, anayemfuatia ni Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko katika wizara hiyo Bw. Stephen Michael. (04.09.2020


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel (mwenye koti jeupe), akiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Stephen Michael (wa kwanza kutoka kushoto) pamoja na familia inayomiliki Afro Farm Ltd, Bw. Remen Kweka (wa pili kutoka kulia) Bibi Amillen Kweka mkewe (wa pili kutoka kushoto) na mtoto wao Bi. Emma Kweka (wa kwanza kutoka kulia), wakionesha baadhi ya makasha (trays) ya mayai kufuatia ufugaji wa kuku wa mayai unaofanywa katika shamba hilo ambao unazalisha zaidi ya makasha 500 kwa siku. (04.09.2020) 

 



Muonekano wa nje wa banda linalotumika kufugia kuku wa mayai katika shamba la Afro Farm ltd lililopo Wilaya ya Hai, Mkoani Kilimanjaro. (04.09.2020) 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni