Nav bar

Ijumaa, 3 Julai 2020

WALIOWAUZIA WAFUGAJI NG’OMBE WASIYO NA SIFA WASAKWA.Serikali imeagiza kutafutwa kwa watu waliohusika kuwauzia kwa njia ya mkopo wafugaji ng’ombe wa maziwa waliozaa tayari na kuwahadaa wafugaji kuwa ng’ombe hao hawana uzao wowote (mitamba) ili wawapatie wafugaji ng’ombe wenye sifa kama walivyokubaliana katika mikataba.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema hayo katika Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga, wakati akikabidhi lori moja la kukusanyia maziwa lenye uwezo wa kubeba lita 15,000, keni za maziwa 50 pamoja na vifaa vingine vya kuboresha vituo vya kukusanyia maziwa wilayani humo kwa Chama Kikuu cha Ushirika cha Wafugaji wa Ng’ombe wa Maziwa Mkoa wa Tanga (TDCU) na kufafanua kuwa serikali imefanya kazi nzuri kuhakikisha wafugaji wanapata mikopo hiyo kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), hivyo lazima ihakikishe wafugaji hao wananufaika.

“Katika hatua ya upatikanaji wa ng’ombe mkajikuta mkaingia kwenye mitego ng’ombe ameshakuwa mkongwe halafu huku unaambiwa hana uzao wowote ilhali ng’ombe amezaa zaidi ya mara mbili, TDCU pamoja na vyama vya msingi hakikisheni wale waliowazuia ng’ombe wafugaji hawa wanafanya maboresho ili lengo la serikali liweze kukamilika najua mmeuziana baina yenu lakini hatuwezi kama serikali kukaa kimya lengo letu ni kuhakikisha mambo yanaenda katika unyoofu wake.”  Amesema Mhe. Ulega

Aidha Mhe. Ulega amefafanua kuwa endapo wafugaji hao wataendelea kuwa na ng’ombe hao watazidi kuwa masikini kwa kuwa watatumia nguvu kubwa kuwapatia malisho na dawa za mifugo ilhali ng’ombe hao wanatoa lita chache za maziwa tofauti na matarajio. 

Katika upande mwingine, Naibu Waziri Ulega amewataka pia wafugaji wa ng’ombe wa maziwa Mkoani Tanga, kuwa waaminifu kwa kuhakikisha wanapeleka maziwa ya kutosha TDCU ili maziwa hayo yaweze kutosheleza mahitaji ya kiwanda cha kuchakata maziwa cha Tanga Fresh ambacho kinapokea maziwa kupitia chama hicho.

Aidha kuhusu bima ya mifugo Naibu Waziri Ulega amefafanua kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi imefanya kazi kubwa kwa kushirikiana na Shirika la Bima la Taifa (NIC) ambapo tayari sera ya bima ya mifugo ipo tayari na kwamba ipo katika hatua ya mwisho kuzinduliwa mwaka huu ili ianze kutumika na kuwanufaisha wafugaji pindi wanapopata majanga mbalimbali ya mifugo yao.

Naye Mratibu wa Miradi kutoka shirika la kimataifa la Heifer Bw. Mark Tsoxo akizungumza juu ya Mradi wa Usindikaji wa Maziwa Tanzania (TMPP) uliowezesha kupatikana kwa lori la kukusanyia maziwa kwa TDCU lenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 170, amesema mradi huo nchi nzima unafadhili matenki 6 ya kuhifadhi maziwa yenye ujazo wa lita 24,000, kukarabati vituo 10, jenereta 7, ufadhili wa malori 5 ya kubebea maziwa pamoja na keni 250.

Bw. Tsoxo amefafanua kuwa kutokana na jitihada za mradi kwa kushirikiana na wasindikaji, ukusanyaji wa maziwa umeongezeka kwa zaidi ya lita 12,000 kwa siku kutoka kati ya mwezi Januari  lita 55,817 kwa siku hadi sasa lita 68,017 kwa siku.

Nao baadhi ya wafugaji waliopatiwa mikopo ya ng’ombe wa maziwa pamoja na ujenzi wa mabanda kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) wamefurahishwa na hatua hiyo huku wakiomba serikali na taasisi zingine kuwaboreshea zaidi mazingira ya ufugaji hapa nchini.

Kuhusu elimu juu ya ufugaji bora wa maziwa wafugaji hao wameiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia wataalam wa wizara hiyo, mikoa na wilaya kuhakikisha wanawatembelea wafugaji mara kwa mara ili kuwapatia elimu bora ikiwemo ya kilimo cha malisho bora ya mifugo.Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (kushoto) akikabidhiwa lori maalum la kukusanyia maziwa kutoka kwa Mratibu wa Miradi kutoka Shirika la Kimataifa la Heifer Bw. Mark Tsoxo, kwa ajili ya Chama Kikuu cha Ushirika cha Wafugaji wa Ng'ombe wa Maziwa Mkoa wa Tanga (TDCU). 

Muonekano wa lori la kukusanyia maziwa lililotolewa na Shirika la Kimataifa la Heifer kwa ajili ya Chama Kikuu cha Ushirika  cha Wafugaji wa Ng'ombe wa Maziwa Mkoa wa Tanga (TDCU). Lori hilo limegharimu zaidi ya Tshs. Mil 170. 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (wa tatu kutoka kushoto) akimkabidhi Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Wafugaji wa Ng'ombe wa Maziwa Mkoa wa Tanga (TDCU) Bw. Hamisi Mzee moja ya keni kwa ajili ya kubebea maziwa kwa chama hicho. 

Akizungumza na wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Wafugaji wa Ng'ombe wa Maziwa Mkoa wa Tanga (TDCU), (hawapo pichani) juu ya umuhimu wa Dawati la Sekta Binafsi lililo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi linaloongozwa na mratibu wa dawati hilo Bw. Stephen Michael (kushoto), Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe. Abdallah Ulega amewataka wafugaji kutumia dawati hilo ili kuwaunganisha na taasisi za kifedha kupata mikopo. 

Mkurugenzi wa Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Angello Mwilawa (kulia) akipatiwa maelekezo na naibu waziri wa wizara hiyo Mhe. Abdallah Ulega juu ya umuhimu wa kutoa elimu ya ufugaji kwa wafugaji wa Mkoa wa Tanga. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni