Nav bar

Jumanne, 21 Julai 2020

NARCO YAMSIMAMISHA KAZI MENEJA WEST KILIMANJARO


Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ranchi ya Taifa (NARCO), Masele Mipawa amemsimamisha kazi Meneja wa Ranchi ya West Kilimanjaro iliyopo Kilimanjaro, Hezron Kyaruzi kwa tuhuma za kukosa uadilifu kwa mali za Umma na kusababisha upotevu wa Ng’ombe takriban 32.

Akiwa katika ziara ya kutembelea Ranchi hiyo ya West Kilimanjaro Mipawa alisema kuwa waliamua kufanya maamuzi hayo kufuatia changamoto nyingi zinazolikumba shamba hilo ambazo kwa kiasi kikubwa zimechangiwa na uongozi mbovu wa meneja huyo.

“Kutokana na upotevu wa Ngombe, uzembe na ukosefu wa maadili tumeamua kumsimamisha kazi Meneja wa Ranchi na Msaidizi wake na hatua nyingine za kisheria na kinidhamu zitafuata ", alisema Mipawa

Mipawa alisema ziara hiyo aliyoifanya katika Ranchi hiyo ilikuwa na lengo la kufanya ukaguzi kutokana na taarifa walizokuwa wakizipata ambazo zilionesha kuwa katika shamba hilo kumetokea upotevu wa Ng’ombe ambao Kampuni ya NARCO haina taarifa nao.

Ziara hii pia imesaidia kubaini kuwa kuna wizi uliokithiri katika shamba hili ambao umechangiwa na mahusiano mabovu kati ya Meneja na jamii inayolizunguka shamba hilo, ukosefu wa maadili na uadilifu wa Meneja ambao umepelekea  Ngombe 32 kupotea.

Kati ya ngombe hao 32 waliopotea 15 wameshapatikana na wengine 17 hawajapatikana mpaka sasa huku ngombe wengine 27 walichinjwa bila kibali cha makao makuu, alifafanua Mipawa

Kufuatia hali hiyo, Mipawa alisema wameamua pia kumsimamisha kazi Msaidizi wake kwa kuwa alishindwa kumshauri vizuri meneja huyo huku ikidaiwa alikuwa akishirikiana na meneja huyo kwenda kuazima ngombe kwa watu binafsi ili Ranchi hiyo ionekane ina idadi kubwa ya ngombe.

Aidha, Mipawa aliwataka wafanyakazi wengine waliobaki katika shamba hilo kuendelea kufanya kazi kwa bidii, wazingatie nidhamu na uzalendo huku akiwaonya kuwa Serikali ya Awamu ya Tano haitavumilia mtu yeyote anayehujumu rasilimali za Taifa.



Kaimu Meneja Mkuu - NARCO, Bw. Masele Mipawa (aliyevaa suti nyeusi) akiongea na wafanyakazi wa Ranchi ya West Kilimanjaro wakati alipokwenda kuangalia maendeleo ya ranchi hiyo. (18.07.2020)



Kaimu Meneja Mkuu - NARCO, Bw. Masele Mipawa akiwa amepanda farasi ambao wapo katika ranchi ya West-Kilimanjaro wakati alipokwenda kukagua maendeleo ya ranchi hiyo. (18.07.2020)



Kaimu Meneja Mkuu - NARCO, Bw. Masele Mipawa akiongoza kikao cha watumishi wa Ranchi ya West-Kilimanjaro wakati alipokwenda kukagua maendeleo ya ranchi hiyo. (18.07.2020)

Kaimu Meneja Mkuu - NARCO, Bw. Masele Mipawa akiongoza kikao cha watumishi wa Ranchi ya West-Kilimanjaro wakati alipokwenda kukagua maendeleo ya ranchi hiyo. (18.07.2020)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni