Nav bar

Jumatatu, 11 Novemba 2019

CHANGAMOTO ZA ZAO LA MWANI ZATAFUTIWA UFUMBUZI




Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah jana (09.11.2019) amekutana na wabunge wa majimbo ya Ukanda wa Pwani jijini Dodoma kujadili jinsi ya kuendeleza na kuimarisha kilimo na biashara ya zao la mwani.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo Katibu Mkuu Dkt. Tamatamah amesema zao la mwani limekuwa mkombozi mkubwa kwa wakulima na wafugaji wadogo wadogo wa maeneo ambayo hapo awali walikuwa wakifanya shughuli za uvuvi na kilimo.

Aidha amesema baada ya mafanikio kuonekana kwenye ukuaji wa zao la mwani kampuni nyingi zimeanza biashara ya kulima na kusafirisha zao hilo nchi za nje.

Pamoja na hayo, imeelezwa kuwa kutokana na changamoto mbalimbali uzalishaji umeshuka na Tanzania sasa hivi ni nchi ya tatu, katika uzalishaji ambao umeshuka hadi kufikia tani 918 kwa mwaka 2018/2019 ukilinganisha na wastani wa tani 1,395 kwa mwaka 2017/2018, tani 1,197 kwa mwaka 2016/2017 na tani 1,500 kwa miaka ya 2000.

Aidha ametoa sababu za kushuka kwa uzalishaji wa zao la mwani ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya tabia nchi, ukosefu wa mitaji na wawekezaji makini, ununuzi wa mwani usiofuata utaratibu na kuleta migogoro baina ya wawekezaji na wazalishaji na kutokuwepo kwa soko la ndani.

Dkt. Tamatamah amewataka wabunge hao kutoka Ukanda wa Pwani kutoa maoni yatakayohakikisha biashara ya zao la mwani inafanyika kikamilifu kwa amani, uaminifu na kufuata sheria zilizopo ili wadau wote wanaojishughulisha kwenye mnyororo wa thamani wa zao hilo waweze kunufaika.

”Kwa upande wa serikali kupitia Wizara yetu tumechukua hatua mbalimbali kufanya tafiti zinazopunguza changamoto zilizopo na kuwajengea uwezo wakulima ikiwemo fursa za mikopo na kuongeza kasi kuwatafutia soko na kuona wakulima wa mwani wanaongeza kiwango cha ulimaji na uwezo wa ubunifu.” Amesema Dkt. Tamatamah.

Aidha amefafanua kuanzishwa kwa Dawati la Sekta Binafsi kumesaidia kwa kiasi kikubwa kuwakutanisha wakulima na wafugaji wadogo wadogo na taasisi za kifedha na imefanya vizuri na sasa kujikita zaidi kwenye zao la mwani.



Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ( Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah akielezea umuhimu na faida za zao la mwani kwa namna ambayo limekuwa mkombozi mkubwa kwa wakulima na wafugaji wadogo wadogo wakati akifungua warsha ya wabunge kutoka ukanda wa Pwani kwenye ukumbi wa NBC jijini Dodoma ili zao hili liweze changia zaidi pato la Taifa. (09/11/2019



Baadhi ya wabunge na wawakilishi wa wabunge kutoka katika ukanda wa Pwani wakimsikiliza kwa makini Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ( Uvuvi ) Dkt. Rashid Tamatamah ( hayupo pichani) wakati akifungua warsha ya kujadili namna ya kuendeleza na kuimarisha kilimo na biashara ya zao la mwani katika ukumbi wa NBC jijini Dodoma. (9/11/2019)




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni